CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Idara ya Habari ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
tangu ilivyopokea kwa masikitiko na mshituko mkubwa taarifa za Serikali ya CCM,
kufungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania, imeendelea kufuatilia kwa ukaribu
hatua zinazochukuliwa na kauli mbalimbali zinazotolewa na pande zote mbili,
serikali na wadau wa uhuru wa habari na vyombo vya habari.
Ni wazi bila shaka yoyote kuwa kwa mara nyingine tena, serikali
hii, imeendelea kutumia sheria mbaya na madaraka vibaya kufanya uamuzi mbaya,
kila inapokosa hoja na uwezo wa kukabiliana na sauti mbadala au maoni kinzani.
Imeamua kuwa tishio kwa uhuru wa habari, vyombo vya habari na maoni.
Suala hili limekuwa dhahiri zaidi baada ya Serikali kuamua hata
kuanza kuingilia uhuru wa habari na maoni kwenye mitandao ya kompyuta (on line)
na pia kutishia kulifungia Gazeti la Rai, linalotolewa na Kampuni ya New Habari
(2006) Limited, kwa sababu limeanza kuchapiswa kila siku badala ya Alhamis
pekee kama ilivyozoeleka.
Wakati wamiliki wa gazeti hilo wametoa ushahidi unaotokana na
nyaraka za serikali hiyo hiyo iliyotoa idhini kwa chombo hicho kuchapishwa kila
siku, Serikali yenyewe kwa upande wake imetoa utetezi wa ajabu juu ya tishio
lake hilo ikijitetea kuwa kibali hicho kilitolewa kwa Kampuni ya Habari
Corporation iliyouza hisa zake kwa Kampuni ya New Habari (2006) Limited.
Katika hili serikali imeanza kujichanganya. Inadhihirisha wazi
kwamba uamuzi wake huo wa kufungia vyombo vya habari, ni mwendelezo wa maamuzi
ya kibabe, yanayofanywa bila kuzingatia maslahi ya Watanzania, ndiyo maana
yanaanza kuipatia taabu jinsi ya kujibu na kujenga hoja za kutetea uovu wake.
CHADEMA, inapinga na itaendelea kupinga kwa kauli na vitendo,
hatua hii ya serikali yenye lengo ovu dhidi ya umma wa Watanzania.
Hoja si maudhui
Kama kawaida yake, serikali kupitia kwa Mkurugenzi wa Habari
Maelezo, Asa Mwambene, imeamua kuja na hoja ya ‘maudhui’ kuwa ndiyo uwe msingi
mkubwa wa kuhalalisha kitendo hicho kibaya cha kufungia magazeti kwa kutumia
Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976.
Tunasema hapa hoja haiwezi kuwa maudhui yaliyosababisha magazeti
hayo kufungiwa kama ambavyo serikali ya CCM siku zote imejaribu kuonesha kila
inaposhughulikia vyombo vya habari, suala la msingi ni utaratibu unaotumiwa
kuviadhibu au kuviwajibisha.
Serikali haiwezi kuwa hakimu wa kesi yake yenyewe. Halikadhalika
haiwezi kufanya kazi zote; kulalamika, kutuhumu, u-polisi (kupeleleza),
kuendesha mashtaka na kisha kuhukumu. Hii ni kinyume kabisa cha misingi ya haki
ya asili. Ni ukiukwaji mkubwa wa haki.
Kama serikali ilifikiri vyombo hivyo vya habari vimekosea au
vimesema uongo, ilipaswa kusema ukweli ni upi, la sivyo ilipaswa kufungua
mashtaka mbele ya vyombo huru vinavyoweza kushughulikia masuala hayo; ama
ingepeleka malalamiko yake Baraza la Habari Tanzania (MCT), kama haina imani
nalo (kinyume na imani waliyonayo Watanzania wengi juu ya baraza hilo) basi
ingeenda kushtaki mahakamani.
Kinyume cha hapo ni kuendeleza uharamia dhidi ya uhuru wa
habari, vyombo vya habari na utoaji wa maoni. Kitendo cha kutisha na kufungia
vyombo vya habari kimekuwa ni moja ya mbinu ya serikali yoyote inayochagua njia
za kidhalimu kupambana na sauti mbadala, uhuru wa habari na maoni.
Hapa kwetu, mbinu hii kwa sasa imekuja wakati nchi na umma wote
wa Watanzania, kupitia taasisi, asasi na makundi mbalimbali ya kijamii, ukiwa
umeungana kuhoji dhamira ya watawala kutaka kuharibu na kukwamisha mchakato wa
Katiba Mpya.
Ni suala linalohitaji tafakuri yetu sote. Kwa nini serikali
imechukua hatua hii wakati huu ambapo nchi nzima iko kwenye mjadala wa Katiba
Mpya ambayo ni fursa adhimu ya taifa kujiumba upya na kuweza kuachana na sheria
mbovu kama hiyo ya mwaka 1976 inayompatia mamlaka waziri husika kufungia gazeti
kadri anavyoona ‘yeye’ inafaa?
Hivyo hapa kuna masuala kadhaa;
◦ Kuna kila dalili za wazi kwamba zipo njama za baadhi ya
watendaji wa serikali kufanya vitendo vya kutaka kuzuia maoni mbadala
yanayojaribu kupaza sauti (kwa niaba ya wasiokuwa na sauti) kuuhabarisha umma
juu ya uchakachuaji unaofanyika kwenye mchakato wa katiba mpya.
