Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Thursday, September 12, 2013

CHADEMA: Wananchi wataamua


    BAADA ya kupitishwa na Bunge kwa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya 2013 bila ya wabunge wa upinzani kuwepo bungeni, kikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), chama hicho kimesema kitalifikisha suala hilo mikononi mwa wananchi ili waamue. Aidha chama hicho kimebainisha kuwa suala la kwenda mahakamani kupinga muswada huo, kwa sasa kinaachia makundi ya kiraia kufanya hivyo ambapo leo sekretarieti ya chama hicho inatarajia kukutana kwa ajili ya kujadili zaidi juu ya kilichojiri bungeni. Pamoja na hayo, Chadema imesisitiza kuwa kamwe haitoacha kugoma na kususa vikao vya Bunge, pale itakapoona inaelekea kushindwa kwa kuwa njia hiyo imeonesha mafanikio tangu waanze kuitumia hadi leo. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika alisema chama hicho kwa sasa kimeamua kurudi kwenye mahakama ya wananchi kuhusu kilichojiri bungeni na suala la kwenda mahakamani kupinga muswada wanaachia makundi ya kiraia kufanya hivyo.

       “Ndio maana kesho (leo) Sekretarieti ya chama chetu itakutana kujadili suala hili, lakini baada ya hapa tutakutana na vyama vya upinzani vyote vyenye wabunge na visivyo na wabunge ili kuja na sauti moja kuhusu muswada huu uliopitishwa kinyemela,” alisema Mnyika. Aidha, Mnyika alielezea kilichojiri bungeni kuwa chama hicho kilinyimwa haki na Naibu Spika, Job Ndugai ya kuwasilisha kupitia Kiongozi wa Upinzani hoja zao, na matokeo yake kiongozi huyo wa Bunge, aliita Polisi kinyume cha Katiba, Sheria na Kanuni za Bunge. Alisema kilichojiri katika Bunge hilo, ni mbinu za Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kuhakikisha muswada huo unapita kwa gharama yoyote baada ya chama hicho kuona kimeshindwa kupenyeza hoja yake ya Serikali mbili kwenye mabaraza ya Katiba na hivyo kubakia na njia moja ya Bunge la Katiba. “Kama chama, baada ya Sekretarieti tutaeleza namna ambavyo tutaitumia nguvu ya wananchi kuhusu suala hili, lakini msimamo wetu ni kwamba hatutaacha kususa bungeni, kwani tulishafanikiwa tangu mwanzo kwa njia hii,” alisisitiza.

Source: Mlacha S. ( Sept. 2013).CHADEMA: Wananchi wataamua. retrieved from HabariLeo

No comments: