CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA), kimemshukia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Steven Wassira jimboni kwake Bunda na kuwaeleza wananchi namna alivyo kigeugeu na mbadhirifu wa msaka tonge. Aidha, kimempa pole Rais Jakaya Kikwete kwa kuumwa lakini wakapinga hatua yake ya kwenda kutibiwa Marekani kwa gharama kubwa wakati tatizo lake lingeweza kutibiwa kwenye hospitali za hapa nchini. Hayo yalisemwa juzi kwa nyakati tofauti na viongozi wa CHADEMA kwenye viwanja vya stendi ya zamani Bunda wakati wakihitimisha ziara ya Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA), kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa. Mbunge wa Viti Maalum, Chiku Abwao na Mratibu Uenezi wa BAVICHA, Edward Simbeye, kwa nyakati tofauti waliwaeleza wananchi hao kuwa Wassira amekuwa mbunge wao kwa vipindi zaidi ya viwili lakini ameshindwa kusaidia kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii kwenye jimbo hilo.
“Mbunge wenu ni msaka tonge tu, mimi namfahamu nilikuwa naye NCCR Mageuzi kabla hajaamua kwenda CCM. Hivi mnajua jimbo lenu ni miongoni mwa majimbo maskini sana nchini licha ya kuwa na mbunge ambaye ni Waziri,” alisema Abwao. Aliwataka wananchi hao kuamka na kuchagua viongozi wenye nia ya dhati kuwaongoza katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo, vinginevyo wataendelea kudidimia kimaendeleo kwa kuikumbatia CCM ambayo haiwajali wananchi maskini wa Tanzania.
Kunti amshukia Bulaya
“Wana CCM daima huimba kama malaika na kucheza kama masheni. Wanabadilika badilika, mimi Bulaya alinichosha kabisa siku nilipomsikia anaipigia chapuo Katiba pendekezwa huku akijua inaminya haki za wananchi wengi maskini wa Taifa hili,” alisema Kunti.
Heche amshukia Rais Kikwete
Mwenyekiti wa Taifa mstaafu wa BAVICHA, John Heche, alisema kuwa wamepokea kwa masikitiko taarifa za kuugua Rais Kikwete, lakini pia wamesikitishwa zaidi na hatua yake ya kuamua kutumia mamilioni ya fedha kwenda kutibiwa kwa gharama kubwa kitu ambacho kingeweza kutibiwa kwa gharama ndogo hapa nchini. Alisema kuwa Rais alipaswa kuwaonea huruma wananchi wake ambao kwa sasa wanakufa zaidi baada ya bohari ya dawa nchini,(MSD), kuacha kutoa dawa kwenye hospitali za serikali kutokana na deni kubwa wanaloidai.“Nianze kwa kumpa pole Rais na tunamuombea apone mapema, lakini tunasikishwa na uamuzi wake wa kwenda kutibiwa nje ugonjwa unaoweza kutibiwa hata na hospitali ya Mwananyamala…
“Angetibiwa hapa nchini angeokoa fedha nyingi anazotumia nchini Marekani na zingetumika kupunguza deni la MSD walau wangeweza kulegeza msimamo na kutoa dawa kwa hospitali za serikali…“Kwa kweli hali ni mbaya sana kwenye hospitali, nyie mnajua kabla ya MSD kugoma dawa zilikuwa tabu kupata, sasa walipoweka wazi kuwa hawatoi dawa na vifaa hali inakuwaje kwa sisi Watanzania maskini,” alihoji Heche. Alisema kuwa, wakati umefika kwa viongozi kuacha kukimbilia nje ya nchi kutibiwa maradhi yanayotibika hapa nchini na badala yake waboreshe hospitali zilizopo kwa kuweka vifaa vya kisasa, kwani wataalam wapo. Heche, alisema kuwa utaratibu wa viongozi kukimbilia nje kutibiwa ndiyo unawafanya wasifanye juhudi zozote za kuboresha sekta ya afya nchini, ambako imekuwa ikikabiliwa na changamoto lukuki.
Tendega alia na ugumu wa maisha
Katibu wa BAWACHA Taifa, Grace Tendega, alisema kuwa hali ya wananchi wa Tanzania kiuchumi inazidi kuwa duni kila kukicha huku viongozi wakiwa hawajali. Alisema mwaka 2005 wakati Rais Kikwete akiingia madarakani, aliahidi maisha bora kwa kila Mtanzania, lakini hali imekuwa tofauti kwani imekuwa maisha duni kwa kila Mtanzania. Alisema kuwa maisha ya wananchi hayawezi kuboreshwa na viongozi kuzunguka duniani kutafuta misaada, bali inabidi kuwe na mipango mizuri ya kutumia rasilimali zilizopo hapa nchini. “Tanzania kama Taifa sisi si maskini hata kidogo, tunakosa uongozi madhubuti utakaosimamia rasilimali zetu ziweze kutunufaisha, haiwezekani nchi yenye dhahabu, almasi, tanzanite, uraniam, mbuga za wanyama, mlima Kilimanjaro bado tukawa maskini…
“Na hili mzee Warioba (Joseph), na tume yake (Tume ya mabadiliko ya katiba), waliliona wakaamua kuweka kipengele kwenye katiba wakitaka wananchi walio kwenye maeneo yenye rasilimali hizi wazimiliki na watambulike kama wabia, lakini wabunge wa CCM wakaamua kukiondoa,” alisema Tendega.
Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment