
WAKATI mjadala kuhusu muundo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uwe wa serikali tatu kama inavyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ama wa serikali mbili kama inavyong’ang’aniwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) ukishika kasi, Raia Mwema limebaini serikali ya shirikisho ndani ya muundo wa serikali tatu si gharama kwa wananchi na takwimu kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zinapingana na hoja za chama hicho tawala. Kwa muda mrefu sasa tangu rasimu ya Katiba mpya izinduliwe na Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal, Juni 3 jijini Dar es Salaam, CCM wamekuwa wakipinga muundo wa serikali tatu kwa madai kuwa ni gharama na utasababisha urasimu, lakini uchunguzi wetu wa hivi karibuni umebaini hoja ya gharama kwa maana ya serikali ya shirikisho (ya Muungano) si ya msingi, kwa sababu mambo ya Muungano yamepunguzwa kutoka 22 hadi saba na ni mambo hayo ambayo ndiyo gharama yenyewe ya uendeshaji.
Kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika serikalini na katika TRA, kwa
sasa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye kusimamia mambo 22
inaendeshwa kwa gharama ya shilingi trilioni 1.2 kwa mwaka, na kwa sababu Tume
ya Warioba kupitia Rasimu ya Katiba imepunguza masuala ya Muungano kutoka 22
hadi saba, maana yake gharama hizo zitashuka kutoka shilingi trilioni 1.2
zinazotafunwa na Serikali ya Muungano kwa sasa. Hizi ni takwimu mpya ambazo hazikuwahi kutolewa na kiongozi
yeyote kutoka Chama tawala wala vyama vya upinzani, licha ya pande hizo kuwamo
katika mvutano wa hoja ya gharama lakini bila kuzingatia matakwa ya takwimu za
uendeshaji wa sasa wa serikali.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, iwapo muundo wa Serikali tatu
utaridhiwa, sehemu kubwa ya mapato yote ya sasa yanayokusanywa na Serikali ya
Muungano ambayo yanakadiriwa kufikia Sh trilioni 5.5, yatatumika kuendesha
Serikali za washirika, yaani ile ya Tanganyika na Zanzibar. “Sasa hivi Serikali ya Muungano inakusanya takribani Sh.
trilioni 5.5, kati ya hizo zinazotokana na kodi ya mapato Sh. trilioni 4,
ushuru wa forodha (Sh. bilioni 500) na ushuru wa bidhaa Sh. trilioni 1.1 ambazo
hutumika kugharamia shughuli za Muungano na zile za Tanzania Bara,” kinaeleza
chanzo chetu na kuongeza: “Kwa mujibu wa rasimu iliyotolewa na Tume ya Warioba,
ibara ya 215 inapendekeza vyanzo vya mapato kwa Serikali ya Shirikisho la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni ushuru wa bidhaa (excise duty)
na maduhuli yatokanayo na na taasisi za Muungano.
Vyanzo vingine vinavyotajwa katika ibara hiyo ni michango kutoka
kwa washirika wa Muungano na mikopo kutoka ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano. Taarifa ambazo Raia Mwema imezipata kutoka kwa watu wenye
uelewa na masuala ya mapato kutoka Tanzania Bara na Zanzibar zinaonyesha kuwa
mapato ya maduhuli yaliyokusanywa na taasisi za Muungano yanakadiriwa kufikia
Sh bilioni 79. “Maduhuli hayo unayosema ni fedha ambazo vyombo kama Uhamiaji,
Polisi, Jeshi la Wananchi na Wizara ya Mambo ya Nje zinakusanya kutoka katika
vyanzo visivyo vya kodi kama tozo kwa huduma mbalimbali wanazotoa,” kilisema
chanzo chetu kutoka Zanzibar mwishoni mwa wiki iliyopita.
“Ukiangalia takwimu hizo ulizonitajia na mambo ya muungano
yanayopendekezwa na rasimu ya katiba, ambayo yamepungua sana, ni wazi kuwa
gharama za kuendesha muungano zitapungua sana na hivyo zile zitakazotokana na
excise duty na maduhuli zitatosha kabisa kuendesha muungano,” anasema kiongozi
mmoja wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar. Tangu kuzinduliwa kwa Rasimu ya Katiba, wadau mbalimbali
wakiwemo wanasiasa wametoa maoni yao kuhusu kilichomo ndani ya rasimu hiyo,
wengine wakiipongeza Tume huku wengine wakiikosoa hususan kuhusu muundo wa
Serikali Tatu.
Kwa upande wake, Chama cha Mapinduzi (CCM), ambacho kimetoa
mwongozo wa namna ya kujadili na kutoa maoni kuhusu rasimu ya Katiba kwa
wanachama wake, kimekosoa muundo wa Serikali Tatu kikisema utaongeza gharama
kwa wananchi na kuongeza urasimu katika maamuzi. Katibu wa CCM wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amenukuliwa na
vyombo vya habari mwishoni mwa wiki akilalamikia urasimu na ongezeko la gharama
utakaosababishwa na muundo wa Serikali Tatu. Mbali na Nape, wengine waliokosoa kutoka CCM ni pamoja na
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Taifa (ALAT), Dk. Didas Masaburi,
aliyekuwa mkoani Singida hivi karibuni ambako amenukuliwa akisema muundo wa
Serikali Tatu utaongeza mzigo kwa wananchi.
Source: Raia Mwema (August 2013).Takwimu TRA zaipinga CCM kuhusu serikali tatu. Retrieved from Raia Mwema
No comments:
Post a Comment