Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Sunday, August 4, 2013

Meya kuburuzwa kortini


     JESHI la polisi mkoani Mwanza, limemkamata na kumhoji Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela, Henry Matata, kuhusiana na tuhuma za kutishia kumuua mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia (CHADEMA). Aidha jeshi hilo linatarajia kuwasilisha jalada la tuhuma hizo katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa mtuhumiwa huyo kufikishwa mahakamani. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu, alithibitisha hayo jana wakati alipoulizwa na Tanzania Daima kuhusiana na tuhuma hizo. Kamanda Mangu alisema kuwa Kiwia alitoa taarifa polisi kuhusu kutishiwa kuuawa na Matata, kwamba baada ya kupokea taarifa hizo, jeshi lake lilimshikilia Matata kwa mahojiano maalumu.

     “Polisi tulishapokea malalamiko ya Kiwia na tumemhoji huyu Meya Matata kuhusiana na tuhuma hizi. “Kwa sasa tunaendelea na upelelezi kuwahoji mashahidi, na baada ya kazi hii kukamilika jalada la tuhuma hizi tutalipeleka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa hatua zaidi za kisheria,” alisema. Hata hivyo, alisema tuhuma hizo ni nzito na jeshi lake linafanya kazi bila kumwogopa mtu yeyote mhalifu, hivyo taratibu zote zikikamilika Matata atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo. Matata anadaiwa kutishia kumuua Kiwia Julai 26, mwaka huu, wakiwa katika kikao cha Baraza la Madiwani mbele ya mkuu wa wilaya hiyo, Amina Masenza, askari polisi, madiwani na wajumbe wengine.


      Matata ambaye ni Diwani wa Kata ya Kitangiri aliyevuliwa uanachama wa CHADEMA mwaka jana kutokana na kusababisha mgogoro ndani ya chama mkoani Mwanza, alifungua kesi mahakamani kupinga uamuzi huo, ambapo kesi hiyo bado inaendelea. Katika hatua ya kushangaza, Septemba mwaka jana, Matata alichaguliwa kwenye mkutano ambao ulikuwa haukidhi akidi ya wajumbe ambao ni madiwani 14 kuwa meya wa manispaa hiyo iliyomegwa kutoka katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza. Inaelezwa kwamba chanzo cha vitisho hivyo ni msimamo wa Kiwia na madiwani wa CHADEMA kumpinga Matata kuongoza kikao hicho, ambapo siku hiyo mbunge huyo alisimama na kumuomba Mkurugenzi wa Manispaa, Zuberi Mbyana, amteue mwenyekiti wa muda ili aongoze kikao.

    Julai 28, mwaka huu, Matata aliiambia Tanzania Daima kwamba mbunge huyo asiogope kuuawa labda apunguze mdomo, na akaongeza: “Nisipomuua mimi atauawa na wengine.” Uchaguzi wa Matata ulikiuka kanuni na sheria za halmashauri. Kwa mujibu wa sheria ni kwamba akidi ya wajumbe iliyokuwa ikihitajika kwa ajili ya meya kupigiwa kura ni madiwani tisa badala ya madiwani sita walioshiriki kwenye uchaguzi huo. Badala yake Matata alichaguliwa kuwa meya na madiwani sita pekee, wanne wa CCM na mmoja wa CUF baada ya madiwani wengine wa CHADEMA kususia mkutano huo wa uchaguzi.

Source: Tumma S. ( August 2013). Meya kuburuzwa kortini. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: