TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UKATILI WA CCM WAMREJESHA KIWIA HOSPITALINI INDIA
Taarifa inatolewa kwa vyombo vya habari kuwa hali ya Mbunge
wa CHADEMA Jimbo la Ilemela, Highness Kiwia ambaye amekuwa akihudhuria matibabu
ndani na nje ya nchi tangu alipovamiwa, kushambuliwa, kupigwa kwa visu na mashoka
na vijana wa ulinzi wa CCM (Green Guard), usiku wa kuamkia Aprili Mosi, 2012,
imebadilika hivyo ameshauriwa kurejea kwa haraka tena nchini India kwa ajili ya
matibabu.
Madaktari wa Hospitali ya Doctor’s Plaza ambao wamekuwa
wakimuuguza kwa kipindi sasa baada ya matibabu aliyopewa nchini India mara
baada ya tukio hilo la kutisha, wamemshauri Kiwia arejee nchini India baada ya
kuona bado hali yake haijatengemaa na anahitaji uangalizi wa hospitali ya Apollo
iliyomtibu awali.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam siku ya Jumanne Septemba 30,
muda mfupi kabla ya kuondoka kuelekea India, Kiwia ameelezea masikitiko yake
kwamba pamoja na kwamba yeye bado yuko kwenye kipindi kigumu cha maumivu
makali, miaka miwili tangu baada ya tukio lile alilosema lilikuwa la tishio
kubwa la uhai wake, hadi leo hakuna hatua yoyote imewahi kuchukuliwa kwa
watuhumiwa aliosema wanajulikana kwa majina na sura.
“Nimelazimika kuondoka kwa dharura kwenda India tena kwa
ajili ya matibabu. Nimeshauriwa hivyo na madaktari wa Doctor’s Plaza ambao
wamekuwa wakinihudumia kwa muda sasa. Baada ya kunichukua vipimo, wameaniambia
niende India kule kule nilikotibiwa awali baada ya lile tukio la kutisha ambalo
adi leo sijui niliponaje.
“Ni jambo linaloumiza na kusikitisha sana. Kwamba haki
inaweza kutolewa kwa double standards kwa kiwango hiki. Kwamba wale watu
waliotushambulia tukiwa na wenzangu akiwemo Mbunge Machemli (Sylvester), kwa
marungu, mapanga na mashoka kwa nia ya kutuua wapo, wanajulikana kwa majina na
sura, lakini hakuna hatua yoyote imewahi kuchukuliwa dhidi yao.
“Inauma na kusikitisha zaidi kuwa tukio lile lilitokea mbele
ya askari polisi wenye bunduki. Vijana wale wa CCM walifanya tukio lile zima la
kinyama, kututeka na kutaka kutuua mbele ya askari polisi ambao tulikuwa
tukiwaomba msaada. Lakini walikuwa wakiangalia kama vile ni sinema au maigizo
ya kutoa uhai wa watu. It was terrible and horrific. Hivi kweli kitendo hiki
angekuwa amefanyiwa mbunge wa CCM haki ingetolewa kwa double standards namna
hii inavyofanyika kwetu,” amesema Kiwia kwa masikitiko.
Mbali ya kuwaambia wananchi wa Jimbo la Ilemela kuwa atarejea
kutoka India na kuendelea kuwatumikia, amesema kuwa atakaporejea kutoka kwenye
matibabu anakusudia kulishughulikia tukio hilo kwa namna aliyosema itakuwa ni tofauti
na ambayo imekuwa ikitumika sasa katika kusaka haki na hatua dhidi ya wahusika.
“Bunge huwa wanatoa wiki moja kwa ajili ya safari ya
matibabu. Lakini mwisho wa siku watakaoamua nirejee lini ni madaktari wa
Apollo. Nina matumaini nitarudi nikiwa na afya njema kuendelea kuwatumikia
wananchi wa Ilemela,” amesema Kiwia huku akiugulia maumivu makali katika mfumo
wa hewa, kichwani (alikokatwa mapanga, shoka na kupigwa marungu) na moyo, huku
pia akisema ile hali ya kupatwa na ganzi iliyokuwa ikimwandama siku za awali
baada ya tukio lile, imekuwa ikimrejea.
Imetolewa leo Jumanne,
Septemba 30, 2014 na;
Idara ya Habari ya
CHADEMA
No comments:
Post a Comment