Na Bryceson Mathias
NAPATA Majibu kutoka kwa Mmoja wa Viongozi wa Ngazi ya Msingi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kata ya Nkenda, Wilaya ya Kyerwa, Mkoa wa Kagera, Evodius Nkwenda,
Nkwenda anaanza kwa kusema; Katika chaguzi zilizopita tumebaini vyama vyenye nguvu na rasilimali, vinapoona vinaelekea kushindwa, wao huanza kwa kuwatia hofu wapiga kura, kutumia Mabomu, na kumaliza kwa kuwategemea Tume na Polisi ili washinde uchaguzi.
Nkwenda anabainisha hayo kwa kunukuu Maandiko ya Biblia; “Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani”. (1 Wakorintho 10:11).
Anadai, yale waliyopitia ndiyo tunayopitia Chadema leo. Kilichowaagusha ndicho kitakachotuangusha na sisi kama hatutatenda kinachotakiwa, na kilichowapa ushindi wao ndicho kitakachotupa nasi ushindi tukitenda sawasawa.
Alisema; Wengi wetu tunafahamu kuhusu habari ya Daudi na Goliati; Ilitokea kulikuwa na vita kati ya Wafilisti na Waisraeli. Kabla ya makabiliano, Wafilisti walikuwa upande mmoja kwenye mlima, na Waisraeli nao kwenye mlima upande mwingine.
Katika nyakati hizo hakukuwa na bunduki wala mabomu kama leo. Vita vilikuwa vikipiganwa kwa makabiliano ya uso kwa uso; mtu kwa mtu. Askari walitumia mikuki, mapanga, mashoka, mawe na silaha zingine ambazo zilihitaji nguvu za kimwili za binadamu.
Goliati alikuwa ni askari shujaa wa Wafilisti. Alikuwa akitoka kila siku asubuhi na jioni na kusimama juu ya mlima. Kisha, kwa sauti ya juu, akawatukana Israeli na kutamba kwa majigambo na dharau nyingi akisema:
Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi. Kama mkiweza kupigana nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda yeye na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia. Alinukuu (1 Samweli 17:8-9).
Ndivyo wanavyofanya baadhi ya Viongozi wetu wenye Mamlaka wakati wa Chaguzi na katika maisha yetu ya kila siku leo, na hivyo kujikuta tunapita katika majaribu mazito ambayo tunapambana nayo lakini inaonekana kama umefika mwisho.
Wakati shetani anasema moyoni mwake, “Hii shida mpaka ikuue! Huna cha kufanya! Hutapona kamwe katika ugumu huu wa maisha! Hata ufanyeje hutoki humu! Chadema tunasema tunaanza na Mungu, Tutamaliza na Mungu, na ndiye atakayetushindia kama Daudi dhidi ya Goliati”.
Katika vita hivi kati ya Wafilisti na Waisraeli, maandiko yanasema: Ndipo akatoka Goliathi, wa Gathi, ambaye urefu wake ulikuwa mikono sita na shubiri moja. Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani, tena amevaa darii ya shaba; na uzani wake ile darii ya shaba ulikuwa shekeli elfu tano za shaba.
Tena alivaa mabamba ya shaba miguuni mwake, naye alikuwa na mkuki wa shaba kati ya mabega yake; na mti wa fumo lake ulikuwa kama mti wa mfumaji; na kichwa cha mkuki wake kilikuwa shekeli mia sita za chuma uzito wake; na mtu aliyemchukulia ngao yake akamtangulia.. Huyu hakika alikuwa ni pandikizi la mtu kweli kweli! (1 Samweli 17:4-7)
Kutokana na jinsi Goliati alivyotisha, kwa kule kutoka kwake kila asubuhi na jioni mbele ya Waisraeli, maandiko yanasema: Yule Mfilisti alisema, Nayatukana leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane. Basi Sauli na Israeli wote waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana. (1 Samweli 17:10-11). Goliati aliendeleza tambo hizi kwa siku 40!
Je, Goliati wetu leo ni nani?.
Hawa ndio akina Goliati wa maisha yetu leo, Ufisadi, Vitisho, Mabomu, ni Tume ya Uchaguzi, Ukosefu wa ajira, Uchumi mbaya, Dawa za kulevya zinakutesa, Hofu na Mashaka juu ya maisha ya kesho, Ugumu wa Maisha (bei za Vitu) , Mauaji ya Wakulima na Wafugaji, Dhuluma na Haki za watu, na kadharika.
Katikati ya fedheha na matukano ya Goliati, alitokea Daudi; kijana mdogo tu. Japo alikuwa hata hajafikia umri wa watu waendao vitani, aliamua kumkabili yule pandikizi. Elewa Chadema ni kijana mdogo (Daudi), anataka kumkabili Goliati mwenye Zana kwa Kombeo.
Alisema: Wewe unanijia mimi kwa mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la BWANA wa Majeshi ya Israeli uliowatukana. Siku hii ya leo atakuua mkononi mwangu, …Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba BWANA haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya BWANA, naye atawatia ninyi mikononi mwetu. (1 Samweli 17:45-47).
Daudi alizungusha Kombeo lililokuwa na kijiwe kidogo kisha akakiachia. Kijiwe kidogo kilimpata jitu wa kutisha na silaha zake hazikumwokoa. Alianguka chini na kufa palepale!
Vitisho, Fedha, Umaarufu, Cheo, Wizi wa Kura, Kununua Shahada, Ujanja au uwezo wowote wa kibinadamu ni sawa na upanga na mkuki. Kuna shida na majaribu mengi ambayo hayatatuliki kwa upanga au mkuki. Kila mwanadamu ana mahali pake pa kukwamia; lazima!
Nkwenda anasema Chadema haina Majeshi, Silaha, Ufisadi, ila ina Kweli, Uadilifu na Nguvu ya Umma, na kutokana na kuona Machungu na mateso wanayopata wananchi ya kudhulumiwa haki na rasilimali zao Mchana kweupe! Ndiyo maana Chadema inaamua kuanza na Mungu na kumaliza naye.
Hivyo ndugu zangu, Bwana anaagiza kwamba, Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako. (Yoshua 1:9).
Jiwe letu ndani ya Kombeo ya kumshinda Goliati ni ‘Daftari la Kura’. Chonde ‘Usisahau kujiandikisha kwenye daftari la kupigia kura kama Yusufu na Mariamu walivyofanya’. Fahamu kuuza Shahada ya kura ni Maafa na Majanga kwako.
Tena Mungu anasema kwamba, Utokapo kwenda vitani kupigana na adui zako, na kuona farasi, na magari, na watu wengi kuliko wewe, usiwaogope; kwa kuwa BWANA, Mungu wako yu pamoja nawe, aliyekukweza kutoka nchi ya Misri. (Kumb. 20:1).
Chadema tutasimama na ahadi ya Bwana. Na nakushauri kila Mtanzania na Mwanachadema, Usiangalie ukubwa wa tatizo au adui yako. Mtazame Yeye aliye Mkuu na Mwaminifu, Mungu! Ni lazima tutashinda! Anamaliza Nkwenda
No comments:
Post a Comment