Mwenyekiti wa
Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, ametahadharisha kuwa hawatakubaliana na mpango
unaosukwa wa kutaka Bunge Maalum lisionyeshwe moja kwa moja.
Kauli hiyo
aliitoa jana mjini hapa katika mkutano wa kuchagua wawakilishi wa Asasi zisizo
za kiserikali ili majina yao yapelekwe kwa Rais kwa ajili ya kuyateua kushiriki
kwenye Bunge Maalum la Katiba linalotarajia kufanyika Februari
mwakani.
Kibamba alisema mpango huo unaosukwa ili Bunge hilo lisionyeshwe moja
kwa moja na vituo vya televisheni nchini hautakubalika na mambo yote yanatakiwa
kuwa hadharani.
Alisema Bunge hilo lisiwe la kificho ili kila mwananchi
ashuhudie kinachoendelea ndani ya Bunge hilo.
“Lazima tuone moja kwa
moja…tuone wabunge wanaolala, wanaochapa kazi, wanaoleta vijembe nao
waonekane…sisi Jukwaa la Katiba kila siku jioni tutakuwa kwenye makorido
mnapotoka tunawasubiri ili tuwaambie walichokifanya,” alisema.
Pia, alisema
kuna dharau ambazo zinaendelea bungeni na kuwa wabunge wapya wa kiingia wale
wakongwe wamekuwa wakiwaita wale wapya kuwa ni wachanga.
“Kuna baadhi ya
wabunge wakongwe ambao wana zaidi ya miaka 30 bungeni, wanapowaona wale
wachanga wanazungumza wanawaambia nyie watoto ebu nyamazeni hamjui kitu hapa,”
alisema.
Aidha, aliwataka wabunge na Wawakilishi kutowanyanyapaa wabunge
watakaoteuliwa na Rais kwa ajili ya Bunge Maalum la Katiba.
Hata hivyo,
alisema Jukwaa la Katiba litatumia nafasi hiyo kuwafunda na kutoa mwongozo kwa
wawakilishi ambao watachaguliwa kuingia katika Bunge hilo ili kuhakikisha kuwa
wanawatetea Watanzania.
Bunge hilo linatarajiwa kushirikisha wabunge wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 358, Wawakilishi wa Zanzibar 76 na Asasi
wawakilishi 201.
Jana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Jakaya
Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein walikabidhiwa Rasimu ya
pili ya Katiba na kinachosubiriwa ni majina ya wawakilishi kutoka asasi hizo na
mwisho wa kutuma majina yao ni kesho kutwa.
Baada ya hapo Bunge hilo
litakutana na kuipitisha katiba. Watakaofanya maamuzi ya mwisho ya kuikubali au
kuipitisha katiba hiyo ni wananchi kupitia kura ya maoni.
Source: Masano J. ( Jan 2014).Kibamba: Hatutakubali Bunge la Katiba kutoonyeshwa live. Retrieved from Ippmedia/Nipashe
No comments:
Post a Comment