Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Monday, September 9, 2013

Chadema yafichua `usanii` muswada wa Katiba


Kamanda Mnyika
     Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2013 umezidi kuibua mapya, baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kudai kwamba, kikao cha Bunge kilichofanya maamuzi ya kuupitisha hakikuwa halali. 
Kimedai akidi ya wabunge inayohitajika na kanuni za Bunge ya kufanya maamuzi haikutimia wakati wa kupitisha muswada huo. Muswada huo uliozua tafrani kubwa bungeni, iliyohusisha baadhi ya wabunge, akiwamo Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kuondolewa na askari bungeni na wengine kurushiana ngumi na maofisa usalama, ulipitishwa ‘kiulaini’ na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ijumaa wiki iliyopita, huku wenzao wa upinzani wakisusia. Madai hayo yalitolewa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, katika mahojiano maalum na NIPASHE jijini Dar es Saalam jana.

       Mnyika alisema kanuni ya Bunge ya 77 (1) inataka kikao cha Bunge wakati wa kufanya maamuzi kiwe na wabunge wasiokuwa chini ya 175. Lakini alidai wabunge waliokuwapo katika kikao kilichofanya maamuzi ya kupitisha muswada huo walikuwa 109. Kanuni hiyo inasema: “Akidi kwa kila kikao cha Bunge wakati wa kufanya maamuzi itakuwa ni nusu ya Wabunge wote, kama ilivyofafanuliwa katika Ibara ya 94 ya Katiba,isipokuwa kwamba, idadi hiyo haitahusu hoja kuhusu uamuzi wa kubadilisha masharti yoyote ya Katiba kwa mujibu wa Ibara ya 98 ya Katiba.” Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lina wabunge 352, ambao nusu yake ni 176. Alipotakiwa kueleza alivyofahamu idadi ya wabunge waliokuwapo katika kikao kilichopitisha muswada huo, Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema atafanya hivyo iwapo atapelekwa mahakamani. 

     Alisema Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliijua idadi hiyo ya wabunge ndiyo maana alitumia fursa hiyo kujitetea japo kuwa utetezi wake haukuwa na msingi. Mnyika alisema katika utetezi wake, Ndugai alisema akidi ilitimizwa na wabunge wa upinzani waliotoka bungeni kwa kuwa waliingia bungeni na kusaini mahudhurio, hivyo wanahesabika pia katika orodha ya wabunge waliokuwapo katika kikao kilichofanya maamuzi ya kupitisha muswada huo. Hata hivyo, Mnyika alisema Sekretarieti ya Kamati Kuu (CC) ya Chadema chini ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, inakutana kuanzia leo kupitia na kujadili kwa kina mambo yote yaliyojiri bungeni, kutoa maamuzi na kutengeneza msingi wa mwelekeo wa baadaye.

       Alisema mbali na hilo, Chadema pia itakutana na wadau wote wa katiba nchini, vikiwamo vyama vingine vya upinzani vyenye wabunge na visivyokuwa na wabunge na makundi mbalimbali ya kijamii ili kujenga sauti ya pamoja. Alisema yote yaliyojiri bungeni, ikiwa ni pamoja na wabunge wa upinzani, akiwamo Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuzuiwa kuzungumza, kutolewa nje na kupitishwa muswada huo kwa mabavu, ni njama zilizokuwa zimepangwa. Mnyika alidai njama hizo zilipangwa na CCM kwa nia mbaya ya kuliteka Bunge Maalum la Katiba litakaloanza Novemba, mwaka huu, ili walitumie kuchakachua Rasimu ya Katiba. Alidai njama hizo zimepangwa na CCM baada ya jaribio lao la kuichakachua rasimu hiyo kupitia mabaraza ya katiba kushindwa na operesheni iliyofanywa na Chadema nchini kote.

