Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Saturday, March 8, 2014

CCM waanza kuviziana bungeni

Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wakiwa kwenye foleni ya kuchukua posho za vikao, Dodoma juzi. Picha na Silvan Kiwale       
          Mpasuko miongoni mwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), umechukua sura mpya, baada ya kuelezwa kuwa wabunge 90 wameorodheshwa kwa lengo la kuhojiwa kwa tuhuma za kukisaliti chama. Wajumbe hao wengi wao wakiwa ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wamekuwa wakiitwa na mmoja wa viongozi waandamizi wa Serikali ya CCM na kuelezwa wazi kuwa chama hakiridhiki na mwenendo wao. Wengi wa wajumbe hao ni wale waliotamka hadharani kuunga mkono muundo wa Muungano wa Serikali tatu, badala ya Muungano wa Serikali mbili ulioboreshwa, ambao ndiyo msimamo wa chama hicho tawala. Wengine ni wale wanaotajwa kuunga mkono upigaji wa kura wa siri katika kupitisha vifungu vya rasimu ya Katiba Mpya, ikiwa ni kinyume na msimamo wa CCM wa kutaka kura ya wazi.
     “Ni kweli hata mimi niliitwa na (akimtaja jina) na kuniambia ametumwa aniletee ujumbe kuwa niko kwenye orodha hiyo na nikiendelea na msimamo huo nitachukuliwa hatua,” alidai mbunge mmoja. Hata hivyo, mjumbe huyo alidai kuwa kinachofanywa na CCM ni sawa na kumpa mgonjwa wa saratani dawa ya kutuliza maumivu, lakini mwishowe ugonjwa alionao uko palepale. “Mimi msimamo wangu ambao naamini ndiyo msimamo wa wabunge wengi ni kutaka kura ya siri na Serikali tatu. Nitasimamia msimamo huo, kwani ndiyo dhamira yangu kwa masilahi ya Watanzania,” alidai. Mbunge mwingine anayetajwa kuwapo kwenye orodha hiyo (jina tunalo) alipoulizwa jana kama ana taarifa hizo alisema, “Ni kweli kuna orodha hiyo ya wabunge 90, lakini mimi sijaulizwa chochote.”
      Mbunge huyo alisema, wabunge hao 90 wamewekwa katika orodha nyeusi (Black list) iliyoandaliwa na CCM kimeandaa kama njia mojawapo ya kuwatesa kisaikolojia ili waachane na msimamo wao. Tayari CCM kupitia kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kilishaweka wazi msimamo wake kuhusu suala la muundo wa Serikali na kutaka wajumbe wake watetee kwa nguvu zote muundo wa Serikali mbili.
Nape: Huu ni uwongo
     Nape alipoulizwa jana kuhusu kuwapo kwa orodha hiyo, alikanusha na kusema huo ni uongo ambao hata shetani ataona aibu kuusema. Chama hakina mpango wa kuwahoji, alisema na kuongeza; “Msimamo wa Serikali mbili siyo wa mtu mmoja mmoja, ni msimamo wa CCM na msimamo wa Watanzania wengi…. Kama kuna haja ya kuwahoji wanaounga Serikali tatu watahojiwa na wapiga kura wao.”
Ngoma nzito kura ya siri
        Wakati CCM wakifanya uamuzi huo, Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu la Katiba, Pandu Ameir Kificho, ameunda kamati ya maridhiano itakayosaidia kufikia mwafaka wa kanuni zenye utata na zilizua mabishano makali bungeni, ikiwamo upigaji kura na Muundo wa Muungano. Akizungumza bungeni mjini jana, Kificho alisema kamati hiyo imeundwa kwa ajili ya kutafuta maridhiano katika maeneo ya kanuni ya 32 hadi 43 ambayo yamekuwa na tofauti kubwa. “Kamati hiyo itakuwa imejumuisha wawakilishi kutoka maeneo mbalimbali ya vyama vya siasa na makundi 201.  Kamati hiyo kamili natarajia  nitaitangaza baadaye saa 9:30 leo (jana), watakutana,”alisema. Alisema makundi mbalimbali katika kamati za vyama vyao na makundi mbalimbali yanayotokana na uteuzi wa Rais kwenye wajumbe 201, ambapo kutokana na wingi wao walipewa nafasi ya kukutana katika Ukumbi wa Pius Msekwa.
