Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemjia juu Balozi wa China nchini, Dk. Lu Youqing, kwa kujiingiza kwenye siasa za ndani ya nchi na kuacha majukumu yake ya kibalozi. Balozi huyo alionekana kwenye mikutano ya hadhara ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Kishapu na Shinyanga mjini, akiwa amevalia sare na kofia ya CCM na kupanda jukwaani kuzungumza na wananchi. Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Chadema, Ezekia Wenje, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, alisema Balozi huyo amevunja mkataba unaowaongoza mabalozi ujulikanao kama ‘Vienna Conversion on Diplomatic Relations’. Wenje ambaye pia ni Mbunge wa Nyamagana, mkoani Mwanza, alisema mkataba huo unazungumzia mahusiano ya kibalozi baina ya nchi na nchi na kazi za balozi awapo kwenye nchi fulani kwamba siyo kujihusisha na mambo ya ndani ya nchi husika zaidi ya kujenga mahusiano baina ya nchi hizo na kusaidia wananchi wa nchi yake na wananchi husika wanaotaka kwenda kwenye nchi yake.
“Ibara ya 41 (1) inakataza mabalozi kujiingiza katika masuala ya ndani ya nchi ikiwamo siasa, ibara ya tatu ikionyesha kazi za balozi na ibara ya 31 (1) inazungumzia kinga ya balozi, kama atajiingiza kwenye kazi ambazo hazimuhusu kinga itaondolewa,” alifafanua Wenje. Alisema kazi ya balozi ni kutengeneza uhusiano baina ya nchi yake na Tanzania na siyo kuwa mwenezi wa chama chochote cha siasa na kwamba alichofanya balozi huyo ni kugeuka kuwa Katibu Mwenezi wa CCM huku akisakata muziki wa chama hicho hadharani. Alisema kimsingi, balozi huyo hakutakiwa kushiriki kwenye mkutano huo na mikutano anayopaswa kushiriki ni ya kiserikali, lakini alisimama kuhutubia wananchi akiwa amevaa sare ya CCM. “Tusingependa uhusiano wa kihistoria kati ya China na Tanzania ambao umedumu kwa muda mrefu tangu uhuru uingizwe matatani au shakani kwa sababu ya mapenzi binafsi ya balozi kwa CCM,” alisisitiza Wenje.
MAAMUZI YA CHADEMA
Alisema chama hicho kimedhamiria kuandika barua kwa Umoja wa Mataifa (UN) ambao ndiyo wamiliki wa mkataba huo ili kupata msimamo wao. Pia, kitaiandikia serikali ya Tanzania ili kujua msimamo wake wa kupeleka mabalozi kwenye mikutano ya CCM na balozi kugeuka kuwa katibu mwenezi. Alisema pia wataiandikia serikali ya China ili kupata msimamo wao na kujua kama ndiyo kazi alizotumwa kufanya balozi huyo. “CCM inatushangaza sana na kuona ni chama cha mzaha kila wakati… wametubambikia kesi za ugaidi, wanatumia watumishi wa serikali kwenye siasa zao…watambue Watanzania hawataki mzaha au propaganda za kupeleka mabalozi kwenye mikutano bali uwajibikaji wa serikali,” alisisitiza Wenje.
Alisema Balozi huyo anatishia uhusiano wa Tanzania na China kwa siku za usoni iwapo Chadema au chama kingine kitaingia madarakani na kwamba wao wanapenda uhusiano baina ya nchi hizo kuimarika na siyo kuharibiwa kwa maslahi binafsi. Alisema hata kama balozi huyo angekuwa mwanachama au mkereketwa wa chama hakupaswa kufanya hivyo kwa nafasi yake. Alisema lengo la kuandika barua hizo ni kutaka hatua zichukuliwe na kuhakikisha wanadiplomasia wa nchi zote ambazo Tanzania ina uhusiano nazo katika ngazi ya serikali, wanaheshimu misingi na taratibu zinazosimamia uhusiano ya kimataifa katika nafasi ya uwakilishi na uhusiano ni baina ya nchi na nchi. “Tunaamini taratibu hizo zimeweka ‘majukwaa’ ambayo wanadiplomasia wanaweza kuendesha shughuli zao za uwakilishi na kushiriki shughuli mbalimbali za kiserikali zinazohusu majukumu na wajibu katika nchi husika,” alisema.
MEMBE: BALOZI AMEKOSEA
Serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, imesema kuwa kitendo kilichofanywa na Balozi huyo siyo sahihi na kinakiuka mkataba wa Vienna. “Wizara inapenda kutamka kwamba kitendo cha Balozi yoyote kuhudhuria mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na kuvaa sare zenye nembo ya vyama vya siasa siyo sahihi na kinakiuka Kifungu cha 41(1) cha Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961, unaoongoza uhusiano wa kidiplomasia,” alisema Membe katika taarifa yake jana jioni. Taarifa hiyo ilisema kuwa mkataba huo unazuia wawakilishi wa nchi za nje kujihusisha na ushabiki wa kisiasa wanapofanya kazi zao kwenye nchi za uwakilishi.
“Katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2012, Wizara ilikumbana na vitendo vinavyofanana na kitendo hiki na ikachukua hatua stahiki, kadhalika kwa tukio hili Wizara itachukua hatua za kidiplomasia zinazostahili ili kuzuia jambo hili lisitokee tena,” alisisitiza. Taarifa hiyo ilisema kuwa Balozi huyo alikwenda wilayani humo kuhudhuria uzinduzi wa mradi wa viwanda vya kuchambulia pamba vinavyojengwa na mwekezaji wa Kichina anayeitwa Tahong, na viwanda hivyo vitakuwa na uwezo wa kuchambua tani 120,000 za pamba kwa mwaka, vitakapokamilika mwakani. Alisema Wizara imeona picha na habari kwenye vyombo vya habari zikieleza na kumuonyesha Balozi huyo akiwa kwenye mkutano wa CCM.
ALICHOSEMA BALOZI
Balozi huyo amenukuliwa na vyambo vya habari wakati akihutubia mkutano wa hadhara akiwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, na kujitahidi kuwasalimia wananchi hao kwa lugha ya kabila la Wasukuma kwa kusema mwadila. Alisema pamoja na Tanzania kuwa na mfumo wa vyama vingi, anaamini kuwa CCM bado iko imara na inaweza kuendelea kuongoza kwa muda mrefu. “Kwa hili inadhihirisha kuwa hakuna chama kama CCM kutokana na uimara wake na hili wanalofanya sasa la kuja kuimarisha chama nasi kule China kupitia chama chetu tawala cha CPC (Chama Cha Kikomunisti cha China), tunafanya kama hivi pia. Mwadila, Shinyanga, CCM Oyeeeeee asanteni sana,” alikaririwa akisema. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alipotafutwa jana kuzungumzia suala hilo, hakupatikana kutokana na simu zake za kiganjani kufungwa. Hata hivyo, Nape juzi alisema atatoa ufafanuzi wa masuala yote kuhusu chama chake atakaporejea kutoka katika ziara hiyo anayofuatana na Kinana.
Source: Kitomary S. (Sept 2013).Balozi wa China matatani. Retrieved from Ippmedia/ Nipashe
No comments:
Post a Comment