◦ Hatua ya kufungia vyombo vya habari sasa hivi ni jaribio la
kuleta hofu kwa vyombo vya habari (vingine) ili visiripoti kwa uhuru, mchakato
wa Katiba Mpya, hasa habari zenye mwelekeo wa kusema ukweli dhidi ya serikali
au watawala wanaotaka kukwamisha na kuharibu mchakato huo.
◦ Kutaka kuhamisha mjadala (diversion of discussion) mkali wa
katiba mpya unaoendelea kwa sasa, ili wananchi na taifa zima lianze kujadili
suala jingine, badala ya kuibana serikali, ili watawala wapate ahueni ya kupita
katikati kutekeleza dhamira yao kwenye mchakato huo nyeti.
◦ Pia kitendo hiki kinakwenda sambamba kabisa na msimamo wa CCM
kwenye Rasimu ya Katiba Mpya, ambapo chama hicho, kimekuwa kikipinga masuala
mengi ya msingi na muhimu kwa wananchi, likiwemo suala la haki za binadamu
lisiwe jambo la muungano na uwazi usiwe miongoni mwa tunu za taifa kwenye
katiba mpya.
Serikali ilipaswa kuonesha au kuiga mfano katika uwajibikaji.
Mathalani, itakumbukwa kuwa Kurugenzi ya Habari na Uenezi ya CHADEMA, ndiyo
taasisi pekee ya kisiasa nchini iliyosaini Azimio la Dar es Salaam Juu ya Uhuru
wa Uhariri na Uwajibikaji, lililopitishwa na Baraza la Habari la Tanzania
(MCT). Pamoja na ubora na upekee wa azimio hilo, barani Afrika na dunia
nzima kwa ujumla, si serikali wala viongozi wake ambao wameonesha kuunga mkono,
ili kuepuka vitendo kama hivi vya kidhalimu.
Idara ya Habari ya CHADEMA inapenda kutoa wito;
◦ Makundi na wadau mbalimbali walioathirika na kufungiwa kwa
magazeti haya wajitokeze wazi, wapaze sauti zao kuungana na makundi mengine ya
kijamii, asasi za kiraia na kitaaluma zinazopinga vitendo hivi. Hasa yale
ambayo habari zilizoandikwa na Magazeti hayo ya Mwananchi na Mtanzania,
zilikuwa zikiyahusu, mathalani;
· Vyama vya wafanyakazi (Habari ya
Mwananchi).
· Madhehebu ya dini (Habari picha ya
Mwananchi).
· Wale wote walioathirika na vitendo
(mauaji, mateso, kutekwa n.k) ambavyo vyombo vya dola vinatuhumiwa kuvifanya au
kuzembea kuchukua hatua kubaini ukweli (habari ya Gazeti la Mtanzania).
◦ Mjadala huu wa kuitaka serikali kuacha kutumia sheria mbovu na
kandamizi na kuyafungulia magazeti haya mawili, utiwe uzito na uende sambamba
na ule wa kulifungulia Gazeti la Mwanahalisi ambalo serikali hii iliyoamua
kugeuka kuwa tishio kwa uhuru wa habari na vyombo vya habari, iliamua
kulifungia kwa muda usiojulikana.
◦ Makundi mbalimbali ya kijamii ambayo yameungana kwa dhati kwenye
mchakato wa Katiba Mpya hasa kupinga dhamira ya serikali na CCM, kutaka
kuuharibu na kuukwamisha, kuzidi kuunganisha nguvu zao, kwani mchakato bora
utatupatia katiba mpya bora, ambayo itaondoa sheria mbovu kama hii ya magazeti
ambayo serikali imeendelea kuitumia kukandamiza umma wa Watanzania.
Tutalaani na kuchukua hatua
Watawala baada ya kufungia vyombo vya habari kadhaa huku jamii
ikikaa kimya, sasa wamefikia mahali wanafikiri wanaweza kuendelea kutekeleza
udhalimu huo huku jamii ikiangalia tu!
Tutachukua hatua. Tutapinga kwa kauli na vitendo. Wakati
tukilaani na kutoa wito kwa makundi mengine ya wadau wote wa masuala ya habari
kushikamana kwa dhati kupinga jambo hili kwa namna wanazoona zinafaa, CHADEMA
kwa upande wake, kwa kuanzia, kinaunga mkono wabunge wake (Zitto Kabwe na John
Mnyika) ambao wameonesha nia ya kuchukua njia za kibunge, ili kufuta sheria
yote ya magazeti ya mwaka 1976 au baadhi ya vifungu vyake vinavyotoa mamlaka
mabovu yanayotumiwa vibaya na watawala kwa ajili ya malengo mabaya.
Hivyo, katika kufanikisha hatua hiyo, tunatoa wito kwa watu wote
walioguswa na kitendo hiki cha ukandamizaji, wakiwemo wabunge waunge mkono njia
itakayochukuliwa na wabunge wa CHADEMA.
Imetolewa leo, Oktoba 2, 2013, Dar es Salaam na;
Tumaini Makene,
Ofisa Mwandamizi wa Habari CHADEMA
No comments:
Post a Comment