Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo-Chadema (Bavicha) limeandaa kongamano kubwa kuadhimisha miaka 52 ya
uhuru wa Tanganyika, litakalohudhuriwa na viongozi waandamizi watano wa chama
hicho.
Viongozi hao, ambao wataongozwa na Mwenyekiti,
ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, ni
pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, ambaye pia ni Mbunge wa Singida
Mashariki, Tundu Lissu.
Wengine ni Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa
Chadema, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, Mjumbe wa Kamati Kuu (CC)
ya chama hicho, Mabere Marando, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, pamoja na Dk. Kamilius
Kasala, ambaye ni bingwa wa masuala ya uchumi.
Katibu Mkuu wa Bavicha, Deogratius Munishi, alisema
jana kuwa kongamano hilo litawahusisha vijana wa Chadema wa majimbo ya Dar es
Salaam , wanafunzi wa vyuo vikuu vya jijini humo, ambao ni wanachama wa chama
hicho.
Alisema msingi mkuu wa kongamano hilo ni kutoa
tathmini halisi ya hali ya Taifa kwa kipindi cha miaka 52 na mwelekeo mbadala
kutoka chama mbadala.
Munishi alisema mgeni rasmi katika kongamano hilo
atakuwa ni Mbowe, ambaye atatumia maadhimisho hayo kuzungumza na vijana juu ya
mustakabali wa nchi, hususan masuala muhimu yanayolikabili Taifa kwa sasa.
Alisema pia kwa mara nyingine tena, kuanzia leo hadi
keshokutwa, Bavicha itakuwa mwenyeji wa mkutano wa vijana wa vyama vya
kidemokrasia kwa Ukanda wa Afrika Mashariki. Munishi alisema mkutano huo
utafanyika jijini Dar es Salaam na utajumuisha vijana 40 kutoka mataifa
wanachama wa Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia barani Afrika (Dua) kwa ukanda
huo.
Alisema pia utawahusisha wageni maalumu kutoka
nchini Ghana na wabunge kutoka Uingereza na utafunguliwa na Mbowe.
No comments:
Post a Comment