Yamebakia masaa 24 ya muhimu katika uchaguzi mdogo wa Kalenga.
Uchaguzi huu ni fursa ya wananchi wa jimbo hili kuwakilisha hisia za mamilioni
ya Watanzania wanaowaka moto na kueneza joto la mabadiliko nchi nzima.
Kama ulivyo uchaguzi mwingine wowote mdogo, hasa unaohusisha
CHADEMA na CCM, uchaguzi huu umepata hadhi yake ya kuvuta attention ya kitaifa
na kuwa moja ya mijadala katikati ya mijadala mikubwa ya kitaifa inayoendelea
nchini.
Uchaguzi huu utakuwa kipimo cha demokrasia...itapima ukomavu wa
demokrasia ya vyama vingi, lakini kikubwa zaidi ni kipima joto kizuri kuelekea
uchaguzi mdogo wa Chalinze, serikali za mitaa na kiasi kikubwa sana, sana
utakuwa mwelekeo wa uchaguzi mkuu mwaka kesho.
CCM wamepotezwa kabisa. Si hadharani, wala kwenye 'yale mambo
yao' mengine, hasa usiku.
Yakiwa yamebakia takriban masaa 48 ya muhimu kwa wananchi wa
Kalenga wafanye maamuzi ambayo yatawashangaza watawala na cronies wao, polisi
sasa wamelazimika kuingia/zwa mstari wa mbele kujaribu kuokoa jahazi.
Hawatafanikiwa.
Muda mfupi uliopita, RPC Mungi amemaliza kufanya mkutano na
waandishi wa habari, central theme ya press conference yake, ilikuwa ni chopa,
usafiri unaotumiwa na viongozi wa CHADEMA na mgombea wake, kurahisisha kufikia
maeneo mengi kwa urahisi ndani ya muda mfupi na hivyo kuwafikia wapiga kura
wengi zaidi.
Usafiri huo ndiyo utatumiwa na mgombea siku ya kupiga kura,
kwanza atakwenda kupiga kura, kisha atazunguka kukagua vituo vya kupigia kura
na kuangalia namna shughuli ya upigaji kura inavyokwenda. Anaruhusiwa kufanya
hivyo kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi.
Sasa kwa RPC hiyo imekuwa nongwa. Bila msingi wowote wa kisheria
ameibuka leo, bila shaka kwa shinikizo la CCM, akisema watazuia chopa ya
CHADEMA kuruka siku hiyo. Sababu aliyotoa, eti itakuwa inawapigia kelele wapiga
kura!
Uhakika uliopo ni kwamba CCM, wameamua kujaribu kupitia kwenye
dirisha hilo la mabavu ya polisi, badala ya sheria, baada ya Mwenyekiti wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damian Lubuva 'kuwakatalia' CCM
kikaoni.
Mwakilishi wa CCM, kwenye kikao cha Jumanne, aliomba tume izuie
matumizi ya chopa siku ya kupiga kura akisema kuwa ni sehemu ya kampeni kwa
sababu kila mtu anajua kuwa helkopta ni usafiri wa CHADEMA, hivyo eti itakuwa
inawakumbusha wapiga kura 'kapigie CHADEMA...kapigie CHADEMA...'.
Jai Lubuva, kwa uwazi kabisa, akaonekana kutoka kuingizwa mkenge
kwenye suala ambalo asingeweza kupata mwanya wa kutokea katika sheria. Akasema
wao hawawezi kuzungumzia nani atatumia usafiri gani, maana mwingine anaweza
kutumia hata punda, akasisitiza wao watasimamia masuala ya msingi yanayohusu
sheria za uchaguzi.
Nguzo pekee iliyobakia kwa CCM, wamekimbiza suala hilo kwa RPC
ili awaokoe, ambaye naye kakurupuka kuwa ngao yao. Labda aulizwe hivi;
1. Usafiri wa aina yoyote ile (bila kuwa na nembo ya chama au
mgombea) kwenye kampeni ni moja ya campaign materials?
2. Uko wapi msingi wa kisheria wa zuio lake hilo? Anataka
uchaguzi uendeshwe kwa hisia na utashi wake?
3. Je, zuio lake hilo pia litakwenda kwa CCM kuwazuia wasitumie
magari yao yale wanayoyatumia siku zote na watu wengi wanajua ni magari ya CCM?
4. Atamzuia mgombea wa CCM kutumia magari yao kuzunguka kukagua
zoezi la uchaguzi?
Ni vyema RPC aandae kombora la kutungulia ndege...ili aitungue
helkopta hiyo ya CHADEMA kama anafikiri mgombea kuitumia kurahisisha usafiri
anavunja sheria.
Usafiri wa namna hiyo hiyo umetumika maeneo mengi siku ya kupiga
kura ikiwemo wakati wa uchaguzi wa Arumeru Mashariki, ambako pia kulikuwa na
polisi, CCM na wapiga kura waliokuwa wanajua kuwa chopa ni 'brand' ya CHADEMA!
Hata maeneo aliyokuwa anatumia RPC kwenye press conference leo
yalikuwa yamejaa ushabiki tupu, kuibeba CCM. Amediriki hata kupuuza namna
ambavyo CCM walimpiga padri, wakatishia kuchoma nyumba ya masister, wakatishia
kuchoma nyumba ya Shehe Ismael pale Magulilwa na kumchoma kiongozi wa CHADEMA
kisu cha moyo. Kwa sababu ya CHADEMA.
RPC wa Iringa na RCO, fanyeni kazi zenu za kusimamia uchaguzi wa
Kalega kwa msingi wa sheria, si shinikizo la CCM (kama walivyokuja jana pale
kituoni usiku) ambao wameshaonja joto la kushindwa kwenye uchaguzi huu.
Tukio la leo, limedhidi kudhihirisha kuwa hata nia ya jana la
kutaka kwenda kukagua kambi za CHADEMA bila search warrant halikuwa na nia
njema. Watu makini wangeweza tu kuwauliza swali rahisi, mmefanya hivyo kwa CCM,
ambao Katibu wao wa Iringa amewaambia watu kuwa wanatembea na SMG 34 kwenye
magari yao?
*Kwa wale wasiomjua RCO wa Iringa vs CHADEMA
Alikuwepo wakati wa tukio la Nyololo ambapo aliyekuwa RPC wa
Iringa, Michael Kamuhanda, alisimamia mauaji ya mwandishi wa habari, Daudi
Mwangosi.
Kabla RPC Kamuhanda hajafika eneo la tukio, aliyekuwa
'anapiganisha' ni RCO, ambaye baada ya mabishano ya muda mrefu na viongozi wa
CHADEMA, hasa kwa kutumia misingi ya Sheria ya Vyama vya Siasa, Sheria ya Jeshi
la Polisi, Sheria ya Sensa, precedence zingine (kama mkutano wa CCM uliokuwa unafanyika
siku hiyo Bububu na maandamano ya wanaCCM Iringa), alionekana kuelewa.
Wakati huo watu wengi walimchukulia RCO huyo kuwa ni mtu
anayefanya kazi zake kwa mujibu wa sheria...wengine wakaenda mbali na kusema ni
kwa sababu ni mwanasheria kitaaluma.
Kwa hakika kabisa siku hiyo RCO aliepusha maafa makubwa.
Askari wale aliokuwa 'akiwapiganisha' wakiwa pamoja na Mkuu wa
FFU Mkoa wa Iringa, walionekana kuwa na uchu wa kushambulia, kupiga, kuumiza na
pengine labda kuua, lakini alikuwa akisikika mara kadhaa akiwaamrisha askari
wale kwa kuwaambia 'move...move...move...stop...stop...stop...rudi nyuma...rudi
nyuma...
Hata kitendo cha yeye kuamua kuondoka baada ya RPC Kamuhanda
kuingia na kuanza kutoa amri, kilitafsiriwa na watu wengi kuwa ilikuwa ni
kuonesha kutoridhika na maagizo ya mkuu wake kuwataka CHADEMA wasiendelee
kufanya vikao vya ndani. Kinyume kabisa na sheria.
Lakini chaguzi kadhaa ndogo za madiwani zilizofanyika mkoani
Iringa tangu baada ya kuuwawa kwa Mwangosi, RCO amedhihirisha kuwa ni 'wale wale'.
Uchaguzi wa hivi karibuni wa kata 27, ambapo Iringa kulikuwa na kata 2, hasa
baada ya kumtishia kijahili Mbunge wa Viti Maalum, Chiku Abwao na makamanda
wengine wa CHADEMA, ulidhihirisha mambo kadhaa kuhusu RCO;
1. Ameamua kuwa wale wale
2. Ametishwa
3. Ame-compromise, badala ya kutenda haki, bila upendeleo kwa
kusimamia sheria.
4. Naye amejiunga na askar polisi wanaoanza kuona kuwa
'ukishughulikia' CHADEMA, ukavunja haki za binadamu na sheria, inakuwa ni ngazi
ya kukupandisha au kupandishwa kwenye 'utukufu' wa kidunia ndani ya jeshi hilo.
Walioko Iringa wanajua kuwa command ya mwisho ya polisi walioko
kwenye operesheni ya uchaguzi wa Kalenga, kwa sasa haiko kwa watu hao wawili
pekee, lakini bado wana mchango na msaada mkubwa kwa wakubwa wao na askari
wengine kibao waliopelekwa huko.
Watende haki, wasimamie sheria, waache ushindani wa kisiasa uwe
kati ya CHADEMA na CCM, uwe kati ya tumaini jipya na tumaini linalofifia,
uwekati ya uadilifu na ufisadi, uwe kati ya wapigania haki na sheria dhidi ya
udhalimu na ukoloni mweusi.
Wananchi wa Kalenga waamue, si waamuliwe.
Kurugenzi Ya Habari CHADEMA
No comments:
Post a Comment