UTANGULIZI
Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
iliyokutana Ubungo Plaza, Dar es Salaam kuanzia asubuhi ya siku ya Jumatano ya
tarehe 20 Novemba, 2013 hadi alfajiri ya leo Ijumaa tarehe 22 Novemba, 2013
imetafakari na kujadili kwa kina taarifa mbali mbali juu ya hali ya kisiasa ndani
na nje ya Chama chetu ambayo kwa muda mrefu imegubikwa na tuhuma kubwa na nzito
dhidi ya Chama chetu na viongozi wake wakuu, yaani Mwenyekiti wa Taifa,
Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (MB), na Katibu Mkuu, Dk. Wilbrod Peter Slaa.
Tuhuma hizi zilikuwa na malengo na athari ya kuwapaka matope na kuwachafua
viongozi wakuu wa Chama na Chama chenyewe, kutengeneza mtandao wa siri ndani na
nje ya Chama ambao hatimaye ungefanikisha sio tu lengo la kufanya mapinduzi nje
ya utaratibu wa kikatiba wa Chama, bali pia ungekipasua Chama vipande vipande
na hivyo kuua matumaini ya Watanzania juu ya uwezekano wa kufanya mabadiliko ya
kisiasa na kiuchumi na kijamii katika nchi yetu kwa kukiondoa madarakani Chama
cha Mapinduzi (CCM).
Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA, Uchunguzi wa Kamati Kuu umebaini kuwepo kwa mkakati mkubwa wa
kutimiza malengo hayo ambao umeandikwa katika waraka unaoitwa ‘Mkakati wa
Mabadiliko 2013.’ Mkakati huu uliandaliwa na kikundi kinachojiita ‘Mtandao wa
Ushindi’ ambacho vinara wake wakuu ni wanne, yaani Naibu Katibu Mkuu na Naibu
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe
ambaye kwenye waraka huo anajulikana pia kama ‘MM’ au ‘Mhusika Mkuu’; mjumbe wa
Kamati Kuu na mwanazuoni kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kitilla
Mkumbo ambaye kwenye waraka anajulikana pia kama M1; Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa
wa Arusha ambaye kwa sasa amesimamishwa uongozi, Bwana Samson Mwigamba na
ambaye kwenye waraka anaitwa M3; na mtu mwingine ambaye hadi sasa jina lake halijajulikana
lakini kwenye waraka anajulikana kama M2 na anatajwa kuwa yuko ‘ukingoni
kupigwa nje’ katika mageuzi ya kiutendaji yanayoendelea katika Sekretariat ya
Chama hapa Makao Makuu.
Kwa mujibu wa waraka wenyewe, “Mkakati huu umeandaliwa kwa
pamoja na M2 na M3 na kupitiwa na kurekebishwa na M1 ili upelekwe kwa MM kwa
maoni ya mwisho na kuanza utekelezaji.” Mbele ya Kamati Kuu, Dk. Mkumbo alikiri
kwamba MM au Mhusika Mkuu ni Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe; M1 ni yeye mwenyewe
Dk. Mkumbo na M3 ni Bwana Mwigamba. Dk. Mkumbo alikataa kata kata kumfahamu M2.
Aidha, Dk. Mkumbo alikiri mbele ya Kamati Kuu kwamba yote yaliyoandikwa katika
‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’ yametoka kwenye ‘Mtandao wa Ushindi’ na
hayajabadilishwa.
Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA, Mkakati wa Mabadiliko 2013 ni mpango wa kuipasua pasua CHADEMA
na kuiangamiza kabisa kwenye uso wa siasa za Tanzania. Huu sio mkakati wa
kufanya mabadiliko ya kiuongozi ndani ya Chama kwa njia za kidemokrasia na za
kikatiba. Ni mpango wa kukiteka nyara Chama na kukiua. Ndio maana watunzi wa
waraka huu wamesema kwenye waraka wao: “Tunahitaji kutekeleza mkakati huu kwa
siri kubwa ili mkuu aliyepo aendelee kubweteka na ndio maana hata lugha
iliyotumika ndani hapa ni ya pekee.” Kamati Kuu inaamini mkakati wenye malengo
halali ya kufanya mabadiliko ndani ya Chama kwa njia halali za kikatiba
usingependekeza kwamba: “Vikao vyetu na yeye (MM aka Mhusika Mkuu aka Naibu
Katibu Mkuu Zitto Kabwe) vitafanyika mara chache sana na mahali pa faragha
kupita kiasi ikiwezekana hata nchi jirani.” Aidha, Kamati Kuu inaamini kwamba
kama mkakati huu ungekuwa na malengo mazuri ya kukijenga Chama na sio kukiteka
nyara na kukiua, wanamtandao hawa wasingependekeza utaratibu ufuatao wa
utekelezaji wa mpango: “M1 (Dk. Mkumbo) ndiye atakayekuwa anawasiliana na
tunayemtaka ambaye ataitwa MM (Mhusika Mkuu). Tumepanga kwamba kusiwe na
mawasiliano mengi kati ya kamati na mhusika mkuu kuepuka tracking ya wapinzani
wetu. M1 ni mtu wa karibu na MM kwa hiyo mawasiliano yao hayataweza kutiliwa
shaka na mtu yeyote hata wangewasiliana mara nyingi kiasi gani. Hata hivyo,
linapokuja suala la mkakati huu tunasihi mawasiliano yawe kwa kuonana uso kwa
uso ama kwa simu na si sms. M1 ndiye atakayewasilisha mambo yote yanayotoka
kwenye kamati ya kitaifa na endapo kuna haja ya MM kukutana na kamati ya
kitaifa, mipango yote ya kikao itafanywa na M1 kwa usiri mkubwa.”
Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA, Mkakati wa Mabadiliko 2013 ni mpango haramu na ambao unaichana
chana Katiba ya Chama chetu. Ni mkakati wa vita dhidi ya Chama chetu na
utaratibu wetu wa kikatiba. Wakati ibara ya 10.1(iv) ya Kanuni za Uendeshaji Kazi za Chama
ambazo ni sehemu ya Katiba ya Chama chetu ya mwaka 2006 inamkataza kiongozi wa
CHADEMA asijihusishe na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini, au ukanda
ambavyo vina makusudi ya kubaguana ndani ya Chama na miongoni mwa jamii kisiasa
au kijamii”, wanaMtandao wa Ushindi wameonyesha wazi kuwa wanaendekeza siasa za
udini kwa kusema yafuatayo juu ya waliemwita ‘mtu tunayemtaka’, yaani Naibu
Katibu Mkuu Zitto Kabwe: “Kwa kuwa ni Mwislamu, hii ni fursa katika kupata
kuungwa mkono na wanachama waislamu ambao wamekuwa na kigugumizi wakidhani
waislamu hawatakiwi katika uongozi wa taasisi yetu.”
Wakati ibara ya 10.1(viii) ya Kanuni za Uendeshaji inamtaka kila
kiongozi wa CHADEMA “... kuwa mkweli na muwazi wakati wote ... na aachane na
vikundi vya majungu na wadanganyifu (rumour mongers) ...”, wanaMtandao wa
Ushindi wameeleza kwenye waraka wao kwamba mipango yao ya utekelezaji wa
Mkakati wa Mabadiliko 2013 ‘itafanyika kwa usiri mkubwa.’ Wakati ibara ya 10.1(ix) ya Kanuni za Uendeshaji Kazi za Chama
inamtaka “kiongozi asijihusishe na vikundi na vitendo vya kuchonganisha au
kuzua migogoro ndani ya uongozi wa chama au wanachama wake”, wanaMtandao wa
Ushindi wamesambaza tuhuma za uongo dhidi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa (ambaye
wanamwita kwenye waraka wao kuwa ni ‘Mpinzani wetu’) kuwa “... hana mahusiano
mema na mazuri na viongozi wa ngazi za chini kutokana na dharau nyingi anazozionyesha
pale anapokutana na viongozi wa ngazi za chini akiwa katika kuijenga taasisi
hii.... Hii imemfanya kutopendwa na viongozi wengi wa ngazi za chini hivi sasa
na kutoa fursa ya pekee kwa tunayemtaka.”
Wakati ibara ya 10.1(x) ya Kanuni za Uendeshaji inamtaka
“kiongozi asitoe tuhuma zozote juu ya viongozi wenzake pasipo kupitia vikao
halali na kuzingatia taratibu na ngazi zilizowekwa kwenye Kanuni”, tuhuma zote
zilizotolewa na wanaMtandao hawa dhidi ya viongozi wakuu wa Chama chetu
hazijawahi kutolewa na yeyote kati ya wanaMtandao hawa katika kikao chochote
halali cha Chama cha ngazi yoyote.
Wakati ibara ya 10.1(xii) ya Kanuni za Uendeshaji inaeleza
kwamba “itakuwa marufuku kwa kiongozi wa CHADEMA kukashifu Chama, kiongozi au
mwanachama yeyote wa Chama ...”, Mkakati wa Mabadiliko 2013 umejaa kashfa
kubwa, matusi mengi na udhalilishaji mkubwa wa Chama, viongozi wake wakuu na
wanachama kwa ujumla. Hivyo, kwa mfano, Mwenyekiti wa Chama Taifa ametuhumiwa
na wanaMtandao hawa kuwa ni mtu mwenye ‘uzalendo unaotia shaka’, mwenye ‘elimu
ya magumashi’, ‘mzito kujieleza’, ‘mtu mwenye akili ndogo’, n.k.
Ndugu wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA, Hakuna chama au taasisi yoyote duniani inayoweza kunyamazia
mkakati wa aina hii dhidi yake na viongozi wake wakuu na ikadumu au kubaki
salama. Chama au taasisi yoyote inayoendekeza vitendo vya aina hii miongoni mwa
viongozi wake wa ngazi yoyote au miongoni mwa wanachama wake wa kawaida
inakaribisha kifo na mauti. Chama chetu na viongozi wake wa juu wamekaa kimya
kwa muda mrefu sana; wamevumilia mashambulizi na kashfa nyingi sana dhidi yao
binafsi na dhidi ya Chama; wamestahimili matusi makubwa sana dhidi yao. Chama
chetu kimevumilia yote haya na viongozi wake wamevumilia yote haya sio kwa
sababu walitaka Chama chetu kiuwawe na wanaMtandao hawa. Uvumilivu wote huu
ulitokana na haja ya kuwapa wanaMtandao wa Ushindi fursa ya kugundua hatari ya
siasa zao na kuwapa muda wa kujirekebisha na kujirudi.
Kama ilivyo kwa binadamu au taasisi yoyote ile, uvumilivu wa
Chama chetu na viongozi wake wakuu una kikomo. Na hiki ndio kikomo cha
uvumilivu wa Chama chetu, viongozi wake na wanachama wake kama
wanavyowakilishwa na Kamati Kuu ya Chama chetu. Hivyo basi, katika kikao chake
tajwa, Kamati Kuu ya Chama chetu, kwa kutumia mamlaka yake ya kikatiba ya
dharura chini ya ibara ya 6.5.2(d) ya Katiba ya Chama, imeazimia yafuatayo
kuhusu Mkakati wa Mabadiliko 2013 na hao wanaojiita wanaMtandao wa Ushindi:
Kwamba, kuanzia sasa, viongozi wote waliohusika ama kuhusishwa
na mkakati huu, yaani Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe, Mjumbe wa Kamati Kuu Dk.
Kitilla Mkumbo na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha Samson Mwigamba wavuliwe
nyadhifa zao zote za uongozi ndani ya Chama; Kwamba timu ndogo ya pamoja ya watendaji wa Sekretariat ya Makao
Makuu ya Chama na wajumbe wa Kamati Kuu ifanye uchunguzi wa haraka ili
kumtambua mtu anayeitwa M2 na ambaye anadaiwa kuwa mtumishi wa Makao Makuu ya
Chama ili hatua stahiki na za haraka zichukuliwe dhidi yake, pamoja na watu
wengine wote watakaobainika kuhusika na mpango huu wa uhaini dhidi ya Chama
chetu; Kwamba Kamati ya Chama ya Wabunge inaelekezwa kuchukua hatua za
haraka za kuhakikisha Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe anavuliwa madaraka yake
yote kama Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, with immediate
effect;
Kwamba viongozi waliotajwa katika aya ya (a) waandikiwe hati
zenye tuhuma dhidi yao haraka iwezekanavyo na watakiwe kujieleza kwa nini
wasifukuzwe kwenye Chama kwa vitendo vyao na wapatiwe fursa kamili ya kujitetea
kama inavyotakiwa na ibara ya 6.5.2(a), (b) na (c) ya Katiba ya Chama; Kwamba mara baada ya utekelezaji wa azimio (d), Kamati Kuu
ikutane kwa dharura kwa ajili ya kufanya uamuzi juu ya hatma ya watuhumiwa na
hatua nyingine zitakazofuata; Kwamba waraka wa wanaojiita wanaMtandao wa Ushindi uwekwe
hadharani na usambazwe kwa vyombo vya habari vya aina zote ili wananchi wa
Tanzania, wanachama na viongozi wa Chama chetu na dunia nzima kwa ujumla iweze
kupima uzito wa Mkakati wa Mabadiliko 2013 na uhalali wa maamuzi haya ya Kamati
Kuu.
Ndugu wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA, Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu Dk.
Kitilla Mkumbo waliiomba Kamati Kuu iwaruhusu kujiuzulu nyadhifa zao baada ya
Mkakati wao wa kukiteka nyara Chama na kukiangamiza kujulikana mbele ya Kamati
Kuu. Kwa kuzingatia uzito wa makosa waliyokifanyia Chama, viongozi wake wakuu
na wanachama wake kwa ujumla; na kwa kuzingatia uzito na umuhimu wa nyadhifa
kubwa walizo nazo ndani ya Chama; na kwa kuzingatia uelewa wao wa Katiba,
Kanuni na taratibu za Chama na uzoefu wao katika safu za juu za uongozi wa
Chama, Kamati Kuu ilikataa kwa kauli moja kuridhia maombi hayo ya kujiuzulu.
Kufanya hivyo ingekuwa ni sawa na kuwaruhusu wajiondoe kwenye uongozi wa Chama
wakiwa na heshima wasizostahili hata kidogo.
Chama chetu ni tumaini pekee la Watanzania wote wanaotaka
mabadiliko ya kweli na ya kimsingi katika mfumo wa kiutawala, kiuchumi na
kijamii wa nchi yetu. Hii ndiyo sababu kubwa na ya pekee iliyosababisha vita
kubwa na chafu inayopigwa dhidi ya Chama chetu na viongozi wetu wakuu. Lengo
kuu ni kuwachafua viongozi wakuu, kuleta mgogoro na mgawanyiko ndani ya
wanachama, viongozi wake na hivyo kukichafua Chama mbele ya macho ya Watanzania.
Chama chetu kikishachafuka kwa mtindo huu, matumaini ya Watanzania wanaotaka
mabadiliko yatakufa. Vita hii kubwa haijaanza jana, na haitaisha kesho. Kama
ambavyo tumekabiliana nayo na kuishinda siku za nyuma, vivyo hivyo
tutakabiliana nayo mara hii na kuishinda. Kama Chama chetu kilivyoibuka na
nguvu na heshima kubwa zaidi katika mapambano ya siku za nyuma, vivyo hivyo
Chama chetu kitaibuka na nguvu na heshima kubwa zaidi katika awamu hii ya
mapambano.
Tunawaomba Watanzania, wanachama na viongozi wetu wasife moyo,
bali waendelee kukiunga mkono chama chao cha ukombozi. Tunawaomba Watanzania,
wanachama na viongozi wetu waendelee kulilinda tumaini lao pekee la mabadiliko
ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. Badala ya kukatishwa tama,
kila mmoja wetu aongeze bidii maradufu ili kuwashinda wale wanaotaka kuleta
majanga katika Chama chetu na kwa Taifa letu.
------------------------------------------
FREEMAN AIKAELI MBOWE (MB) - MWENYEKITI, TAIFA
------------------------------------------
WILBROD PETER SLAA - KATIBU MKUU
No comments:
Post a Comment