Ahmed Rajabu
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) ni chama
cha siasa chenye uzoefu wa kutawala kwa muda mrefu barani Afrika kuvipita vyama
vyote vingine. Ni chama chenye ujanja mwingi, ulaghai mwingi lakini pia
kina umahiri wa aina yake. Nadhani cha pili yake barani humo
ni kile cha Movimento Popular de Libertação de Angola – Partido do Trabalho
(kwa ufupi, MPLA) kilichoanza kuitawala Angola tangu nchi hiyo ilipopewa uhuru
wake na Wareno mwaka 1975. Hiki cha MPLA nacho kina ujanja
mwingi, ulaghai mwingi lakini pia kina umahiri wa aina yake. Vyote vinanuka
uvundo wa ufisadi, ingawa kuna kuzidiana.
Kweli ufisadi ni ufisadi lakini
tukiwaweka kwenye mizani tutaona kwamba viongozi wa MPLA wamewazidi wenzao wa
CCM kwa ufisadi. Ufisadi wao umefurutu ada nani wa babu kubwa. Ingawa CCM kiliundwa 1977
vilipounganishwa vyama vya Tanganyika African Union (TANU) na Afro-Shirazi
Party (ASP) kwa hakika kimekuwa na uzoefu wa kutawala tangu Tanganyika ipate
uhuru 1961 na hatamu za utawala kukabidhiwa chama cha TANU. ASP kilianza kutawala tangu 1964
baada ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Wakati wa enzi ya mfumo wa chama
kimoja CCM kilikuwa hakishikiki. Kilijifanyia kitakavyo. Kulikuwa hakuna wa kukisemesha nje
ya chama. Na hata pangekuwako kisingelimsikiliza. Kibri chake kilikuwa kikubwa.
Ndo maana kikawa na mazoea ya kujitwaza. Ndani ya chama kikimsikiliza
Mwalimu Julius Nyerere peke yake wakati wa uhai wake. Wala chama hicho hakikukabiliwa na
upinzani rasmi nchini kwa vile ulipigwa marufuku. Hata ndani ya chama
chenyewe upinzani au ukinzani wa aina yoyote ile haukuwa ukivumiliwa.
Kulifikia lengo hili CCM
kinajaribu kutumia mbinu zile zile kama zinazotumiwa na MPLA nchini Angola
kwani ni wazi kwamba viongozi wa CCM wana mengi ya kujifunza kutoka kwa
viongozi wa MPLA kuhusu namna ya kusehelea katika madaraka. Kwa hili viongozi wa MPLA
wamewapiku wa CCM na zaidi kwa kuwa Angola nayo siku hizi ina mfumo wa vyama
vingi vya siasa. Viongozi wa MPLA wameweza kuwapiku
wale wa CCM kwa sababu vyama vya upinzani vya Angola ni dhaifu mno na havifui
dafu kwa MPLA. Vyama hivyo ni dhaifu kwa sababu MPLA imekuwa ikitumia hila na
mbinu mahususi za kuvivunja nguvu.
La kushangaza na labda
linalohusudiwa zaidi na viongozi wa juu wa CCM ni jinsi viongozi wa MPLA
walivyoweza kuwa madarakani kwa muda mrefu, wengine tangu 1975. José Eduardo dos Santos bado ni
Rais tangu ayashike madaraka hayo Septemba 21, 1979 siku kumi na moja baada ya
kufariki Agostinho Neto, Rais wa kwanza wa nchi hiyo. Nchini Tanzania licha ya upinzani
mkali wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) huko Bara na Chama cha
Wananchi (CUF) Zanzibar — CCM kimejiandaa vilivyo kukiuka vizingiti vilivyopo
bila ya kuonekana kwamba kinafanya hivyo. Mfano mzuri ni mchezo uliochezwa
na makada pamoja na wafuasi wengine wa CCM katika Mabaraza ya Katiba ya wilaya
za Unguja. Ninasema ‘mchezo’ kwa sababu wana-CCM hao walicheza.
Ya Bara siyajui; ya Pemba ni
mengine lakini ya hapa Unguja yanaonyesha wazi jinsi CCM/Zanzibar ilivyojiandaa
kuucheza mchezo wao wakati wa kuichambua Rasimu ya Katiba mpya iliyozinduliwa
Juni 3 na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilal. Kuna jambo moja lililodhihirika
katika vikao vya Unguja vya Mabaraza ya Katiba ambapo Tume ya Mabadiliko ya
Katiba ilipokea maoni ya wajumbe wa mabaraza hayo waliochaguliwa na
wananchi. Nalo ni kwamba wengi wa wajumbe hao walikuwa ni wana-CCM na
walikuwa ‘wamekwishapikwa’ na CCM. Si hayo tu bali wamesikika wazi
wakiimba nyimbo yao hiyo hiyo moja ya kutaka muundo wa Muungano ubakie uwe wa
serikali mbili, kama ulivyo sasa.
Hapa Unguja ni wajumbe wachache
waliopendekeza pawepo muundo wa shirikisho la serikali tatu. Na wachache mno
waliopendekeza Muungano wa Mkataba. Isitoshe. Hao wajumbe
waliotaka serikali mbili wamekuwa pia wakitoa hoja zilizo sare,
zisizotafautiana hata kwa kauli. Wengine wakionekana wakisoma kutoka
waraka wa mwongozo ambao inasemekana walipewa na CCM kuhusu suala hilo. Ni mapema kwa sasa kuweza kujua
iwapo mbinu hiyo ya CCM itafanikiwa hatimaye au la kwa sababu baada ya
kumalizika mikutano ya Mabaraza ya Katiba Septemba 2 mwaka huu, kutabaki hatua
mbili nyingine za kufikiwa kabla ya kupatikana Katiba Mpya.
Ya kwanza ni kujadiliwa Rasimu
katika Bunge la Katiba na ya pili ni ya kuwaachia wananchi waamue kuhusu Rasimu
hiyo kwenye Kura ya Maoni. Binafsi siamini kwamba mbinu hiyo
itafanikiwa. Sababu kubwa niliyo nayo ni kwamba Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba Jaji Mstaafu Joseph Warioba amekwishatoa kauli yake kwamba
vikao hivyo vya Mabaraza ya Katiba vinafuata taratibu maalum zilizopo. Mimi ninaifasiri ifuatavyo kauli
ya Warioba: lengo la Mabaraza ya Katiba ni kuwapa wananchi fursa ya kutoa maoni
yao juu ya namna ya kuifanya Rasimu ya Katiba iwe bora — sio kubadili
mapendekezo makuu ya Rasimu hiyo au kuijadili Rasimu Mbadala ambayo inasemekana
imeandaliwa na CCM.
Aidha Warioba amekwishasema wazi
kwamba hakuna yoyote, ikiwa pamoja na vyama vya siasa, mwenye ruhusa ya kuingia
katika Mabaraza hayo kwa lengo la kushawishi maoni ya aina fulani
yakubaliwe. Lengo la vikao vya Mabaraza ya
Katiba, kwa mujibu wa Warioba, siyo kupiga kura bali ni kujadili na kutoa hoja. Idadi ya Mabaraza yote ya Katiba
ni 177. Kati ya haya Bara ina mabaraza 163 na Zanzibar ina 13. Muundo wa
Muungano wa serikali tatu umekuwa ukiungwa mkono sana huko Bara. Hata hivyo lazima tukubali kwamba
CCM/Zanzibar ‘ilicheza’ kama ilivyozoea kucheza. CCM haikumkiuka Warioba
aliyevionya vyama vya siasa visiviingilie vikao vya Mabaraza ya Katiba.
CCM/Zanzibar ilikuwa na mkakati
mwingine. Baada ya Rasimu ya Katiba kusambazwa katika vijiji, mitaa na
shehia kwa ajili ya kujadiliwa na wananchi CCM/Zanzibar ilikuwa na vikao vya
siri vya kuwaandaa watu wao waliokuwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya
kwa kuwapa mwongozo wa kufuata walipokuwa wanachangia mawazo yao juu ya Rasimu
ya Katiba. Hivyo CCM/Zanzibar haikulala. Muda
wote huu tangu izinduliwe Rasimu ya Katiba imekuwa ikifanya kampeni ya chini
kwa chini na ya dhahiri ya kuwaeleza wanachama wake msimamo wake kuhusu muundo
wa Muungano.
Kwa upande mwingine, watetezi wa
muundo wa Muungano utaoipa Zanzibar mamlaka kamili wamepata pigo kubwa tangu
watiwe ndani mashekhe wa Uamsho ambao ingawa si wanasiasa waliwahamasisha
Wazanzibari na kuwaunganisha juu ya suala hilo. Hivyo sitostaajabu ikiwa
wenye nguvu wataendelea kuwaweka ndani mashekhe hao hadi itapopatikana Katiba
mpya au hata mpaka uchaguzi ujao wa 2015.

No comments:
Post a Comment