         Mnyika alidai njama hizo zilijadiliwa na kupitishwa pia katika kikao cha wabunge wa CCM kilichofanyika mjini Dodoma, wiki iliyopita. Alidai kitendo cha yeye (Mnyika) na wabunge wengine, hasa wa Chadema kuzuiwa kuzungumza bungeni kilifanywa makusudi. Mnyika alidai CCM walijua kuwa kama wabunge wa Chadema wangeruhusiwa kuzungumza bungeni, wangeweka hadharani mambo yote, ambayo walijadiliana na timu ya serikali kuhusu masuala yanayohusu katiba katika vikao viwili baina ya timu zao za majadiliano. Alidai katika vikao vyote vya timu hizo, Chadema hawakukubaliana na mambo mengi ya msingi yaliyomo kwenye muswada uliopitishwa bungeni, ambao alidai ni mbaya kuliko kile kilichoandaliwa awali.Mnyika alisema baada ya yote yaliyojiri bungeni, walipokea mapendekezo tofauti kutoka kwa wadau juu ya hatua za kuchukua.

     Alisema baadhi ya wadau wamependekeza kwenda mahakamani kuomba tafsiri ya sheria ili kuzuia Rais Jakaya Kikwete asiusaini muswada huo ili kuanza kutumika kuwa sheria rasmi. Mnyika alisema wadau wengine wamependekeza kutumia njia za kibunge kumshtaki Naibu Spika kwenye Kamati ya Bunge ya Kanuni kwa kukiuka kanuni za Bunge. “Hata hivyo, kipaumbele chetu (Chadema) ni kurudi kwa wananchi. Tutajikita zaidi katika kutafakari namna tutakavyounganisha nguvu ya umma,” alisema Mnyika na kuwashauri wadau wengine kuendelea na mchakato wa kwenda mahakamani. Wakati huo huo, Chama cha Wananchi (CUF), kimelaani vikali kitendo cha Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, kuwanyanyasa na kuwadhalilisha wabunge wa upinzani akiwemo Kiongozi wa Kambi Rasmi ya upinzani Bungeni  Freeman Mbowe. 

       Vurugu hizo zilizuka bungeni wakati wa mjadala wa kupitisha Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 wiki iliyopita, baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani  kusimama na  kuomba kuongea. Hayo yalisemwa jana jijini  Dar es Salaam na Mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Ibrahim  Lipumba.  Alisema kitendo cha Naibu Spika kumkataza   Mbowe asiongee na kuamuru askari wamtoe bungeni kwa nguvu, hakikubaliki na kusema Serikali na kiti cha Spika wajitazame upya kwenye mchakato wa Katiba. Profesa Lipumba alisema, ni kitendo cha aibu na hakikupaswa kufanywa na Naibu Spika wa Bunge. “Sisi CUF tunajiuliza, angesimama  Mizengo Pinda kuongea Naibu Spika angemnyima nafasi? na angethubutu kuamrisha askari wamtoe nje? Kwa nini haya yanatendwa na kiti cha Spika kwa vyama vya pinzani na hayatokei viongozi wa serikali,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza kuwa:

      “Serikali ina mamlaka makubwa katika Bunge kuliko Bunge lenyewe, hadi kiti cha Spika kiendeshe masuala kwa taratibu za kupendelea serikali kwa kadri ambavyo Spika ataona,” alisema. Alisema, muswada husika uliojadiliwa kwa dakika 90 ulikuwa na utata mkubwa, serikali imeubadili kwa nguvu na kuondoa maoni muhimu ya wadau, pia upande wa Zanzibar haukushirikishwa ipasavyo na wajumbe wa Kamati ya Sheria na Katiba ya Bunge.Alisema, akiwamo  Tundu Lisu, wamesisitiza kuwa hawakupewa fursa ya kuchukua maoni kutoka kwa taasisi na watu muhimu waliopo Zanzibar. Aliongeza kuwa, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF upande wa Zanzibar  Hamad Masoud ambaye pia ni mjumbe wa baraza la Wawakilishi anathibitisha kuwa Zanzibar haikushirikishwa. 

Imeandikwa na Muhibu Said, Mary Geodfrey na Enles Mbegalo


Source: Said M., Saidi M., Geodfrey M., & Mbegalo E. (Sept. 2013).Chadema yafichua `usanii` muswada wa Katiba. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: