|
Mh. Wassirra |
WAZIRI wa Nchi, Ofisi
ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira, amesema wapinzani wasitarajie
tena kukaribishwa Ikulu, kutokana na msimamo wao wa kususia mjadala wa Muswada
wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013, wakati wa kikao
cha Bunge mjini Dodoma hivi karibuni, kwa majadiliano mengine. Waziri Wassira, alitoa kauli
hiyo siku moja baada ya wasomi, wanasiasa na wanaharakati kutoa ushauri wa
kumsihi Rais Jakaya Kikwete asisaini muswada huo ili kuwa sheria kamili, kwa
vile hauna tija kwa Watanzania.
Akizungumza na MTANZANIA jana juu ya ushauri
huo, Wassira alisema hoja na ushauri unaotolewa na makundi hayo hauna mantiki
kwa sababu taratibu zote za sheria zilifuatwa, kuanzia mwanzo hadi kuupitisha
muswada huo.
“Nianze kwa wanasiasa wa upinzani kususia na kutoka ndani ya
Bunge kwa hoja ya kutowashirikisha wananchi wa Zanzibar, hili si kweli, kwa
sababu Kamati ya Katiba na Sheria ilikwenda huko, sasa wasitake kulalamika na
kutaka kukutana na Rais Kikwete.
“Hawa tumewalea siku nyingi
na sasa wanafanya mazoea, ninachotaka kuwaeleza wasitarajie tena kuitwa Ikulu,
nchi hii inaongozwa na misingi na kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa
sheria.
“Kwanza kitendo cha Kiongozi wa Upinzani, Freeman Mbowe kutotii kiti
cha Spika wa Bunge ni dharau na alikiuka taratibu zinazoongoza Bunge, kwanza
alisababisha kuwapo vurumai ambazo zimeshusha heshima ya Bunge.
“Upinzani
wajue vurumai zao haziwezi kutengeneza Katiba wanayoitaka Watanzania, bali ni
kufuata taratibu pale wanapoona kuna kasoro, hivyo kulalamika kwao bila kufuata
taratibu hakutawasaidia kamwe.
“Kuna mazoea ya kwenda kwa wananchi
kuwadanganya, sasa tunasubiri tumesikia wanaandaa tamko lao la upinzani,
tutalisoma na kama wakienda kwa wananchi kueneza propaganda zao tutawafuata nyuma
na kuwaeleza ukweli wananchi,” alisema.
Alisema Watanzania milioni
45, hawawezi kuaminishwa uongo wakati Serikali ipo na kuongeza kwamba nchi
haiwezi kuendeshwa na vurugu wakati kuna vyombo vya dola vyenye mamlaka yake.
Kuhusu
ushauri wa wasomi kutaka Rais Kikwete kukutana na wanaolalamika, alisema
inategemea na utashi wake na jinsi atakavyoona inafaa.
Alisema imegundulika
wasomi wa vyuo vikuu mbalimbali wamekuwa wakitumia mwavuli wa elimu yao kutoa
maoni yao ambayo yanaonekana wazi ni ya itikadi ya vyama vya siasa.
“Hawa
wanaojiita wasomi wote wana itikadi ya vyama vya siasa, sasa badala ya kutoa
ushauri ambao utaonekana ni wa msomi, wanajikuta wanakuwa sehemu ya siasa tena.
“Sasa
watu kama hao inapaswa kuwaangalia kwa makini sana, kwa sababu wanafanya kazi
ya chama cha siasa kwa kutumia mwavuli wa usomi wake, hivyo hivyo kwa
wanaharakati, badala ya kufanya kazi kama ilivyoelekezwa kwenye usajili wao,
nao wanaingia kwenye siasa.
“Ninachowashauri, nchi hii
haiendeshwi kwa ubabe, bali inasimamiwa na sheria, hivyo kila mmoja akifuata
sheria hakuna ugomvi, pia haya madai ya kusema kuwa Katiba ijayo itakuwa ni ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) hayana msingi wowote,” alisema.
Juzi wasomi kutoka
vyuo mbalimbali, kikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha
Tunguu kilichopo Zanzibar na vingine, walitoa ushauri wao wa kumtaka Rais
Kikwete kufikiri zaidi na kuchukua tahadhari kabla ya kusaini muswada huo ili
kuwa sheria kamili.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Katiba na Sheria, Pindi Chana, alipoulizwa na MTANZANIA kuhusiana na malalamiko
hayo, alisema: “Kamati yangu ilifanya kazi iliyotumwa na taratibu zote
zilifuatwa.”
Source: Mases B. (Sept. 2013).Wassira: Wapinzani hatutawaita Ikulu. Retrieved from Mtanzania
1 comment:
Homo sapiens mtu wa kale alibadilika(evolution) hadi akawa binadamu kamili ,wassira mbona hubadiliki na kuwa binadamu kamili?
Post a Comment