Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Sunday, September 15, 2013

MAKALA: Tuwaandae kwanza CCM kisaikolojia


Edson Kamukara

     MCHAKATO wa Katiba Mpya unaoendelea sasa umewachanganya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Wao walizoea katiba za kuwekwa viraka kila wakati yalipohitajika mabadiliko. Huu ndio msimamo na maono ya Wana-CCM wengi. Kwao Katiba mpya haikuwa kipaumbele, hawakuona hata maana yoyote wakaamua kutoiweka kwenye ilani yao ya uchaguzi. Kila mara wapinzani walipozungumzia suala la Katiba mpya viongozi wote wa serikali na CCM walilibeza suala hilo wakidai wananchi hawahitaji Katiba mpya.

      Hofu yao ni kupoteza vyeo, kupoteza fursa za kujineemesha binafsi na familia zao. Ndiyo maana hata baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010 wapinzani walipoanza vuguvugu la kudai Katiba Mpya, tulisikia majibu mengi na ya hovyo. Aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria wakati huo, Celina Kombani na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, walisema kuwa Watanzania hawahitaji Katiba mpya bali hii iliyopo inatosha ikifanyiwa marekebisho madogo. Hawa bado ni viongozi ndani ya serikali, wanaketi na rais kwenye baraza la mawaziri kujadili mchakato wa Katiba mpya pamoja na kuandaa miswada ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

        Kilichotokea bungeni hivi karibuni kwa Naibu Spika, Job Ndugai, kuamua kwa makusudi kumdhalilisha Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe na wabunge wa upinzani ni mwendelezo uleule wa hofu ya CCM kwenye mchakato wa Katiba. Tuna kila sababu ya kuwaandaa CCM kisaikolojia watambue sasa kuwa Katiba mpya haikwepeki. Kwamba yale matashi yao waliyoyazoea kuyapenyeza kwenye viraka vya Katiba zilizopita safari hii hayana nafasi kwenye Katiba ya wananchi. Tatizo walilonalo CCM ni kuutazama mchakato huu kama suala binafsi la matashi ya rais. Wao wanadhani kuwa rais anayetajwa kwenye Katiba mpya ijayo ni Kikwete.

        Wanadhani wabunge na mawaziri wanaotajwa kwenye Katiba ni wao. Kwa hiyo wanaposikia rais kupunguziwa madaraka moja kwa moja akili zao zinagonga kwa Kikwete. Wanahisi chama chao na Rais Kikwete watakuwa madarakani milele, hivyo kumwondolea madaraka ya uteuzi, wao na familia zao hawatapata nafasi za upendeleo walizokuwa wamezizoea. Kila yanapotolewa maoni ya wabunge kutokuwa mawaziri, utaona mawaziri wa sasa wanavuta midomo kana kwamba Katiba itaanza kutumika kesho na wao kutupwa nje.

       Kwa kifupi hofu hiyo ya vyeo ndiyo inawanyima raha CCM katika mchakato wa Katiba, kwa hiyo wakawa na akili za karibu kwamba wakitengeneza sheria ya kuwawezesha kuwa na wajumbe wengi kwenye mabaraza ya Katiba na Bunge Maalumu la Katiba watafanikisha. Nilifurahishwa na kauli ya Mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete kwenye kikao cha NEC cha hivi karibuni ya kuwataka CCM kujiandaa kisaikolojia endapo pendekezo lao la muungano wa serikali mbili litakataliwa na wananchi. Ni wazi kwa kauli ile alishaona mbali kwamba wananchi wamefunguka kiakili, hawakubali tena mambo ya kuburuzwa. Huyu anajua kuwa suala na mchakato wa Katiba walilibeba kutoka kwa wapinzani baada ya kuona hili ya kisiasa limegeuka.

       Sasa Wana CCM aina ya Ndugai, mwanasheria mkuu, mawaziri na wabunge ambao mpaka sasa wanategemea mabavu kuendesha mchakato wa Katiba mpya wanapaswa kujitayarisha kisaikolojia. Watambue kuwa baada ya yote Katiba hiyo lazima irudi kwa wananchi kupigiwa kura ya maoni, kwa hiyo mambo yote yatakayokuwa yamechomekwa kwa mashinikizo lazima Katiba itakataliwa, hivyo mchakayo huo kuanza upya. Lazima tukubali kuwa CCM hawawezi kuhadaa ulimwengu leo kuwa wana dhamira njema ya kutengeneza Katiba mpya wakati ajenda hiyo walikuwa wakiipiga vita ya ajabu.

       Pamoja na dhamira nzuri ya Rais Kikwete kukubali kuibeba hoja hiyo ya wapinzani lakini alipaswa kwanza kuandaa mjadala wa kitaifa ili kubadilishana mawazo na wenye hoja kabla ya kutangaza mchakato. Lakini uharaka huu wa kuridhia na kisha kuwapa kazi viongozi wale wale waliokuwa wakiipinga Katiba mpya kusimamia mchakato ndiyo maana tunaona mambo ya ajabu kama hayo yaliyotokea bungeni. Mwanasheria Mkuu, Jaji Frederick Werema, alishakiri kwa kinywa chake kuwa haoni sababu ya kuwa na Katiba mpya, halafu huyo ndiye leo msimaizi wa serikali katika mchakato huo.

       Miswada ya kuchekesha inaletwa bungeni bila upande wa pili wa muungano kushirikishwa, halafu Jaji Werema anasimama na kutetea kasoro hiyo. Hapa nia njema wanayoisema CCM iko wapi kama si kuinajisi Katiba ya wananchi. Bunge ni chombo cha wananchi, kazi ya wabunge ni kuihoji na kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi. Sasa kama una Bunge linaloongozwa na Ndugai ambaye kila anapokalia kiti anaanzisha vurugu bungeni, unatarajia serikali inaweza kusimamiwa na kuhojiwa? Wanaoihoji serikali leo, viongozi wa Bunge wanawaona kama waasi, wanatumia mabavu ya dola kuwatoa nje ya ukumbi, ikishindikana wanazima na vyombo vyao vya habari ili wananchi wasione udhaifu wa kiti chao cha uamuzi.

      Akili ya CCM iko kwenye kumaliza Katiba ifikapo Aprili 26, mwaka 2014, potelea mbali ina mambo ya msingi ya wananchi au la! Cha msingi ni kuihadaa dunia kuwa Tanzania imeandika Katiba mpya. Tunapaswa kuwaandaa kisaikolojia kwanza na kuweka mwafaka wa pamoja ni katiba gani tunakusudia kuiandaa badala ya hizi sarakasi za CCM za kukimbilia kutangaza tarehe ya Katiba ya Muungano kuzinduliwa bila kuwa na maandalizi mazuri. Tafakari!

No comments: