C/HQ/ADM/PRESS/37 21/12/2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu
waandishi wa habari,
Tumewaita
hapa leo baada ya kupata fununu kuwa Rais Jakaya Kikwete anataka kutumia hotuba
yake ya kesho na wanaoitwa, “Wazee wa Dar es Salaam” kutetea wizi mkubwa wa
fedha za umma uliofanyika ndani ya Benki Kuu (BoT), kupitia Akaunti ya Tegeta
Escrow.
Tunazo
taarifa kuwa Rais Kikwete amejipanga kuuhadaa umma kwa kisingizio cha uchunguzi
wa Ikulu, ili kuwalinda watuhumiwa ambao wanapaswa kuwajibishwa kwa kuwafuta
kazi, kushitakiwa na kufirisiwa. Habari
tulizozipata kutoka ndani ya Ikulu kwenyewe, zinasema Rais Kikwete amejiandaa
kumlinda Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu
wa wizara hiyo, Eliakim Maswi.
Tunapenda
kumtahadharisha Rais Kikwete kuachana mara moja na mpango wowote wa kumlinda
Profesa Muhongo na Maswi, ambao hadi muda huu walipaswa siyo kuwa nje ya ofisi,
bali walitakiwa kuwako gerezani.
Ndugu
waandishi wa habari;
Umma
unafahamu kwamba anayejiita mmiliki wa kampuni ya PAP, alikabidhiwa fedha
zilizokuwa katika Akaunti ya Escrow, kabla ya kuwa mmiliki halali wa kampuni
hiyo.
Ushahidi
wa hili, unapatikana katika kesi iliyofunguliwa Mahakama Kuu ya Tanzania na
James Rugamalira, dhidi ya Gavana wa Benki Kuu (BoT), Prof. Benno Ndulu,
kampuni ya PAP na Benki ya Stanbic, tawi la Tanzania.
Rugamalira
alifungua shauri hili baada ya kukuta fedha zilizokuwapo kwenye akaunti ya
Escrow zimeshachukuliwa, wakati yeye akiwa bado hajamaliziwa kiasi chake cha
fedha alichokuwa anadai baada ya kuuza asilimia 30 ya hisa zake katika IPTL.
Katika
shauri hilo lililomalizika kwa njia ya usuluhishi wa mahakama, Mahakama Kuu ya
Tanzania, pamoja na mengine, ilisema yafuatayo:
Kwamba
baada ya kampuni ya VIP kulipwa fedha zake zilizotajwa katika mkataba, itailipa
Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) kodi yote ya mapato inayotokana na mkataba
inayofikia Sh. 38,
186,584,322/- (bilioni thelathini na nane milioni mia moja na themani na sita laki
tano na elfu themanini na nne na mia tatu ishirini na mbili) kama
zilivyokadiriwa na TRA kupitia Kadirio la Kodi Na. 427038820 la tarehe 15
Januari 2014.
Kesi
hiyo iliwasilishwa mahakamani tarehe 8 Januari 2014 na VIP ENGINEERING AND
MARKETING LIMITED (VIP) kama mdai na iliunganisha kesi za madai Na. 49/
2002 na kesi ndogo Na. 254 YA 2003.
Kwamba
baada ya VIP kulipa kodi hiyo kwa TRA, fedha zake zilizobaki hazitalipwa kwake
mpaka pale itakapowasilisha Cheti cha Kulipa Kodi na hati za kuhamisha asilimia
30 ya hisa zake katika IPTL kwa mwanasheria wa PAP, na wasilisho hilo
lilitakiwa kufanyika kabla ya saa 10 jioni ya tarehe 27 Januari 2014.
Aidha,
baada ya kulipwa kiwango chote cha mkataba kilichotajwa hapo juu, VIP
itathibitisha uridhiaji na ukubali wake wa kuhamishwa asilimia 70 ya hisa za
MECHMAR CORPORATION (MALAYSIA) BERHAD katika IPTL, na uridhiaji na ukubali huo
unarudishwa nyuma kuanzia tarehe ya mauzo na uhamishaji wa hisa hizo kwa PAP.
Ndugu
waandishi wa habari;
Hii
maana yake nini? Jibu ni kwamba, wakati PAP analipwa kiasi cha Sh. 321 bilioni
kutoka BoT, haikuwa mmiliki halali wa IPTL. Hakuwahi kusajili hisa zake BRELA
wala hakuwa amenunua asimia 30 ya hisa za VIP.
