BUNGE limeitaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba kulipa deni la pango la sh bilioni 1.2 kwa Wizara ya Mambo ya Ndani, badala ya kuendelea kulitumia jengo lao bila malipo. Agizo hilo lilitolewa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali, Abdul Marobwa, baada ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mbarak Abdulwakil, kusema jengo hilo ni mali ya wizara yake. Kwa mujibu wa katibu mkuu huyo, lilijengwa kwa makusudi ya matumizi ya wizara kutokana na ofisi zake nyingine kulazimika kupanga kwa kukosa eneo. Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji mstaafu Joseph Warioba imelitumia jengo hilo kwa miaka miwili bila kulipa chochote wakati Wizara ya Mambo ya Ndani ikidaiwa fedha na mkandarasi wa jengo hilo.
Abdulwakil alisema ofisi yake ilipokea ombi kutoka serikalini la kutoa ghorofa tatu kati ya nane zilizopo kwenye jengo hilo, kwa ajili ya matumizi ya tume hiyo. Alisema kabla ya kukubali ombi hilo alipokea barua nyingine iliyomtaka kuliachia jengo lote la ghorofa nane litumiwe na tume ya Jaji Warioba. “Niliridhia agizo hilo nikitarajia kwamba ofisi yangu itapata malipo hasa kwa kuzingatia kuwa wizara yetu ilikuwa na uhaba wa ofisi… lakini hadi sasa tume ipo kimya inaendelea kulitumia jengo bila malipo,” alisema Abdulwakil mbele ya wajumbe wa kamati hiyo. Madai hayo yaliibua hoja miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo waliohoji sababu za tume kushindwa kulipa pango ambapo Mbunge wa Viti Maalumu, Zainab Vullu, aliitaka tume hiyo itoe maelezo ya kushindwa kulipa pango huku akisisitiza Bunge liliidhinisha fedha za pango kwa tume hiyo wakati inaundwa.
Source: Mark I. (Oct. 2013).Tume ya Warioba yadaiwa bil. 1.2/- za pango. Retrieved from Tanzania Daima

No comments:
Post a Comment