Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimefungua milango
kwa Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, katika harakati za kuelekea uchaguzi
mkuu wa mwaka 2015.
Kimesema wanaombeza kwa madai kwamba rushwa anayoipigia
kelele iliasisiwa wakati akiwa madarakani, hawalitakii mema taifa.
Kauli ya
kumkaribisha Sumaye kujiunga na Chadema ilitolewa na Mwenyekiti wake, Freeman
Mbowe, juzi muda mfupi baada ya Sumaye kumaliza hotuba yake wakati wa hafla ya
uzinduzi wa Kanisa la Lole la Usharika wa Mwika, Dayosisi ya Kaskazini ya
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
Hatua ya Mbowe kumkaribisha
Sumaye kujiunga na Chadema inafuatia kauli aliyoitoa Waziri Mkuu huyo mstaafu
wiki iliyopita kwamba mahasimu wake kisiasa ‘wanampakazia’ kwamba yeye ni
maskini wa kutupwa, hivyo hana uwezo wa kuwapa fedha wanaomuunga mkono katika
kupinga rushwa ya uchaguzi, ufisadi na aina nyingine ya uovu kwa jamii ya
Watanzania.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu mstaafu (Sumaye), kama nilivyokwisha
tangulia kukuomba radhi, huko ulipo ni pagumu, karibu kwetu kwa sababu sisi
tunakemea rushwa wazi wazi, tena bila ya kificho, tumekemea rushwa siyo leo,
siyo jana.
Tuko tayari kufanya kazi na wewe kwa sababu unakemea rushwa,
tunakupongeza na karibu sana,” alisema Mbowe mbele ya viongozi mbalimbali wa
kisiasa na dini akiwamo Mkuu wa Kanisa hilo nchini, Askofu Dk. Alex Malasusa.
Mbowe
alisema kwamba maneno aliyozungumza Sumaye ameyatafakari kwa kina na kujiuliza
maswali mengi kwa kuwa maneno hayo siyo mepesi sana kuyasikia hasa kwa viongozi
ambao wamekuwa na mamlaka ya kikatiba kuwaongoza Watanzania.
Alisema kuwa hoja
ya rushwa inayotolewa na Sumaye, ni ya msingi sana na haki katika taifa la
Tanzania ni bidhaa adimu na kwamba wanaotetea haki wengi wao huipata kwa
gharama ya maisha yao. “Kwa watu ambao tuko katika active politics (siasa hai),
tunaona namna siasa zinavyobadilika na kuwa ni mambo ya kutishia uhai wa watu.
Wenzetu viongozi wa Kanisa mtusaidie kuomba ili tusije tukajenga misingi ya
kulipasua taifa hili kwa itikadi ya vyama vya siasa,” alisema na kuongeza:
“Haya
ni mambo ya kupita na Mheshimiwa Sumaye siasa ni kazi ya kupita kesho CCM
inaweza isiwapo na Chadema ikawapo…njoo sasa Chadema.”
KAULI YA SUMAYE
Hata
hivyo, baada ya ombi la Mbowe, Sumaye hakujibu lolote zaidi ya kutikisa kichwa
na kutabasamu.
Sumaye, alipoulizwa na NIPASHE kwa njia ya simu jana kuhusiana
na kauli ya Mbowe, alisema yeye ni mwana-CCM halisi, hivyo ataendelea kubaki
ndani ya chama hicho daima kama mwanachama mwaminifu.
“Kwenye vyama vya
siasa, hakuna kualikana, ukijisikia na wakati ukifika unakwenda, Mbowe
kazungumza vile kwa kuwa amejisikia kuzungumza mbele ya hadhara ila sina mpango
wa kuhamia Chadema,” alisema Sumaye.
Kuhusu uwajibikaji wa kibunge, Mbowe
alisema wawakilishi wote wa wananchi, mwezi ujao watakwenda kuanza Bunge la
Katiba ambalo litachukua miezi mitatu na kwamba kuna mambo mengi ambayo yako
gizani mbele yao, hivyo wanaliomba Kanisa lisikae mbali kushiriki nao katika
hatua zote za kiukombozi.
Kwa nyakati tofauti akiwa katika harambee ya
kuchangia ujenzi wa ukumbi wa mikutano wa Kanisa la Visitation Maonano, Parokia
ya Mawela katika Jimbo Katoliki la Moshi na hafla ya uzinduzi wa Kanisa la
Usharika wa Lole-Mwika wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT mwishoni mwa wiki,
Sumaye alisema kuwa hivi sasa rushwa na matumizi makubwa ya fedha za kuwanunua
wapigakura, vinataka kuwa utaratibu halali wa kuwapata viongozi kuanzia ngazi
za vijiji hadi urais.
“Ukikemea rushwa tu basi utapachikwa sababu nyingi
zisizohusika ikiwamo ya kugombea urais mwaka 2015. Nasema katika hili suala la
kugombea au kutogombea urais si sababu. Vita yangu dhidi vya rushwa si ya leo,”
alisema.
Source: Mushi G. ( Jan. 2014).Sumaye aitwa Chadema. Retrieed from Ippmedia/Nipashe
No comments:
Post a Comment