Ngoma ikilia sana……. Hupasuka!
na Bryceson Mathias
ENZI za umanamba wakati wazazi wetu wakitembea kwa mguu kwenda Tanga kufanya kazi za kukata Mkonge, walikuwa wakiwaacha wake zao kwa Wakwe zao, kwa madai kwamba wanakwenda kutafuta kipato kwa kibena ‘Hupagala’ ili kuzisaidia familia zao, na pindi wakipata watarudi.
Baada ya kukata Mkonge Tanga muda mrefu na kujipatia kipato walichohitaji; manamba hawa walioiitwa watu wa bara wakitoka mikoa ya nyanda za juu kusini, walirudi makwao na walipofika, kwanza waliwarejesha wake zao!
Wakwe hawakushangaa kufuatwa na mama zao, kwa sababu kwa kutunza familia hizo; walibahatika kupewa zawadi nono toka kwa wakwe walizochuma walikokuwa; Ingawa pia walikuwako wanaume wazembe waliolowea na kuitwa walowezi.
Kwa msingi huo; Nitawashangaa sana watanganyika, watakaoikataa nchi yao, eti kwa sababu tu imeitwa Serikali Tatu. Uoga huo hauna tofauti na mwanamke wa kwanza kwenye ndoa, kuiogopa nyumba ndogo kama vile Simba, auungurumapo, anakosekana mchezaji!
Mwanamke Mkubwa mwenye uhakika na ndoa yake akijua walikotoka Mume wake, hawezi kuiogopa nyumba ndogo kwa sababu imemkuta yumo ndani ya nyumba! Mvua na Jua vikiwa vyao katika maisha yao, ila mke mdogo amenyatia kula kivulini! Hajui adha yake.
Niombe radhi ili niwaulize wasomaji; hivi kwa heshima za ki-afrika tulizonazo, mtu akikuuliza nionyeshe nyumba ndogo, utamuonesha wapi? …..kama jibu unalo, basi elewa kufumua nyumba ndogo ni rahisi sana kuliko kufumua nyumba kubwa.
Tanganyika ni Mama Mkubwa aliyepata Tabu ya kuutafuta uhuru na Jamhuri ya nchi yetu, lakini kwa sababu wazazi wetu (Baba) Tanzania alikwenda kutafuta kipato Tanga kwenye Mkonge, na sasa amerudi bara hakulowea huko akaitwa mlowezi, lazima arudi kwa Babu akamchukue Mama na watoto wake.
Hivi karibuni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini Tanzania Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba alisema kuwa, muundo wa sasa wa muungano haukidhi matakwa ya Watanzania walio wengi.
Jaji Warioba aliyasema hayo wakati wa kukabidhi rasimu ya katiba kwa Rais Jakaya Kikwete wa nchi yetu, ambapo Jaji Warioba alisema, miongoni mwa mambo yaliyopendekezwa kwenye rasimu hiyo ni kwamba;
Spika na Naibu Spika wasitokane na wabunge au kiongozi wa juu wa chama cha siasa, na mbunge atawajibishwa na wananchi.
Pia Tume hiyo ilipendekeza Msajili wa Vyama vya Siasa iwe taasisi inayojitegemea na si kuwa sehemu ya Tume Huru ya Uchaguzi.
Dondoo nyingine kwenye rasimu hiyo ni pamoja na wabunge kuwa na ukomo, mawaziri kutokuwa wabunge na kupunguzwa kwa madaraka ya rais.
Wananchi wa Tanzania kwa miaka kadhaa, wameonyesha kuchoshwa na marekebisho yaliyokuwa yakifanywa mara kwa mara katika baadhi ya vipengele vya katiba, jambo lililomsukuma Rais Kikwete aanzishe mchakato wa kupatikana katiba mpya kabla hajamaliza kipindi chake cha uongozi mwaka 2015.
Nimechukizwa kuona; siku ya kwanza tu ya wajumbe wa rasimu ya pili katika Bunge hilo maalum, kabla hawajaanza kujadili hoja, kumekuwa na vituko, kejeli na vioja huku wanaotarajiwa wawe na hekima na heshima katika mjadala huo, wamekuwa kama watoto.
Waswahili wanasema; Ngoma ikilia sana! Hupasuka! Nadhani pamoja na heshima ambayo nchi yetu imekuwa ikisfiwa na kuitwa ni kisiwa cha Amani, kwa vurugu za kura za siku ya awali, tutaitwa kisiwa cha vurugu!
Lakini nauliza nani anasababisha watanganyika waikatae nchi yao?
No comments:
Post a Comment