Mh. Rais
nakusalimu;
Kauli yako
iliyonukuliwa na vyombo mbambali mbali vya habari wakati wa Ufunguzi wa Mkutano
wako wa NEC (CCM ) ni kauli hatari na yenye laana kubwa sana ya damu za Watu
wengi katika Taifa letu . Ninaona wakati mgumu mwingine ambao Taifa letu
linaingia kwa sababu ya kauli yako ambayo sasa imetangaza mauaji rasmi
yatakayoongozwa na Viongozi mbali mbali wa CCM Nchi nzima huku Polisi
wakiendelea kusimamia kama kawaida yao .
Mh Rais , Kwa
mujibu wa maneno yako umethibitishia Umma wa Watanzania kuwa mmejadiliana
kwenye kamati Kuu na kukubaliana kuwa sasa yale mambo mliyokuwa mnayafanya kwa
kificho sasa yamethibitishwa na Kamati Kuu ya Chama chako na kutangazwa na wewe
mwenyewe kuwa , kuumiza , kuua , kutesa na kudhalisha sasa imekuwa sera rasmi
ya CCM na umeithibitisha kauli hiyo mbele ya Wajumbe wa Baraza Kuu la CCM (
NEC)
Mh Rais , kwa
kauli hii naomba nikuambie kuwa umeamua kumalizia kipindi chako kwa mikono
iliyojaa Damu na Roho za Watu . Nafasi uliyonayo ni kubwa sana sio jambo jepesi
kuona makosa makubwa au madogo na kutubu , wapambe ni wengi ambao kwa kumsifu
Mfalme hata kwa ujinga maisha yao na ya watoto wao yataendelea kuwa bora ,
lakini nakuhakikishia kwa kauli hii iko siku utajuta na kulaani ni kwanini
ulitoa kauli mbaya na yenye hatia kama hii kwa Kiongozi mkubwa wa Nchi kama
wewe . Vijana wa CCM sasa wamejipanga kuua na kuchinja hadharani kama ambavyo
umeagiza wafanye na Polisi watakuwa Kimya kabisa kama ambavyo siku zote
wamekuwa lakini mara hii watasaidia wazi wazi kabisa unyama wote utakaofanywa
kwani wao pia wamesikia Amri yako na wewe ndio Mkuu wa Nchi hii .
Mh Rais , mambo
mengi yanachangia kuvurugika kwa Amani lakini moja kubwa ni pale Polisi na
Mahakama zitakaposhindwa kutenda wajibu wake katika kutenda haki haswa pale
uonevu unapokuwa dhahiri . Naweza kutambua matendo yote mabaya yanayotokea
wakati wa Uchaguzi kuwa yamesababishwa na Upendeleo wa Jeshi la Polisi kwa
Wanachama wa CCM pindi wanapofanya uhalifu dhidi ya wenzao wa Vyama Vingine vya
Siasa . Mwaka jana 2013 wakati wa uchaguzi wa marudio wa Madiwani wa kata nne
Arusha Mjini watu zaidi ya 16 waliumizwa vibaya na Green Guard na matukio yote
yaliripotiwa lakini mpaka leo hakuna Mtu aliyefikishwa mahakamani kujibu
mashitaka , lakini unakumbuka na unajua kuwa mkutano wetu wa kufunga Kampeni
hizo za Udiwani ulipigwa BOMU na Watu Wanne waliuuwa na Zaidi ya 100 kuumizwa
vibaya na wengine wamebaki na Vilema hata leo na tumekuomba uunde tume ya
Kimahakama ili tukuletee Wauaji wa watesaji wa tukio hilo lakini mpaka leo
umegoma na badala yake zimekuwepo jitihada nyingi zinazofanywa na Jeshi la
Polisi kubambikia Watu kesi nikiwemo mimi na kutesa watu kwa kiwango ambacho
hakielezeki .
Mh Rais , Watu
wameteswa na wanaendelea kuteswa sana katika Nchi hii na kazi hiyo inafanywa na
Polisi na ccm na hapa ndipo mashaka katika jamii yanatokea na Jamii kuona
ulinzi wao huko mikononi mwao na sio mikononi mwa Polisi na sheria za Nchi .
Sasa umetangaza Watu wapigwe na wachinjwe hadharani , jambo ambalo nina uhakika
nalo ni kwamba umeamua kuangamiza Nchi uliyoapa kuitetetea na ulioagiza wapigwe
sina uhakika kama watakua wamelala chini wakati wanapigwa au wamefumba macho
wakati wanateswa na kama itakuwa kinyume maana yake kutatokea Ugomvi ambao
madhara yake mimi kwa sasa sielewi ila wewe MKUU uliyotoa amri utakuwa unajua .
Mh Rais , Wewe
wewe ndiye Amri Jeshi Mkuu umeshindwa kuamrisha Polisi walinde Raia na mali zao
na sasa umeamua Watu wachinjane ? kwa kauli hii unasubiri nini Ikulu ? Hata
hivyo Nguvu ulizonazo sio Imara sana kama Nguvu alizonazo Mwenyezi Mungu.
Mateso na Damu iliyomwagika katika Taifa hili kwa uzembe wa utawala wako hakika
utalipa kama sio wewe Watoto wako na Wajukuu zako elewa kuwa hakuna dhambi
itakayopita bila kulipwa . Kauli yako hii inaleta hofu kubwa kuelekea Uchaguzi
Mkuu 2015 lakini hatutaogopa kufanya kampeni kwa sababu Rais ameruhusu tupigwe
na tuchinjwe , tutasonga mbele kutafuta haki tunayoamini kama ambavyo pamoja na
matangazo mengi ya malaria kuua lakini hatujawahi kutembea huku tumevaa
chandarua.
Mh Rais wewe
sio Mungu , hata hivyo unamkumbuka Jean Kambanda aliyekuwa Waziri Mkuu wa
Rwanda mwaka 1994 alishatakiwa kwa kutoa kauli kama yako na kugawa mapanga kwa
Vijana wa Nterahamwe na kusababisha mauaji makubwa sana Rwanda na tarehe
18/7/1997 alikamatwa Nairobi na baadae alishitakiwa na kufungwa Maisha kwenye
mahakama ya ICTR Arusha na hii ilikuwa tarehe 4 sept 1998 , sikufundishi uoga
hata kidogo ila ni muhimu kujadili historia muhimu kulingana na wakati.
Mh Rais thamani
yako haitatokana na kusababisha CCM iwe madarakani tena bali Haki kuwa
madarakani katika kipindi ulichotawala ni hekima ngumu kuielewa lakini ni
lazima tuiseme . Tunaenda Kalenga kupigwa na kuchinjwa kwa sababu tu umewapa
Watu wako ujasiri wa kufanya hivyo lakini elewa kuwa kila tukio
litakalosababishwa na kauli zako ni tukio ambalo utalipa gharama zake . Makala
zangu kama hizi uwezi kuzipenda sana Mh Rais , Wapambe watakuambia huyu kijana
ni muhuni na maneno mengi ya kejeli lakini elewa kwamba anayekupenda ni
anayekuambia ukweli , kwani ukweli thamani yake ni kubwa mno hata kama una
madhara ya muda .
Mh Rais ,
Ninapata hofu ninapoandika waraka huu kwani kama ni kwazo basi unaweza kuamua
kufanya chochote dhidi yangu lakini napata faraja kuwa kifo kipo tu hata kama
utafuti haki na ukweli kwani Bibi yangu kule Machame hakufa kwa kuwa aliandika
waraka bali ni umri tu ulimuondoa . Mh Rais ukweli nakuambia usipofuta kauli
yako yenye lengo baya kwa Nchi yetu basi nimemuomba Mungu afanye jambo muhimu
dhidi yako na jambo hilo muhimu liko wazi kuwa kama wewe ni chanzo cha Taifa
kuharibika kwani nini anaendelea kukupa pumzi ? Hapa nitaonekana muhuni tena
lakini Mh Rais wema wako ni katika haki na sio sifa .
Mwisho , Mh
Rais , Mamlaka yana tabia ya kudanganya akili nikuombe Rais wangu usikubali
mamlaka ikudanganye hata kidogo , futa kauli yako , watakaokuona mjinga wao
ndio wajinga . Najua Polisi na Jeshi wanakutii wewe lakini Dhambi na hila iko
mbali na MUNGU .
Godbless
Lema (Mb)
No comments:
Post a Comment