Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Thursday, August 1, 2013

Kambi za CCM halali, za CHADEMA haramu?


Danson Kaijage
Mtazamo Wangu


      WANA CCM ni waongo, hawajui watendalo, wanatuyumbisha Watanzania kwa matakwa yao. Watanzania tunataka kujua, Msajili wa Vyama vya Siasa yupo kwa ajili ya vyama vya siasa au kwa ajili ya chama cha siasa? Vyombo vya dola navyo vinafanya kazi ya wananchi au kulinda chama cha siasa? Hapo ndipo napata shida kuelewa. Siku chache zilizopita Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alitangaza kuwa wanajipanga kuanzisha kambi za vijana kwa ajili ya kujilinda kutokana na kuchoshwa na vitendo vya wanachama wa chama hicho kupigwa.

     Nafurahi kuwa kauli ya Mbowe haikuwa ya kificho wala hakuisemea katika mitandao ya kijamii bali alizungumza na waandishi wa habari akiwa na uhakika na kile alichokisema. Matokeo yake viongozi mbalimbali wa CCM wakaibuka na kutaka CHADEMA ifutwe kwani inajipanga kufanya vurugu na kusababisha kupotea kwa amani nchini. Nasema wanasiasa kupinga kauli ya Mbowe ni sawa, kwa sababu ni propaganda, lakini hapa najiuliza kuhusu vyombo vya dola kuingilia kati kauli hiyo na wao kupigilia msumari kuwa kauli ya Mbowe ni hatarishi.
Suala la Mbowe limehamisha mijadala ya kimaendeleo na likawa kubwa na kuona wananchi watapoteza amani kutokana na makundi yatakayoanzishwa na CHADEMA.

     Je, ni kweli au ni kutaka kuwatishia wananchi ambao kwa sasa si wale wa ndiyo mzee? Tutafakari kwa kina uongo na ukweli tunaoupeleka kwa wananchi. Ni sahihi serikali kwa kushirikiana na vyombo vya dola kuinyooshea kidole CHADEMA kwa wazo lao la kutaka kuanzisha kambi za vijana ndani ya chama chao? Kuna sababu gani ya kuwakatalia wakati chama kinachodai ni sikivu wao wana makambi ambayo pia kwa mujibu wa vielelezo mbalimbali kama magazeti yameonesha makambi hayo ya CCM yakitumia silaha za moto? Je, sheria za kuanzisha kambi kwa CCM ni tofauti na zile za uanzishwaji wa makambi kwa vyama vingine vya siasa?

      Ili kuthibitisha kuwa kambi zipo katika vyama vyote, Katibu wa CHADEMA wa Mkoa wa Dodoma, Stephen Masawe, anawataka viongozi wa CCM kusoma kitabu chao cha Sera za Msingi za CCM, toleo la 57 ukurasa wa 87, ibara ya 9.1 (i)(ii)(iii). Masawe anasema Wana CCM pamoja na viongozi mbalimbali wanaopinga kauli ya Mbowe wanatakiwa kusoma zaidi vitabu na sheria ili kutambua kile ambacho wamekuwa wakikisema. Akinukuu sera za msingi za CCM, toleo la 87 ukurasa wa 87 ibara ya 9.1 (I),(ii) (iii) inasema kuwa: 

(i) Umoja wa Vijana CCM unapaswa kuwajenga vijana katika Itikadi, ukakamavu na mafunzo yatakayowafanya wajiamini, wawe vijana wenye ari ya kutimiza wajibu wao wakiwa walinzi wa chama, viongozi na wagombea wa CCM.

(ii) Vijana watambue kuwa kudumu kwa CCM ndio kudumu kwa masilahi yao, maana chama hiki ni chao na wanategemewa kutetea na kulinda mshikamano. Uongozi wa CCM katika kila ngazi uwe na mipango ya kuwasaidia vijana kuwapatia zana wanazohitaji kama usafiri, mawasiliano na kadhalika.

(iii) Utaratibu wa kuandaa kambi za vijana usimamiwe kwa dhati, chama kiwe na mipango mizuri ya kutafuta na kuwateua wakufunzi watakao faa kuwapa vijana mwelekeo unaotakiwa ikiwa ni pamoja na elimu, uchaguzi /uraia.

    Mafunzo ya makambi ya vijana mbali ya kujifunza nyimbo za hamasa yatilie mkazo pia mafunzo ya ukakamavu kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya kihuni vya baadhi ya vijana wa vyama vya upinzani. Kutokana na hali hiyo baadhi ya wanachama wa CHADEMA pamoja na jamii hususan vijana wanamuunga mkono Mbowe, je, kama hairuhusiwi kuwa na kambi kwa nini CCM ambayo tayari ina uzoefu na imefanya kambi mara kadhaa isifutwe ili uwe mfano kwa vyama vingine vya siasa?

    Chonde chonde wananchi tufunguke, viongozi wa nchi kuweni wawazi na vyombo vya dola fanyeni kazi yenu kwa mujibu wa sheria na kanuni zenu pasipo kuwa na mikataba ya siasa. Wakati wa kumweka wakfu Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Jacob Chimeledya, Rais Jakaya Kikwete ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema yanapotokea machafuko viongozi wana mahali pa kukimbilia. Hapa najiuliza yakitokea machafuko yatasababishwa na nini na yatatokea kwa jinsi gani? Je, ni kwa kuukataa ukweli na kukumbatia uonevu au kupindisha sheria? Je, chama tawala watatumia vibaya madaraka yao kwa kuwaonea wasiokuwa na dola na hapo sisi tusiokuwa na mbele wala nyuma tutakimbilia wapi? Je, tutakuwa na uwezo?

No comments: