Asante ... kwa uchambuzi wenye
tafakuri tunduizi. Nitajaribu baadaye kufuata nyazo zako. Lakini kitu kimoja
kiko wazi. Chadema kama taasisi imechukua uamuzi sahihi. Kaulimbiu ya CCM ya
tangu Aprili 2012 ni eti "Umoja ni Ushindi" hivyo malumbano ya
kutuhumiana ufisadi na UGAMBA yanabomoa umoja na kupunguza uwezekano wa ushindi
kwa hiyo lazima kuwavumilia viongozi wandamizi walio na nguvu ndani ya CCM vile
kuwavua vyeo vyao katika chama kutatufanya tushindwe kushinda katika chaguzi.
Chadema imetekeleza kaulimbiu
mbadala na kusema; hapana, viongozi wandamizi wanaocheza karata nje ya uwanja
na kuandamwa na tuhuma za usaliti tutathubutu kuwavua uongozi hata kama hilo
litayumbisha chama kwa muda kwa sababu ya umaarufu wao au kuwa kwao na uwezo
mkubwa wa uchambuzi wa mambo hautakizua chama kama taasisi kuwavua vyeo au hata
kuwafukuza uanachama.
Mfano wa Dakta Salim Ahmed Salim ni
muafaka hapa. Alipigwa vita na kutuhumiwa hata mauaji ya mwaasisi wa Zanzibar
ya baada ya Mapinduzi lakini hata baada ya kuzushiwa mambo mengi ya hovyo na
mwisho wa siku CCM kikashinda uchaguzi 2005 bendera yake ikipeperushwa na
mgombea ambaye hakuwa na sifa za uadilifu na umahiri wa uchambuzi wa masuala ya
kitaifa na kimataifa wa kulingana na wa Dakta Salim Ahmed Salim . Lakini vile
yeye ni mwenye hulka ya unyenyekevu na kutojiona bora kuliko wenzake na
kutotawaliwa na dhana ya kuwa bila yeye kuwa Rais basi hakuna la maana chama
chake kingeweza kikafanya, aliendelea kuwa mwanachama wa CCM na mwaka 2010
alijitokeza kumpigia kampeni ya urais kipindi cha pili mgombea ambaye mtandao
ulimbeba 2005.
Bila shaka mgombea wa urais wa CCM
wa 2005 na 2010 alinufaika na kuchafuliwa kisiasa kwa Dakta Salim. Labda
tofauti ya wale waliovuliwa uongozi na Chadema na Dakta Salim Ahmed Salim ni
wao kutokuwa na nidhamu ya kichama cha ukombozi ambayo inadai kuwa au ujiondoe
kama hujaridhika na uongozi uliopo au ukibaki basi uwe tayari kuvumilia
kuchafuliwa na wale wasio na uwezo wa kiakili kama wewe pale unapotaka
kuwaondoa madarakani tena kwa kucheza nje ya uwanja wa mchezo wa siasa
unaofuata sheria zinazotungwa na wale wale ambao kwa wakati huo ndio wenye
uwingi wa kura katika vikao halali za chama husika.
Vinginevyo wewe utakuwa unakisaidia
chama tawala cha CCM kwa kuanzisha zogo kuhusu eti mapungufu ya viongozi
waliopo kwa kujiaminisha kuwa wewe ni bora kuliko wao ambapo na wao wanajiona
ni bora kuliko wewe. Kwani Kambona si alikuwa kiongozi mahiri na mwenye maono
kuliko hata wazee wetu kama Mzee Kawawa? Lakini historia ya TANU ikiandikwa
yeye ataonekana msaliti na Mzee Kawawa ataonekana shujaa, siyo? Kwani Rais
Reagan na Rais George Bush ndio walikuwa wenye akili na umahiri kuliko viongozi
wa Republican Party ya enzi zao au ndio walikuwa muafaka kuongoza ili kuleta
umoja ndani ya chama?
Alipokufa Dakta Mondlane ni kwa
nini wasomi kama Marcelino dos Santos walimpisha Samora Machel kuongoza Frelimo
kama si kutii dhana ya nidhamu ya juu ndani ya chama cha ukombozi kuzuia
kuanzisha migogoro inayowasaidia watawala wa wakati huo kujinadi kama wenye
utulivu na hivyo kutokuwepo na mbadala. Kwa nini hadi leo Malkia wa Uingereza
ni mama Elizabeth badala ya Prince Charles? hivi kuongoza taasisi lazima
aliyeonekana anafaa lazima awe mwenye akili au umahiri wa uchambuzi wa mambo
kuliko wenzake?
Kuanzisha mtandao wa siri wenye
lengo la kubadili uongozi wa juu wa chama cha ukombozi ni usaliti na anayeandaa
mkakati huo wa siri hawezi kujinadi kama eti mwanademokrasia, yeye ni
mwanamakundi ya siri siri ndani ya chama husika kama hao anaowatuhumu yeye kuwa
na makundi yao yakuwadumisha kwenye uongozi. Haiwezekani kusema ni sawa kutumia
mbinu za kisirisiri nje ya utaratibu uliopo halafu ukajinadi kuwa mtetezi wa
demokrasia na wenzako eti wahafidhina.
Ningewaelewa hawa waliovuliwa
uongozi kama wangejenga hoja hiyo ndani ya chama chao kwa uwazi kabisa na hoja
hiyo ikikosa kupata kuungwa mkono basi wangetulia na kujaribu tena na tena hadi
hoja yao ipate kuungwa mkono na wajumbe wengi wa vikao husika vya chama chao.
Vinginevyo wangejitoa uanachama wa chama husika. Hivyo ndivyo mwanademokrasia
anavyotarajiwa kufanya. Mimi nilijitoa TANU tangu 1973 na sijarudi CCM hadi leo
vile najua hoja zangu zitakuwa na uungwaji mkono finyu kwa sasa katika vyombo
vya maamuzi, labda pale CCM kikiondolewa madarakani kikabaki na waumini wa
kweli wa ujamaa na umajumui wa kiafrika.
Kama wewe ni akina Abdul Nasser
anayepanga mapinduzi ya kutumia nguvu kisisiri basi sema hivyo nayo inaitaji
ujipange kufanikisha hilo wakati muafaka na ukishindwa katika mipango yako
kubali kushindwa na anzisha chama chako au kama Ndugu yangu Mabere Marando
jiunge na chama unachokubaliana nacho zaidi ya hicho ulimo.
Haiwezekani eti chama cha maana
kiogope kuondoka kwa wanachama wafuasi wa mwanachama au kiongozi mmoja au
wawili au watatu wanaojiona wao ni bora kuliko wenzao. Kwa kitendo cha Chadema
kuwavua uanachama viongozi wao wanadamizi wanaokiri tena na tena kuwa walisuka
mtandao wa siri wa kuwaondoa katika chaguzi zijazo viongozi wenzao wanaowaona
wao kuwa ni wahafidhina na wao ni wanademokrasia ni kitendo cha ujasiri na
kujenga uhalali wa kudumu wa Chadema hata kama kitayumba na kutorokwa na
wanachama kiasi kidogo au kikubwa kwa sasa na hata kukosa ushindi kwenye
changuzi za wakati huo.
Uchambuzi wenye kusukumwa na
tafakuri tunduizi unanituma niseme heko Chadema kwa kuthubutu hata kama chama
kitashindwa katika uchaguzi wowote ujao. Kitendo hiki pekee kimeonesha njia kwa
kusema kuwa dhana ya "Umoja ni Ushindi" ni dhana bora kuacha
itekelezwe na CCM ya mafisadi ambao kwao kuwa na timu ambayo ina akina Ronaldo
kibao kila mmoja akikimbia na mpira kufunga yeye badala ya kutoa pasi ni jadi
ya CCM ya leo. Lengo ni labda kutafuta kumzidishia umaarufu Ronaldo mhusika
binafsi na labda kwa CCM ya sasa hilo ni sawa kwa vile CCM haijioni kama chama
cha ukombozi tena bali chama dume na chama tawala milele na milele. Chadema ya
Freeman Mbowe, Dakta Slaa, John Mnyika, Mabere Marando, Prof Baregu na Prof
Safari, kutaja wachache, ni bora iendelee kujiona kama chama cha ukombozi kuona
ni sawa kukataa dhana ya ki-CCM ya "Umoja ni Ushindi"
Uchambuzi wangu unaweka kando
urafiki na udugu wa kifamilia wa karibu kati yangu na Dakta kitila Mkumbo na
mwanangu Zitto Kabwe na heshima na mapenzi yangu kwao kama wachambuzi mahiri wa
mambo vinabaki pale pale. Wanaweza kuishi bila hata kuwakwenye chama chochote
kama mimi na bado wakaendelea kutetea mabadiliko Tanzania katika nafasi zao
katika jamii.
No comments:
Post a Comment