WADAI MUSWADA ULIOPITISHWA NA CCM NI MAAFA
VYAMA vitatu vya CHADEMA, CUF na NCCR Mageuzi vimeamua kuunganisha nguvu ili kunusuru mchakato wa Katiba unaoendelea kwa kile walichodai kuwa CCM inataka kuhodhi mchakato huo.Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, viongozi wakuu wa vyama hivyo, Freeman Mbowe (CHADEMA), Prof. Ibrahim Lipumba (CUF) na James Mbatia (NCCR-Mageuzi, walisema wametafakari na kujadili mustakabali wa taifa. Walisema kuwa tangu kupitishwa kinyemela mwa muswada wa marekebisho ya mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013, kumekuwa na taarifa za upotoshwaji kwa umma juu ya kile kilichotokea bungneni. Kwa mujibu wa viongozi hao, mchakato wa Katiba mpya unahitaji uvumilivu, stahamala, hekima, kuheshimiana na kamwe usitawaliwe kwa mizengwe na nia mbaya, ubabe, mabavu, kejeli na dharau hasa kutoka kwa watawala na wadau wengine.
“Kufanya vile kutasababisha kulitumbukiza taifa letu katika mipasuko, migogoro na machafuko,” walisema. Walisema kuwa nguvu ya pamoja ya wananchi, wadau wote na Watanzania wenye kuitakia mema nchi yetu zinapaswa kuunganishwa kuunusuru mchakato wa Katiba mpya uliotekwa na kuhodhiwa na CCM na serikali yake. Katika kuhakikisha wananchi wanafahamu kile kilichotokea bungeni kwa wapinznai kususia muswada huo uliochakachuliwa kwa kuchomekwa vifungu visivyo na manufaa, viongozi hao wameanza utaratibu wa kukutana na makundi mbalimbali ya wadau na wananchi. Kwa jana viongozi hao walikutana na wahariri wa habari na ndani ya wiki hii watakutana na makundi mengine ya viongozi wa dini, asasi za kijamii, wanazuoni na wananchi wengine.
Waliuchambua muswada uliopitishwa kinyemela hivi karibuni na wabunge wa CCM wakisema ulikuwa na kasoro nyingi za wazi na kwamba Serikali ya Muungano iliidanganya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. “Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikushirikishwa katika kuandaa muswada uliopelekwa bungeni wa sheria ya mabadiliko ya Katiba,” walisema. Pia waligusia hatua ya wabunge wa CCM kuridhia muswada huo unaoainisha kuwa baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba kukabidhi rasimu kwa Bunge Maalumu la Katiba inafutwa. Viongozi hao walipendekeza kuwa tume hiyo haipaswi kufutwa hadi hapo mchakato utakapofikia hatua ya kura ya maoni ili kuipa nafasi ya kulisaidia Bunge Maalum la Katiba kufafanua baadhi ya vifungu vitakavyokuwa na utata kwenye rasimu.
“Huu si mpambano baina ya CCM na wapinzani na katika hili hakuna mshindi wala mshindwa bali unatafutwa muafaka wa pamoja katika taifa lililoparaganyika,” walisema katika tamko lao. Wenyeviti hao waliongeza kuwa Mei mwaka huu, Serikali ya Muungano ilipeleka muswada wa sheria ya mabadiliko ya Katiba uliokuwa na vifungu sita. Kwamba serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliujadili na kupeleka mapendekezo yao ya rasimu ya muswada huo. Lakini muswada uliopelekwa bungeni hivi karibuni uliongezwa vifungu vingi ambavyo havikuwepo katika rasimu iliyopelekewa Zanzibar. Walitolea mfano kifungu cha 26 cha sheria mama kurekebishwa kuruhusu iwapo theluthi mbili za kila upande hazikupatikana, hivyo kufanya utaratibu wa kupitisha hoja kuwa wa wingi wa kawaida (simple majority).
Vilevile walimuonya Rais Jakaya Kikwete kutousaini muswada huo kuwa sheria, kwani marekebisho yaliyofanyika na utaratibu uliotumika kuyapitisha ni kinyume na dhamira na dhima ya majadiliano aliyofanya na vyama hivyo na wadau mwaka 2011 na 2012. Kutokana na hali hivyo, vyama hivyo vimeazimia kufanya mkutano mkubwa jijini Dar es Salaam Septemba 21 mwaka huu, katika viwanja vya Jangwani ili kupeleka ujumbe kwa wananchi kunusuru mchakato usiendelee kuhodhiwa na kutekwa na CCM. Waliziomba asasi za kiraia, taasisi za dini, vyama vingine vya siasa, taasisi zingine za elimu ya juu, vyama vya wafanyakazi, jumuiya za wakulima, wafugaji, nyinginezo na wananchi kwa ujumla kuweka pembeni tofauti zao na kuunga mkono hoja yao.
Source: Isango J (Sept. 2013). Mbowe, Lipumba, Mbatia waungana. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment