PRESS RELEASE
Ndugu waandishi
Ndugu waandishi wa habari na wananchi
kwa ujumla, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya
njema kufikisha miaka mitatu ya kuwatumikia Madaktari na Watanzania kwa ujumla
kwa vile nimekuwa kiongozi wa Chama Cha Madaktari Tanzania (MAT) kwanza kama
Katibu Mkuu wa Chama hicho kwa miaka miwili na baadae Makamu wa Rais wa Chama
hicho.
Kwa kupitia nafasi hizo za MAT
nimeweza kuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Kitaaluma vya Afya ambapo
shirikisho hilo linajumuisha vyama vyote vya kitaaluma katika sekta ya afya.
Nafasi nyingine muhimu ya kujivunia kuwatumikia Watanzania kitaaluma ni pamoja
na ni kuwa katibu mkuu wa kwanza wa Chama Cha Wafanyakazi Madaktari na
Wafamasia Tanzania (TMDPWU) nikiwa mwanzilishi na kaimu katika nafasi hiyo.
Ndugu waandishi, katika kipindi cha
uongozi wangu nikishirikiana na wenzangu tumejitahidi kushiriki katika
uboreshwaji wa huduma za afya Tanzania, na yafuatayo ni mfano;
1. Kushiriki katika kupitia Rasimu ya Sheria
ya Madaktari ambayo itawezesha madaktari kufanya kazi kwa weledi zaidi na hivyo
kupunguza makosa ya kitaaluma wakati wa utoaji wa huduma za afya. Rasimu hii
iko katika hatua za mwisho za kwenda bungeni.
2. Kuandaa rasimu na kusajili chama cha
Wafanyakazi Madaktari na Wafamasia Tanzania ambacho kitajikita zaidi katika
kudai maslahi huku kikiacha MAT kifanye kazi ya kuboresha taaluma. Chama hiki
tayari kinaendelea kushamiri katika vituo vya kazi vya madaktari.
3. Kudai mazingira bora ya kazi katika
sekta ya afya ikihusisha upatikanaji wa vifaa tiba na madawa kwa manufaa ya
kuboresha huduma za afya.
4. Kwa kushirikiana na SIKIKA kufanya utafiti
uliowezesha kujua upungufu mkubwa wa madaktari katika utoaji wa huduma za afya.
Utafiti huu utaiwezesha serikali kufanya maamuzi sahihi katika kushughulikia
suala la Rasilimali watu katika afya.
Pamoja na haya yote mazuri
niliyohusika katika kuongoza Madaktari na kuwa na moyo wa kuendelea kufanya
hivyo, bado kuna mambo mengi hayaendi vizuri ambayo ni ya kimfumo katika
serikali hii ya CCM ambayo yanaendelea kudidimiza huduma za afya. Mifano mizuri katika hili ni urasimu usio na
maana katika usambazaji wa madawa na vifaa tiba, kutojali wataalamu, ufisadi na
uzembe kauanzia wizarani, taasisi zake mfano Bohari la dawa mpaka katika vituo
vya afya.
Ni kutokana na sababu hii inakuwa
ngumu kwa vyama vya kitaaluma kuweza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta hii
na hivyo kuendelea kwa huduma duni za afya. Naamini kuwa ili kuwezesha
upatikanaji wa huduma bora za afya katika jamii hii ya kitanzania kuna haja ya
kubadilisha mfumo huu wa afya uliopo kwa kupata sera madhabuti zenye kujali
Mtanzania maskini ambaye kwa kiasi kikubwa hawezi kumudu gharama za afya
zinazopanda kila siku. Kwa hiyo mchango wa kisiasa ili kuwezesha haya
unahitajika ili kubadilisha sekta hii ya afya Tanzania.
Ndugu waandishi
Ni kwa nia hii nzuri niliyonayo na
niliyoonyesha ya kuboresha sekta ya afya nchini ninafurahi kusema kuwa sasa
ninahamishia rasmi nguvu zangu katika Chama cha siasa na hiki si kingine ni
CHADEMA ambacho kimejipambanua kuwa chama cha watu kwa ajili ya maendeleo ya
watu.
Na kwa vile tayari nimeaminiwa
kushika wadhifa wa Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Ziwa Magharibi wa CHADEMA,
nitataoa mchango wangu katika chama hicho ambacho nina hakika kitaweza
kufikisha mazuri katika vyombo husika vya kimaamuzi mfano ni Bunge la Jamhuri
ya Tanzania, halmashauri n.k.
Hivyo basi kwa kupitia sababu hii ya
kuwa kada rasmi wa CHADEMA bila kushurutishwa na kwa hiari yangu nang’atuka
nafasi zangu zote za kuongoza Madaktari na watumishi wengine wa afya na tayari
nimepata Baraka ya Halmashari kuu ya MAT ya kufanya hivyo kupitia kwa Rais wa
Chama hicho;
Ndugu waandishi,
Nimeamua kufanya maamuzi haya ili
i) Kuondoa
mgongano wa kimaslahi (conflicts of interests) kati ya Vyama ninavyoongooza,
Madaktari, mimi mwenyewe na CHADEMA.
ii) Kuweza
kuchangia kwa karibu zaidi katika Chama hiki mawazo yangu ya kitaaluma ambayo
nina hakika yatafanyiwa kazi na kuwa manufaa zaidi katika uboreshaji wa sekta
hii hasa wakati huu ambapo chama tayari kinaendelea kuandaa sera zake
mbalimbali ikiwemo ya afya.
iii) Nikiwa
kama msomi kukiri waziwazi kuwa nitajishughulisha bila kificho katika kutoa mawazo
na utaalamu wangu CHADEMA ili tuweze kwa pamoja kuwa na sera nzuri na kuboresha
huduma za afya Tanzania.
iv) Kuwakumbusha
watumishi wote wenye taaluma mbalimbali kuwa kushiriki katika harakati za
kisiasa ili kuiondoa CCM si kosa la jinai kama ambavyo inataka kuaminishwa, na hii
inajionyesha hata katika vifungu vya kanuni za maadili ya utendaji katika
utumishi wa umma;
· 5 (1) - Kinatoa haki ya kidemokrasia ya kuwa
mwanachama wa Chama chochote.
· 5(2) – Kushiriki masuala ya siasa
lakini usionyeshe upendeleo wa kisiasa
· 5(3)(a) – Usijuhusishe na siasa saa
za kazi au mahala pa kazi
Ndugu waandishi
Napenda kuwashukuru Madaktari na
watumishi wengine wa afya walioniamini na kunipa uongozi katika kipindi chote
hiki na kuwa mimi bado ni mtaaluma na nitaendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa
Vyama hivyo. Pia napenda kuupongeza na kuushukuru uongozi imara wa CHADEMA kwa
kuniamini na kunipa nafasi ya mimi kushiriki katika mapambano haya ya ukombozi.
Mwisho kabisa, Napenda kuwasihi
wataalamu wote wa chi hii kutokuwa waoga katika kujihusisha na mageuzi ya kiuchumi
na kijamii ya nchi hii yanayoendelea na kwamba waache kulalamika tu bali
wachukue hatua. Nchi hii ni yetu sote na
sote tushiriki kuijenga.
MUNGU IBARIKI TANZANI.
Dr. Rodrick Kabangila- Daktari bingwa wa Magonjwa ya Tiba,
tafiti za huduma za afya na epidemiolojia
-Mhadhiri Mwandamizi – CUHAS-Bugando
-Makamu Mwenyekiti – CHADEMA Kanda ya ziwa
Magharibi
No comments:
Post a Comment