     “Kamati ya maridhiano inaweza kusaidia kuwajulisha wawakilishi wao nini ambacho tumefikia katika kamati ile ya mashauriano ili iwe rahisi na wao wawe wamepata ile taarifa. Kimsingi ili tuwe na mtazamo wa pamoja kuifanya kazi ya kumaliza kanuni hizo kwa wepesi,” alisema. Kificho alisema amefikia uamuzi huo ili wiki ijayo waanze kazi ya kupitia na kuichambua rasmi Rasimu ya Katiba. Hata hivyo, baada ya kauli hiyo, wajumbe kadhaa waliibuka wakiomba miongozo akiwemo, Dk Ave Maria Semakafu, aliyeshauri uteuzi wa Kamati ya Maridhiano kuzingatia usawa wa kijinsia katika upande wa kundi la watu 201. “Ningeomba busara hiyo kuanzia siku tulipojadili iwe inaongoza uteuzi wote kwa kuhakikisha katika kila kitu ambacho tunakiweka watu tulioko humu ndani tuweze kuwakilishwa kihalali,” alisema Dk Semakafu.
       Hali hiyo ilimfanya Kificho kuwataka wajumbe kumpendekeza mwakilishi ambaye anayewakilisha wajumbe 201 walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete ambapo baadhi yao walipaza sauti wakitaka Dk Semakafu kuwawakilisha. Uamuzi huo ulipingwa na Halima Mdee, aliyetaka Kificho kutumia busara alizotumia wakati wa kuteua kamati ya kanuni  na kumtaka kutumia busara hizo hizo kupata watu makini ambao wanatoka katika makundi tofauti yaliyomo ndani ya Bunge hilo. “Nadhani hadi saa 9.00 mchana leo (jana), utatosha wewe ama wasaidizi wako kuwasiliana  tukiamini kwamba tutapata watu ambao watatupa suluhu vitu vidogo ambavyo vimetupa tabu,” alisema Mdee. Kauli iliyoungwa mkono na Christopher Ole Sendeka aliyesema mamlaka ya kuteuwa wajumbe hao ni ya Kificho na kumtaka kuchagua wajumbe hao.
       “Una namba zetu wote tulijisajili utawaita hao kwa simu na hasa kwa sababu kazi yetu ni kukupa mamlaka, kazi yetu hapa hatuchagui tumekupa mzigo huo wewe na wenzako,” alisema Sendeka. Alishauri makundi mbalimbali yanayounda Bunge hilo kukutana kwanza, jambo litakalowawezesha kuwa na agenda wakati Kamati ya Maridhiano inapokutana. Alisema hiyo itawawezesha kujua mpasuko uliopo kati ya makundi hayo na kuchukua hoja zao kama agenda. Mjumbe mwingine Joshua Nassari alisimama na kuunga mkono kauli za wajumbe waliotangulia kuwa kazi inayokwenda si ndogo na kwamba inahitaji uzoefu na uwezo katika kuifanya. “Kazi ambayo inakwenda kufanywa na hii timu siyo kazi ndogo ni lazima uzingatie uzoefu, uwezo, uwakilishi wa watu. Haiwezi kufanyika kwa haraka haraka kwa dakika moja humu ndani. Tulikuamini kuchagua Kamati ya Kanuni, kazi hii ya kuchagua Kamati ya Maridhiano uifanye wewe halafu uje uitangaze,” alisema Nassari. Hata hivyo, kauli hiyo ilipingwa na  Abdalah Bulembo, anayetoka katika kundi la wateule 201, alisema wajumbe walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete 201 wamemchagua Dk Ave Maria Semakafu kuwawakisha katika kamati hiyo.
Mjema D., & Sauwa S./ Mwananchi

No comments: