Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Wednesday, September 11, 2013

Mbunge Mbilinyi asahau kutia saini dhamana


   
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (kushoto) akiwa na wakili wake, Tundu Lissu nje ya Kituo Kikuu cha Polisi mjini Dodoma, jana, ambako aliitwa kwa ajili ya kuhojiwa kutokana na vurugu zilizotokea bungeni Septemba 5 mwaka huu. Picha na Masoud Masas
          
 Polisi mkoani Dodoma, wamelazimika kumrudisha kwa mara ya pili Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi katika ofisi za Kituo Kikuu cha mjini hapa, baada ya kusahau kuweka saini katika dhamana yake. Mbilinyi maarufu Sugu, anatuhumiwa kumpiga askari, kuharibu kipaza sauti na kuchana koti la mpambe wa Bunge. Tukio hilo la kurudi kwa mara ya pili katika ofisi za upelelezi, lilitokeza jana baada ya Sugu kuripoti na kuruhusiwa kuondoka mahali hapo. Mbunge huyo ambaye aliitwa na mmoja wa maofisa wapelelezi wa jeshi hilo, alikuwa tayari ameshaingia ndani ya gari tayari kwa kuondoka katika eneo hilo. Akiwa katika hali ya ucheshi na kufikia hatua ya kugongeshana mikono na afisa huyo wa polisi, aliingia katika ofisi za upelelezi na kutoka baada ya dakika 15.
       Wakili wa Mbilinyi, Tundu Lissu, aliliambia gazeti hili kuwa waliitwa kwa mara ya pili ili kwenda kusaini dhamana ya polisi kwa sababu awali hawakufanya hivyo. Mapema akizungumza na waandishi wa habari, Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, alisema waliitika wito wa jeshi hilo na walipofika waliambiwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea. “RCO (Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa), ametuambia kuwa atawasiliana na sisi baada ya kama wiki mbili hivi ili kujua wamefikia uamuzi gani,” alisema: “Mimi nitashangaa sana kama polisi watampeleka mahakamani, katiba ya sasa ibara 100 (2), inasema mbunge hatashtakiwa wala kufunguliwa shauri lolote la madai kwa jambo lolote alilosema ama kufanya akiwa ndani ya Bunge, alisema.
       Alisema hilo neno Bunge limetafsiriwa ndani ya sheria ya Kinga na Mamlaka ya Bunge, ndani ya Bunge, nje ya ukumbi na maeneo yote yaliyopo ndani ya uzio wa Bunge. “Mbunge akifanya lolote ama kusema lolote huwezi kushtakiwa, nitashangaa sana hao wanaopiga kelele na kundi lao na Serikali yao wataamua hili jambo liende mahakamani,” alisema. Kwa upande wake, Mbilinyi, alisema tukio hilo halijamletea usumbufu wowote. Mbunge huyo alihojiwa Ijumaa, kutokana na vurugu zilizotokea bungeni Alhamisi iliyopita wakati wa Mjadala wa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba. Vurugu hizo zilitokea wakati wabunge wa Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF, walipokuwa wakimzuia Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, asitolewe kwa nguvu na askari wa Bunge ndani ya ukumbi.
Source: Sauwa S., & Masasi M. ( Sept. 2013).Mbunge Mbilinyi asahau kutia saini dhamana. Retrieved from Mwananchi

No comments: