KADA wa Chama cha Mapinduzi mkoani Morogoro, David Mgesi, amedai kushangazwa na kauli ya Rais Jakaya Kikwete ya kuwalaumu viongozi kwamba hawaelezi mafanikio ya serikali kwa wananchi. Mgesi mwenye kadi ya uanachama Aa 145213 iliyotolewa mwaka 2005, alisema kuwa Rais Kikwete alitoa kauli hiyo karibuni akiwa ziarani mkoani Mwanza. Alisema kuwa kinachosababisha mafanikio ya serikali ya CCM kushindwa kuonekana ni mfumo uliopo wa viongozi wa chama na serikali kuwa wafanyabiashara badala ya kuwa watumishi wa wananchi. “Viongozi wengi ni wafanyabiashara tena za ujanja ujanja sasa watu kama hao ni lazima watatumia muda mwingi kuhakikisha biashara zao zinakwenda vizuri . Unadhani watakuwa na muda wa kuwatumikia wananchi?” alihoji.
Mgesi aliwataka viongozi wa CCM na serikali kujikita katika kueneza sera za chama hicho na kutekeleza ilani iliyowapa nafasi ya kuingia madarakani badala ya kutumia nguvu kubwa kuwasumbua wapinzani. Alisema kila kiongozi anayepata fursa ya kuzungumza jukwaani au kwenye vyombo vya habari, anashindwa kueleza mafanikio yaliyopatikana badala yake anajikita kuwatukana Dk. Willibrod Slaa na Freeman Mbowe wa CHADEMA. Mgesi ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Morogoro kabla ya kutimkia CCM 2005, alitoa kauli hiyo juzi jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Tanzania Daima.
“Leo tunafikiri kushindwa kwetu kushughulikia matatizo ya wananchi kunasababishwa na viongozi wa upinzani hasa CHADEMA na tumejenga fikra kuwa njia nzuri ya kurudisha imani ya chama kwa wananchi ni kuwasakama viongozi wa chama hicho hili si kweli hata kidogo,” alisema. Alisema kuwa kutokana na udhaifu wa kushindwa kuwachukulia hatua viongozi wanaozembea au kuwakemea, kila tuhuma nzito leo zinazoibuliwa zinawahusisha viongozi wa CCM na serikali yake. Aliongeza kuwa CCM na serikali yake vinasimamia dhulma ya wazi dhidi ya wananchi, hususan kwa wafugaji pasipo kukumbuka matatizo hayo yalitokana na serikali kuwaondoa katika maeneo yao ya asili.
Kwa mujibu wa kada huyu, dhulma nyingine ni viongozi kuuziana nyumba za serikali kwa bei nafuu pasipo kujali maslahi ya wananchi katika upatikanaji wa nyumba zingine. Kuhusu wataka urais, Mgesi lisema mpaka sasa kwa watu wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ndani ya CCM hakuna mwenye sifa ya kukabiliana na nguvu ya vyama vya upinzani. Alisema kwa mazingira ya sasa ya uelewa wa wananchi juu ya masuala mbalimbali CCM kurejea madarakani katika uchaguzi mkuu wa 2015 ni ndogo zaidi. Aliongeza kuwa matumaini ya CCM kushinda yanazidi kutoweka kila siku huku wabunge wake nao wakichangia hali hiyo kutokana na udhaifu wao wanaouonyesha bungeni. “Tulikofika ndani ya CCM ni kubaya, kama wabunge wetu bungeni wakiamua wanaweza kuokoa jahazi na hili ni kwa kupiga moyo konde na kuhakikisha viongozi wa Bunge, Spika na naibu wake wanawekwa pembeni,” alisema.
Source: Khamis A. (Sept. 2013). Kada CCM amvaa JK. Retrieved from Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment