Bunge Maalum la
Katiba limeendelea kugawanyika kutokana na wajumbe kutoafikiana kuhusu
utaratibu wa kupitisha vifungu vya Rasimu ya Kanuni za Bunge hilo, huku
Mwenyekiti wa Muda, Pandu Ameir Kificho, akitaka rasimu hiyo ipitishwe kwa
kuhojiwa kwa uwazi wanaosema ‘ndiyo au hapa.’
Hali hiyo ilianza kujitokeza
jana asubuhi baada ya Kificho kuwaeleza wajumbe kuhusu utaratibu utakaotumika
kuboresha Rasimu ya Kanuni hiyo.
Akiwa amechelewa kwa muda wa dakika 45 wakati
lilitakiwa kuanza saa 4:00, Kificho alisema: “Tumechelewa kuanza kwa sababu
tulikuwa na kikao na Mwenyekiti wa Kamati ya Kumshauri Mwenyekiti wa Muda
kuhusu Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalum, Profesa Costa Ricky Mahalu.
”
Pia
alisema: “Tulichokubaliana na Mwenyekiti wa Kamati, twende sura kwa sura ili
tupate mwelekeo panapohitaji marekebisho yawekwe vizuri kwa kuchapishwa au
kuandikwa kwa mkono...wenye marekebisho wayaandike na kuyawasilisha kwa kamati
kabla ya saa 7:00 na kamati itayawasilisha kwenye semina hii saa 11:00 jioni
(jana).
“Unapofanya kazi ambazo hazina utaratibu (kanuni) lazima ufikiri
utaratibu utakaofaa kutumika, baada ya kujadiliana na Profesa tumeona utaratibu
huu unafaa kutupitisha eneo hilo na pia yakizungumziwa humu bungeni
yatachukuliwa kwenye hansard kwa ajili ya kumbukumbu.”
Alisema wakirejea saa
11 jioni (jana) watapitisha marekebisho na vifungu vya rasimu hiyo.
SENDEKA
Baada
ya Kificho kutoa utaratibu huo, Mjumbe Christopher Ole Sendeka, aliunga mkono
utaratibu uliotolewa na Mwenyekiti wa kuwapa muda wajumbe kuandika marekebisho
na kuyawasilisha kwa wakati aliosema kwani utaweka utaratibu mzuri na
kutopoteza muda.
“Vinginevyo kila mjumbe akitaka kuzungumza hapa akisema ondoa
kifungu hiki na weka hivi na wajumbe wakiwa zaidi ya 50 wakaomba kutoa maoni
katika kifungu kimoja tutakaa hapa bila kumaliza,” alisema.
Akizungumzia
kuhusu Ole Sendeka, Kificho alisema alichofanya mjumbe huyo ni kuunga mkono
wazo lililotolewa awali la kuwataka wajumbe wawasilishe mapendekezo yao
kimaandishi, vinginevyo itakuwa ngumu kufikia mwafaka.
KAWAWA
Kwa
upande wake, Vita Kawawa, alisema wiki iliyopita wachangiaji walitoa
mapendekezo ya vifungu mbalimbali na kamati ilitolea ufafanuzi vifungu vyenye
maelezo makubwa tu lakini haikutoa ufafanuzi kwa mawazo ya watu wachache.
“Majumuisho
yaliyotolewa kwenye kamati yalikuwa ni akidi, kura za siri au wazi, hoja
kinzani, uwasilishaji na matokeo, hivyo tunaomba kamati izingatie sana mawazo
ya vifungu vya wachache,” alisema.
MANYANYA
Mjumbe mwingine, Stella
Manyanya, alisema kuna baadhi ya mambo ambayo yalitolewa ufafanuzi vizuri na
kamati ya Profesa Mahalu wiki iliyopo na wajumbe baadhi waliyapokea kwa mtazamo
chanya.
“Lakini tulipowaomba waende wakatuandike tumekuja kuona kuna mambo
tofauti kabisa ya vile ambavyo walikuwa wametolea ufafanuzi. Sasa mimi naanza
kupata wasiwasi na kamati yenyewe,” alisema na kuongeza:
“Tunataka tupate
nakala za hansard ili tufanye ulinganisho wa yale yaliyochangiwa bungeni na
rasimu hii,” alisema Manyanya.
Hata hivyo, Mwenyekiti Kificho alisema mjumbe
ambaye ameona kwamba hoja yake imeripotiwa tofauti kwenye rasimu hiyo basi
anaweza kuomba nakala ya hansard na siyo kwa wajumbe wote.
MWIJAGE
Charles
Mwijage, aliunga mkono pendekezo la kuwataka wajumbe wawasilishe mapendekezo
yao kimaandishi, lakini alishauri kwamba wafanye hivyo ukurasa hadi ukurasa.
OLUOCHI
NA DOVUTWA
Wajumbe Fahmi Dovutwa na Ezekile Oluochi, walitaka kamati
izingatie hoja za makundi ya watu wachache ili sauti zao ziweze kusikika.
Walisema
kwa muda mrefu makundi hayo hayajasikika.
NZEMBA
Mjumbe kutoka kundi la
watu wenye ulemavu, Vinvent Nzemba, alisema kamati iwahakikishie yale
watakayoyawasilisha kimaandishi kama taarifa zao zitajumuishwa kwani awali
walifanya hivyo, lakini hazijajumuishwa.
DK. MICHAEL
Dk. Francis
Michael, aliunga mkono mawazo ya Sendeka na Oluochi ya kuwasilisha
mapendekezo yao ukurasa kwa ukurasa wa Rasimu ya Kanuni, lakini akataka kujua
namna gani wanaweza kupiga kura.
“Napenda tujue hapa tutakapofika kwenye
kupiga kura tunafanyaje, tumekuwa tukizungumza uwazi na siri kwa siku nzima,
hivyo ni vema tukalimaliza hapa kabla hatujatoka,” alisema.
GHASIA
Mjumbe
Hawa Ghasia alimtaka Mwenyekiti kuahirisha kikao hadi jioni ili wajumbe wapate
muda wa kuandika marekebisho yao na kuyawasilisha.
“Uturuhusu kupata muda,
vinginevyo hatutafikia mwafaka hapa bila kuandika, huo ndio utaratibu wa
Bunge,” alisema.
ADHARI YA KIFICHO
Mwenyekiti Kificho alisema:
“Unaipitishaje rasimu. Ili iwezekane kuifanya practically (kwa vitendo) mimi
nitawauliza, "kifungu hicho kimeafikiwa, nanyi mtajibu ndiyo au hapa.”
“Lile
la uwazi au siri tukitaka lianze kwenye rasimu hii hatutafika. Nataka rasimu
ile (Rasimu ya Katiba) ndiyo tuanze. Tuliangalie kiutendaji wake, hili jambo
hili mnalolizungumza lina uzito mkubwa sana,” alisema na kuongeza:
“Vipo
vifungu 87 katika rasimu hii, sasa niwaambie makatibu watayarishe karatasi za
kura kwa wajumbe 600 kwa kila kifungu ni kazi kubwa sana.”
LIPUMBA
Profesa
Lipumba, alisema dhamira ya kura ya wazi au ya siri ni muhimu sana na
wanatakiwa kufikia mwafaka kwanza kuhusu dhamira hiyo.
Alinukuu kifungu cha 4
cha Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalum kinachozungumzia uhuru wa mawazo na maoni
katika mijadala ya Bunge Maalum.
Pia alisema kifungu hicho kinataka kila
mjumbe wa bunge hilo kutekeleza majukumu yake kwa uhuru na hatashurutishwa na
kwamba hatashinikizwa wala kupokea maelekezo kutoka kwa mtu au chombo chochote.
Lakini,
alisema kwa hali ilivyo bungeni humo imekuwa tofauti na akataka suala la kura
ya siri au uwazi ni jambo la msingi katika kupitisha vifungu.
“Haiwezekani
suala kwamba tunapigaje kura lipitishwe kwa kuulizwa wabunge, je,
mmekubali au ama hamkubali. Ni jambo la msingi lipitishwe kwa maridhiano
ya kidemokrasia,” alisema na kuongeza:
“Misingi ya kidemokrasia inaweza
kuwalinda watu wanaodhani kwamba kutakuwa na vitisho.”
“Utaratibu wa kidemokrasia
ni kuwa na kura ya siri inayoonyesha dhamira ya kila mjumbe,” alisema na
kuongeza: “Hali imeonyesha tayari kuna shurutisho kwa maelekezo ya kichama.”
Ippmedia/Nipashe
No comments:
Post a Comment