Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.
Willibrod Slaa, ameanza ziara katika Jimbo la Kigoma Kaskazini linalowakilishwa
na Zitto Kabwe, huku akiwaeleza wananchi kuwa chama hicho hakikirupuka
kumsimamisha uongozi Zitto kama inavyoelezwa na baadhi ya watu.
Aidha,
amewalipua wenyeviti wa Chadema waliojizulu baada ya sakata la Zitto kwa kusema
kuwa wamefanya hivyo kutokana na kupewa fedha ambazo mmoja wao zimemsaidia
kujenga nyumba haraka.
Wenyeviti wa Chadema waliojiuzulu ni Wilfred Kitandu wa
mkoa wa Singida na Ally Chitanda wa Lindi, ambao walifikia uamuzi huo baada ya
Zitto kuvuliwa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, ambaye
alivuliwa ujumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho.
Hata hivyo, Dk. Slaa
hakufafanua kama wenyeviti hao walihogwa na nani.
Akizungumza jana na mamia ya
wananchi wa kijiji cha Nyalubanda Jimbo la Kigoma Kaskazini waliohoji sababu za
Chadema kuchukua hatua za kumsimamisha Zitto uongozi, alisema chama hicho
kinafanya kazi kwa kuzingatia katiba yake.
Dk. Slaa akihutubia wananchi hao
huku mvua ikinyesha iliyoambatana na ukungu mzito, alisema katiba ya Chadema
haina kipengele kinachotaka chama hicho kinapotaka kuchukua hatua dhidi ya
kiongozi au mwanachama aliyefanya kosa hadi suala hilo waulizwe wananchi.
"Nilichogundua
wenyeviti waliojiuzulu nyadhifa zao wamenunuliwa kwa pesa na mmoja wao baada ya
siku mbili tatu, alijenga nyumba na amekuja kupiga magoti akiomba arudi Chadema,
lakini hatuwezi kumkubalia," alisema Dk. Slaa bila kumtaja jina.
Dk. Slaa
alisema wananchi na wanachama lazima watambue kuwa Chadema haijawahi kutetereka
toka mwaka 2011, hivyo wanaodhani inaweza kutokea hivyo baada ya hatua
zilizochukuliwa dhidi ya Zitto wanajidanganya.
Alisema kiongozi yeyote au
mwanachama atakayekiuka au kuvunja maadili na misingi ya katiba ya chama hicho
awe ni Dk. Slaa, Mbowe au Mtei, lazima atachukuliwa hatua za kinidhamu
kulingana na katiba.
Alitoa mfano mwaka 2011 madiwani wa Chadema mkoa wa
Arusha walipobainika kukiuka kanuni za chama, walichukuliwa hatua na hadi sasa
chama hakijayumba na kinadunda.
Alisema wananchi wakiwamo wa Kigoma wasiumize
kichwa kwa hatua zilizokwisha chukuliwa dhidi ya Zitto kwa sababu suala hilo siyo
la kwanza kuchukuliwa kwa kiongozi anayebainika kukiuka katiba ya chama.
Dk.
Slaa alisema kabla ya Zitto, Dk. Kitila na Samson Mwigamba, kuchukuliwa hatua
hizo, waliitwa na kuhojiwa kwenye vikao vya chama.
"Utakuwa mtu wa ajabu
una kansa inakutafuna unataka uiache iendelee kukutafuna hadi kwenye moyo
ambako huwezi kukata ni bora kuikata kabla haijafika sehemu ambayo
haitawezekana kukatwa," alisema.
Dk. Slaa alisema hatua zilizochukuliwa
dhidi ya Zitto hazina uhusiano wowote na suala la Zitto kuhoji ukaguzi wa
hesabu katika vyama.
Juzi, Dk. Slaa alipowasili mjini Kigoma alipokelewa kwa
kishindo na mamia ya wananchi huku pikipiki zaidi ya 150 na magari zaidi ya 20
yakiandamana kumlaki.
Source: Mwanakatwe T. ( Dec. 2013). `Chadema haijakurupuka kuwasimamisha Zitto, Kitila`. Retrieved from Ippmedia/Nipashe

No comments:
Post a Comment