Wakati serikali ikiendelea kulalamikiwa kwa usiri wa mikataba ya gesi, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ameibuka na kusisitiza kuwa usiri huo utaendelea kwa sababu duniani kote mikataba ni siri kati ya serikali na mwekezaji aliyeingia naye mikataba. Prof. Muhongo alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam waliomuuliza ni kwa sababu gani serikali inakataa kuweka wazi mikataba ya gesi na mafuta kwa Kamati ya Bunge ya Hesabau za Serikali (PAC). “Mikataba yote duniani kote kuna kipengele cha sheria kinachoeleza kuwa ni siri kati ya serikali husika na mwekezaji, na kama serikali itaiweka wazi mikataba hiyo inaweza kushitakiwa na mwekezaji,” alisema. Alisema kiutaratibu kama serikali itahitaji kuitoa mikataba hiyo ni lazima iwasiliane na yule ambaye ilisainiana naye kwani masharti yakivunjwa, serikali inaweza kuingia katika matatizo ikiwamo kushtakiwa mahakamani.
Prof.Muhongo alisema hatua ya PAC kuomba mikataba ya gesi na mafuta kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) haikuwa sahihi kwa sababu mikataba hiyo siyo mali ya TPDC bali ni ya serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini. “Staili iliyotumiwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuomba mikataba hiyo haikuwa sahihi, kuna utaratibu wake na kimsingi, mikataba ni siri duniani kote, haiwezi kutoka hivi hivi,” alisema. Waziri huyo alisema baada ya PAC kutaka mikataba hiyo, TPDC iliandika barua katika Wizara ya Nishati na Madini kuomba idhini, lakini kulingana na taratibu za kisheria, aliomba ushauri kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambaye alihauri kisheria kwamba mikataba ni siri na haiwezi kutolewa. Prof.Muhongo alisema Watanzania lazima watambue kuwa siyo kwamba serikali inakataa kutoa mikataba hiyo, bali ni taratibu za kisheria kwamba mikataba ni jambo la siri duniani kote.
Tamko hilo la Wizara ya Nishati na Madini kuhusu usiri wa mikataba ya gesi na mfuta limetolewa katika kipindi ambacho PAC ikiwa imeandika barua ya kumtaka Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, awafungulie mashtaka Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TPDC), Michael Mwanda, na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, James Andilile. Vigogo hao walikamatwa na polisi hivi karibuni kisha kupelekwa rumande kwa saa kadhaa katika Kituo cha Kati cha Polisi jijini Dar es Salaam, kutokana na kukaidi maagizo ya kamati hiyo kutakiwa kuwasilisha mikataba 26 ya gesi iliyofikiwa kati ya serikali na wawekezaji. Hata hivyo, viongozi hao waliachiwa baadaye kwa maelezo kuwa PAC ilitakiwa kuzungumza kwanza na Ofisi ya Spika wa Bunge. Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe (pichani), wiki iliyopita alisema wameshamwandikia barua Spika Anne Makinda, aingilie kati wafunguliwe mashtaka kwa kudharau Bunge na kamati.
Nipashe
No comments:
Post a Comment