*Asema mchakato wa sheria kuvibana vyama unaanza
HATIMAYE Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis
Mutungi ameanza kuonyesha makali, baada ya kukipa onyo kali Chama Cha Mapinduzi
(CCM) na kukitaka kuacha mara moja kutumia viongozi wa kidiplomasia kwenye
shughuli za kisiasa.
Hatua ya Jaji Mutungi, imekuja siku chache baada ya CCM
kumtumia Balozi wa China, Dk. Lu Youping katika shughuli za kisiasa mkoani
Shinyanga wiki iliyopita.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Dar
es Salaam jana, ilisema suala la ushiriki wa raia wa kigeni ikijumuisha
wanadiplomasia katika shughuli za kisiasa nchini, halikubaliki.
Alisema ofisi
yake, inaunga mkono kwa dhati hatua iliyochukuliwa na Serikali kupitia Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kukemea jambo hilo.
“Tamko la
Serikali limezingatia sheria na wajibu wa wanadiplomasia, wakati wa uwepo wao
hapa nchini, mimi nikiwa mlezi wa vyama vya siasa, ninakemea kitendo cha CCM
kumshirikisha Balozi wa China katika shughuli za kisiasa,” alisema Jaji
Mutungi.
Alisema katika tukio hilo, CCM kuruhusu raia wa kigeni kutumia jukwaa
lake ni dhahiri limezua hali ya taharuki kwa wananchi, japo sheria ya vyama vya
siasa kwa upande wake iko kimya katika suala hilo.
“Naviasa vyama vya siasa
kwa ujumla wake, kuzingatia na kufuata sheria na taratibu stahiki katika
utekelezaji wa shughuli zao za kisiasa.
“Napenda kuujulisha umma kwamba, ofisi
ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa wakati huu ipo kwenye mchakato wa marekebisho
ya sheria husika ya vyama vya siasa, ambayo imebainika kuwa na upungufu….lengo
ni kukabiliana na changamoto zilizopo likiwemo suala hili,” alisema Msajili,
Jaji Mutungi katika taarifa yake.
CHADEMA imesema inalaani kitendo hicho na itachukua
hatua kwenda Umoja wa Mataifa na pia kupata maelezo toka Serikali ya China kama
imemtuma balozi huyo kujihusisha na mambo ya siasa za ndani za vyama au
kuiwakilisha nchi.
Akijibu tuhuma hizo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,
Nape Nnauye alisema alichofanya balozi huyo ni kitendo cha kuungwa mkono, maana
alikuwepo kwa nia ya kuangalia maeneo ya uwekezaji wa zao la Pamba katika Mkoa
wa Shinyanga.
Alisema uwekezaji kutoka China, utasaidia kuondoa tatizo sugu la
ajira, kupanda kwa bei ya zao la pamba ambacho kimekuwa kilio kikubwa cha
wakulima pamoja na ujengwaji wa viwanda vya nguo na kuchuja mafuta.
Hivyo ni
vema kumpongeza balozi huyo na kuunga juhudi za CCM za kuwatafuta wawekezaji wa
nje, badala ya kusingizia uvunjaji wa Mkataba wa Vienna ili kupata umaarufu wa
kisiasa.
Source: Mzee K. (Sept. 2013). Jaji Mutungi aiumbua CCM. Retrieved from Mtanzania
No comments:
Post a Comment