Hatima ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto
Kabwe, na wenzake waliovuliwa nyadhifa ndani ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), itajulikana Ijumaa wiki hii wakati Kamati Kuu ya chama
hicho itakapokutana kuzungumzia sakata hilo na kutoa maamuzi ya mwisho.
Afisa
Uhusiano wa Chadema, Tumaini Makene, alisema jana kuwa chama kimewaandikia
barua ya kuitwa mbele ya kikao ili wasikilizwe.
Mbali na Zitto aliyevuliwa
unaibu katibu mkuu na Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, wengine waliovuliwa
nafasi zao ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba
na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo, Novemba 22, mwaka huu kwa tuhuma za
kukisaliti chama.
“Chama kimewaandikia barua hiyo baada ya kuwa
kimeshawaandikia barua ya kuwajulisha kuwa kimeshapokea maelezo yao ya
maandishi kuhusu tuhuma 11 walizotuhumiwa nazo. Kwa hiyo wametakiwa kufika
kwenye kikao cha Kamati Kuu Januari 3, mwakani (Ijumaa) ,” alisema.
Makene
alisema wameitwa ili wasikilizwe kutoka midomoni mwao kuhusu tuhuma zinazowakabili
na kwamba hilo limefanyika kwa mujibu wa kanuni ya uendeshaji chama, katika
kifungu cha 6.5.2 (b) na 6.5.2 (d).
Alisema kifungu hicho kinaelekeza kwamba
Kamati Kuu inaweza kuchukua hatua za dharura bila kuzingatia utaratibu wa (b)
na (c) kama itaona maslahi ya chama kwa ujumla yako hatarini.
“Lakini katika
kuchukua hatua hizo za dharura, mwanachama au kiongozi anayelalamikiwa
atalazimika kuitwa kwenye kikao husika. Hivyo chama baada ya kupokea maelezo
yao ya maandishi sasa wameitwa wajieleze kwa mdomo. Kila kitu kinakwenda kwa
utaratibu hapa,” alisema.
Makene alisema tangu mwanzo chama kiliweka utaratibu
kwa kuzingatia katiba, kanuni, maadili, taratibu na miongozo ya chama, ndiyo
maana ya taasisi.
Source: Mwanakatwe T. (Jan 2013). Chadema kuwahoji Zitto, Kitila, Mwigamba Ijumaa. Retrieved from Ippmedia/Nipashe
No comments:
Post a Comment