Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu |
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepata mwaliko wa kukutana na Bunge la Ulaya pamoja na Chama tawala cha Christian Democratic Union of Germany (CDU) cha Ujerumani, kinachoongozwa na Angela Merkel. Ziara hiyo itakayowahusisha viongozi wakuu wa kitaifa itachukua siku 10 na itaanza leo. Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu (pichani), alisema, msafara huo utaongozwa na Mwenyekiti, Freeman Mbowe, ambaye atakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Bunge la Ujerumani, akiwamo Naibu Spika wa Bunge hilo na Mkurugenzi.
Mwalimu alisema kuwa mbali na kukutana na viongozi wa Bunge hilo, pia watapata fursa ya kuzungumza na Merkel. Viongozi wengine katika msafara huo ni Makamu Mwenyekiti Bara, Profesa Abdallah Safari; Mwalimu; Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), Patrobas Katambi; Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Grace Tendega na Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri, John Mrema, ambao watashiriki katika mkutano wa 27 wa CDU. Mwalimu alisema: “Ajenda ambazo viongozi hao watakwenda kuzijadili na wenzao wa Ujerumani ni pamoja na mchakato wa katiba, uchaguzi, wanavyopambana na ufisadi, ikiwamo kashfa ya fedha zilizochotwa katika akaunti ya Tegeta Escrow zaidi ya Sh. bilioni 300, ukiukwaji wa haki za binadamu, pamoja na tume huru ya uchaguzi.”
Mwalimu alisema anaamini chama hicho kitawawakilisha vyema Watanzania pamoja na vyama vingine vya upinzani hususani Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Kuhusu matumizi ya mfumo mpya utakaotumika katika uandikishaji katika daftari la wapiga kura (BVR), Mwalimu alisema anaamini watapata majibu ya uhakika kwa kuwa suala hilo kwa Tanzania linaleta utata. Aliongeza kuwa mwaliko huo ni fursa nzuri kwao ambayo itasaidia zaidi katika kudumisha uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi hizo.
Nipashe
No comments:
Post a Comment