Viongozi wa vyama vya siasa wilayani
hapa Mkoa wa Geita wamesusia kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya (DCC)
kilicholenga kujadili bajeti ya maendeleo ya halmashauri ya wilaya hiyo.
Viongozi
hao wa Chadema, UDP, TLP, CUF na NCCR Mageuzi, walisusia kikao hicho mwishoni
mwa wiki iliyopita wakidai kudharauliwa na ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo
kwa kushindwa kuwalipa posho za vikao hivyo tangu mwaka jana.
Hatua hiyo
ilikuja baada ya Kaimu mwenyekiti wa Chama cha UDP wilaya ya Chato, Francis
Katambi, kuomba mwongozo juu ya malipo ya kikao hicho kabla ya kufunguliwa. Baada
ya swali hilo, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Clement Belege, alisema malipo
ya posho hizo hufanywa na Ofisi ya mkuu wa mkoa na inapotokea mkoa hauna
fedha huwasiliana na halmashauri husika ili kusaidia malipo.
Alisema hawezi kuzungumzia
posho ya mwaka jana kwa kuwa yeye hakuwa mtumishi wa halmashauri hiyo, licha ya
kuthibitisha ofisi ya mkuu wa mkoa imemwandikia barua ili kuwalipa wajumbe
katika kikao cha mwaka huu lakini kutokana na halmashauri yake kutokuwa na
fedha hapatakuwa na malipo yoyote.
Kauli hiyo ilionekana kuwakera viongozi hao
na kulazimika kutoka ukumbini kisha kuondoka hata kabla ya kikao hicho
kufunguliwa kwa madai hawawezi kuendela kudharauliwa wakati mchango wao ni mkubwa
kujadili na kutoa mapendekezo yao katika bajeti ya halmashauri kabla ya
kupelekwa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Wakati
viongozi hao wakisusia na kuondoka, mkuu wa wilaya hiyo, Rodrick Mpogolo
alikuwa ameketi akisubiri kuruhusiwa kufungua kikao hicho ambacho baadaye
kiliendelea kikiwa na wajumbe wachache wakiongozwa na wakuu wa idara za
halmashauri hiyo.
Source: Mkate D. ( Dec. 2020). .Retrieved from Ippmedia/ Nipashe
No comments:
Post a Comment