Huu
ni wizi ambao hauwezi kuvumiliwa na umma na chama chetu, ambacho ni tegemeo la
Watanzania katika kulinda rasimaliza za taifa, ikiwamo fedha na kutetea haki za
wanyonge na kusimamia misingi ya uwajibijkaji, hakiwezi kunyamaza na kumuacha
Rais Kikwete akitekeleza mradi wake wa kulinda wezi. Hakiwezi!
Kwa
msingi huo, tunamtaka Rais Kikwete katika hotuba yake ya kesho, kuwajibisha
wale wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine, katika kutekeleza wizi huo.
Miongoni
mwao, ni Prof. Muhongo, Maswi, Gavana wa BoT, Prof. Ndulu, Katibu Mkuu wizara ya
Fedha, Silviacius Likwelile, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Jaji Fredric Werema na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felicesmi Mramba.
Ndugu
waandishi wa habari,
Watanzania
bado wanakumbuka kauli iliyotolewa bungeni wakati wa mkutano uliopita kuwa
familia ya Rais Kikwete nayo iko nyuma ya sakata hili ikiwa mnufaikaji mkubwa
kupitia kwa mtu aitwaye Albert Marwa ambaye ana uhusiano na familia hiyo.
Kitendo
cha Rais Kikwete kushindwa kuchukua hatua madhubuti katika jambo hili, utakuwa
ni ushahidi wa wazi kuwa kigugumizi ambacho kimekuwa kikiikabili serikali yake
katika jambo hili kinasukumwa na jambo kubwa nyuma yake, ikiwamo kujilinda
binafsi na kulinda familia yake.
Ndugu
waandishi wa habari,
Suala
la miamala iliyofanyika kupitia Benki ya Stanbic katika sehemu ya kashfa hiyo
ya Akaunti ya Escrow, si suala la kufanyia mzaha au kupuuzwa hata kidogo katika
ufisadi huu.
Ni
kupitia benki hiyo ndiko kiwango kikubwa cha fedha zaidi ya Sh. 160 bilioni,
zilibebwa kwa magunia, malumbesa na sandarusi ndani ya siku moja mchana kweupe,
tena tunaambiwa wengine walikwenda kwa magari yenye nambari za serikali na
fedha hizo zilipelekwa Ikulu ambako Rais Kikwete anafanyia kazi na kuishi.
Ni
ukweli ulio wazi kuwa hakuna benki ndani ya nchi yetu inayoweza kufanya miamala
ya mabilioni ya fedha kwa kiwango hicho, bila BoT kuidhinisha. Kwa mantiki hiyo
hiyo, Gavana Prof. Ndulu hawezi kukwepa uwajibikaji kwenye jambo hili zito kwa
kuwa alilifahamu na kulilidhia.
Tunatarajia
Rais Kikwete ataueleza umma wa Watanzania hatua zilizochukuliwa dhidi ya
watumishi hawa wa umma na siyo kuja na visingizio vya miamala iliyochukuliwa
katika Benki ya Mkombozi.
Watanzania
wanasubiri kusikia Rais Kikwete anachukua hatua dhidi ya Waziri wa Fedha Saada
Mkuya Salum ambaye wakati fedha katika Akaunti ya Escrow zinatolewa kati ya Septemba
na Desemba mwaka jana, alikuwa ndiye Kaimu Waziri wa Fedha.
Wakati
huo, aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa alikuwa katika matibabu ya
ugonjwa uliopelekea kifo chake ambacho kimedaiwa kuwa na utata, nchini Afrika
Kusini.
Ndugu
waandishi wa habari;
Aidha,
katika kuwatafuta watu waliochukua fedha za Akaunti ya Escrow kwa magunia na
malumbesa, Rais Kikwete aweke wazi kile kinachoonekana ushirika wa ufisadi kati
ya serikali, Benki ya Stanbic na chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM),
kupitia Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulahman Kinana.
Tunazo
taarifa za uhakika kwamba Kinana alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo na
Mjumbe wa Bodi ya Stanbic, na ambaye alikuwa kiunganishi kikubwa kati ya
serikali, CCM na Benki katika kufanya miamala ya aina hiyo ya kifisadi.
Rais
Kikwete anatarajiwa kumwagiza Kinana awataje watu waliokwenda kuchukua
mabilioni ya fedha kwa malumbesa, magunia na sandarusi, vinginevyo atakuwa
anahalalisha madai haya kuwa ushirikiano huu si bahati mbaya na ndiyo maana,
fedha kutoka Akaunti ya Escrow ya Tegeta, zilipitia katika benki hiyo.
………………………
Arcado
Ntagazwa
MWENYEKITI WA BODI YA WADHAMINI
CHADEMA.
No comments:
Post a Comment