MBIO za kusaka urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM), na uteuzi wa nafasi nne za mawaziri, vinaelezwa kukibomoa chama hicho,
Tanzania Daima limedokezwa. Mbali na mambo hayo, mchakato wa uundwaji wa katiba mpya
ambayo rasimu ya pili imetoka hivi karibuni na kuingizwa kwa serikali tatu,
umeonekana kukiathiri zaidi chama hicho kinachotaka uwepo wa serikali mbili. Tayari viongozi wa CCM wameshaanza maandalizi ya kukutana
na wabunge, wawakilishi na wabunge wa Bunge la Katiba watakaochaguliwa, kwa
lengo la kuweka msimamo wa kutopitisha serikali tatu wakati wa majadiliano. Wanataka hoja ya serikali tatu isifikishwe kwenye kura ya
maoni ambako wana hofu inaweza kupata uungwaji mkono. Hofu ya makada hao wa CCM ni kuwa muundo wa serikali tatu
utabomoa muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa na Rais wa Kwanza wa
Zanzibar, Abeid Amani Karume na Julius Nyerere aliyekuwa Rais wa Tanganyika.
Wakati suala la katiba mpya likionekana kuwaumiza vichwa
makada wa chama hicho, mbio za urais unaotarajiwa kufanyika mwakani, nazo
zimezidi kukipasua chama hicho. Hadi hivi sasa viongozi wa CCM wamekuwa wakipambana na
aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ambaye katika siku za hivi karibuni
alitangaza safari ya matumaini kuelekea ndoto zake za kuwapatia Watanzania
elimu bure na huduma bora za msingi. Lowassa, alitangaza safari hiyo iliyotafsiriwa ni ya
kuwania urais katika mkesha wa mwaka mpya jimboni kwake Monduli, ambako
aliwaalika makada mbalimbali wa CCM wakiwemo wajumbe wa vikao muhimu vya
maamuzi. Miongoni mwa waliokuwepo kwenye hafla hiyo ni Mwenyekiti
wa wenyeviti wa chama hicho, Mgana Msindai, ambaye alisema wanaunga mkono
safari ya Lowassa. Tangu Lowassa atangaze safari yake hiyo, viongozi wa CCM,
akiwemo Makamu Mwenyekiti (bara), Philip Mangula, wamejitokeza hadharani
kumpinga.
Mangula alisema chama chake kimeunda timu ya kuchunguza
makada wake walioanza harakati za kuwania uongozi kabla ya pazia kufunguliwa,
na wakibainika kutenda kosa hawatapewa nafasi ya kuwania nafasi husika. Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), nao ulitaka Lowassa
atimuliwe kwa madai ya kukivuruga chama na kupanga safu yake ya kuwania
madaraka ilhali Rais Jakaya Kikwete hajamaliza muda wake. Wakati chama hicho kikionekana kupambana na Lowassa,
mbunge huyo juzi katika ukusara wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook
aliandika: “Ukiona unatumia nguvu nyingi kumchafua mtu kwa kumpakazia mambo,
kumsengenya, kumfitinisha na kumsingizia, ujue yeye ni bora kuliko wewe,
kichafu kinaonekana hata bila kuambiwa.”
Uwaziri moto
Baraza la mawaziri hadharani
Leo huenda kiu ya Watanzania kujua nani ametoswa nani
amekumbukwa kwenye Baraza la Mawaziri ikakatwa ambapo majina yao yataanikwa. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari
jana jijini Dar es Salaam na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Sefue, leo atakutana na waandishi wa habari Ikulu. Ingawa taarifa hiyo haikubainisha ni jambo gani
litakalozungumzwa, suala la kutajwa kwa mawaziri wapya na mabadiliko ya baraza
hilo ni jambo linalotarajiwa.
Source: Tanznia Daima (Jan. 2014).
Mambo matatu yaitesa CCM. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment