Na Mwandishi wetu, ALABAMA,
Marekani
ZIARA ya Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa nchini Merekani imezidi
kuwa gumzo kutokana na mapokezi makubwa anayoyapata katika maeneo mbalimbali,
huku akiinanga Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa ina ukubwa wa Baraza
la Mawaziri lisilokuwa na tija. Dk. Slaa ambaye yuko Marekani kwa
siku kadhaa katika ziara yake iliyoandaliwa na umoja wa vyuo vikubwa nchini
humo ya kujifunza mambo mbalimbali, juzi aliingia katika jimbo la Alabama na
kupokelewa na wakuu wa jimbo hilo akiwemo Gavana Robert J. Bentley pamoja na
Waziri wa Biashara.
Alabama ambayo uchumi wake
ulitegemea kilimo kwa asilimia 90 ni moja ya majimbo yaliyokuwa nyuma sana
kiuchumi na kimaendeleo siku za nyuma, lakini miaka 25 iliyopita, viongozi wake
walibuni mikakatati ya kuibadilisha. Kwa sasa jimbo hilo ndilo moja ya majimbo
yenye viwanda vikubwa vya magari kama Honda, Mercedes Benz, Airbus, Hyundai,
Raytheon, Space Station, Wallgreens na mengineyo, na uchumi wake unakua kwa
kasi kubwa. Kupitia kaulimbiu yake ya “Vision
Tanzania” Dk. Slaa alipata nafasi ya kukutana na viongozi wa jimbo hilo ili
aweze kujifunza mbinu ambayo ataweza kuwarudishia Watanzania ili nao waondokane
na umasikini. Kwa mujibu wa taarifa za mitandao ya kijamii, gavana wa jimbo hilo
pamoja na mawaziri wake, wako tayari kushirikiana na Tanzania kwenye mambo ya
biashara, hasa miundombinu ikiwemo bandari na ujenzi wa madaraja na bandari.
Katika ziara yake jimboni humo, Dk.
Slaa na mkewe Josephine walipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo
bandari kubwa. Katibu mkuu huyo, alisema kuwa alichojifunza ni kwamba, serikali
inaweza kuwa na ufanisi hata ikiwa na baraza dogo la mawaziri. Kwamba Jimbo la
Alabama lina mawaziri sita tu, huku Serikali ya CCM ikiwapa walipakodi wa Tanzania
mawaziri zaidi ya 50 wasiokuwa na kazi. “Mawaziri wengi wana matumizi
makubwa huku wakina mama wakijifungua sakafuni, walimu wakinyimwa haki zao,
polisi na wanajeshi wakiishi hali duni na wanafunzi wakisoma chini ya miembe.
CCM ni janga kubwa lililowakumba Watanzania,” alinukuliwa Dk. Slaa.
Katika ziara hiyo, Dk. Slaa alipata
nafasi ya kutembelea Chuo Kikuu cha Auburn ambacho ni moja ya vyuo vikuu
vikubwa zaidi vya utafiti duniani. Auburn inafanya shughuli zake
nchini Kenya, Uganda, Senegal na kwingineko barani Afrika. Nchini Kenya, Auburn
inawasaidia wakulima mbalimbali hasa wafugaji wa samaki kutumia teknolojia ya
kisasa inayowawezesha kusafirisha samaki wengi kwenda Ulaya. Katika Kenya na Uganda, utafiti wao
umetoa zaidi ya ajira 7,000. Kwamba watafiti hao walipoulizwa
kwa nini walikwepa Tanzania, walidai kuwa ni vigumu sana kufanya kazi wakitaja
kuzuiwa na vitendo vya ufisadi ingawa wangekuja na fedha zao kutoka Benki ya
Dunia na Shirika la Kimarekani la Misaada (USAID) ambayo inadhamini miradi yao
sehemu nyingi barani Afrika ikiwemo Kenya na Uganda.
Taarifa hiyo ilidai kuwa viongozi
wa chuo hicho wako tayari kurudi Tanzania ikiwa mazingira ya kazi yatabadilika
hasa kukiwepo na serikali mbadala, ambayo Dk. Slaa amewahakikishia kwamba
CHADEMA iko tayari kufanya nao kazi. Kwamba viongozi wa Auburn wako tayari
kusaidia vyuo vya Tanzania kama kile cha Kilimo cha Sokoine mkoani Morogoro kwa
kuwafundisha walimu na pia kubadilishana nao teknolojia za kisasa za kilimo
pamoja na kuwafundisha wakulima wa aina zote na hata walaji mbalimbali. Dk. Slaa alifika pia katika moja ya
bandari kubwa nchini Marekani ya Mobile Alabama ambako alipokelewa na
Mkurugenzi wa Shirika la Bandari ya Alabama. Akiwa hapo alielezwa kuwa shirika
hilo linapitisha makontena 100 kwa saa moja na mizigo inayozidi tani milioni 30
kwa mwaka na kuipa bandari hiyo inayojitegemea kiasi cha dola za Kimarekani
milioni 152 kwa mwaka ambazo ni faida.
Shirika hilo la bandari lina
wafanyakazi 600 tu, lakini limeweza kutoa ajira ambazo siyo za moja kwa moja
280,000. Akieleza kile alichojifunza bandarini hapo, Dk. Slaa alisema kuwa
mashirika ya umma yanaweza kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa pasipo uingiliaji wa
kisiasa. Dk. Slaa pia alijifunza kwamba kama
jimbo dogo kama Alabama linaweza kupitisha tani milioni 30 kwa mwaka, basi
Tanzania inaweza kupitisha tani milioni 100 kwa mwaka kutokana na jiografia
yake. Alisema kuwa anaamini kwamba
bandari ya Tanzania inaweza kuajiri vijana 350,000 chini ya utawala wa CHADEMA. Kwa mujibu wa Dk. Slaa, anaamini
kwamba mashirika ya umma kama bandari hayana ufanisi kwa sababu waendeshaji
wake wanateuliwa kiurafiki na kindugu bila ya kuzingatia uwezo wa mtu. “Chini ya utawala wa CHADEMA haya
yote yatafikia kikomo kwa manufaa ya Watanzania wanaoumia na umasikini,”
alisema.
Pia Dk. Slaa alikutana na viongozi
wa juu wawili wa Baraza la Biashara la Alabama katika chakula cha jioni
kilichoandaliwa kwa ajili yake na taasisi hiyo. Mwenyekiti wa baraza hilo,
ameahidi kuhamasisha makampuni makubwa kwenye jimbo la Alabama kumsaidia Dk.
Slaa na CHADEMA kunyanyua uchumi wa Tanzania kwa kuwekeza kwenye sekta
mbalimbali za uchumi kama kilimo, elimu, viwanda, miundombinu na nishati.
No comments:
Post a Comment