Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Wednesday, July 10, 2013

Rafu za udiwani zaanza Arusha


MIZENGWE ya uchaguzi wa madiwani wa kata nne za Jiji la Arusha imeanza zikiwa zimebaki siku nne kabla ya kufanyika. Baadhi ya wakazi wa Kata ya Kaloleni wamelalamika kutishiwa kuhamishwa kata na mabalozi wa nyumba kumi wanaopita majumbani kwao usiku kwa madai ya kugoma kutoa shahada za kura. Malalamiko hayo waliyatoa jana kwa waandishi wa habari mkoani hapa. Walisema hivi sasa wanaishi kwa mashaka baada ya kutishiwa na mabalozi wao wa Kata ya Kaloleni kuwa endapo wasipotaka kutoa shahada zao na kunukuliwa na mabalozi hao watahamishwa maeneo hayo wanayoishi. Balozi wa nyumba kumi Kata ya Kaloleni Magharibi, Edington Mshana akizungumzia suala hilo kwa waandishi wa habari, alisema kuwa walipewa maagizo na Katibu wa Tawi la CCM Kaloleni Magharibi, Kata ya Kaloleni aliyemtaja kwa jina Erinesta John.

      Alisema waliambiwa wahakikishe kila balozi anakusanya idadi ya wapigakura wake kwenye nyumba kumi wanazoziongoza ili kujua idadi ya wapigakura na kupata tathimini ya ushindi kwenye uchaguzi utakaofanyika Julai 14 jijini Arusha. Mshana alisema kila balozi katika Kata ya Katoleni alipewa daftari na kalamu ili apite kwenye mtaa wake na kukusanya idadi ya wapigakura wa CCM kupata tathimini ya ushindi, na kwa mtaa wake alipata idadi ya watu 35 ambao aliwaandikisha kwenye daftari hilo na kisha kupeleka kwa katibu wake. “Mabalozi wamepewa maelekezo na baadhi yetu tumeyatimiza, sasa sijui kama hilo ni kosa na ikibainika kama nimefanya kosa kupitia chama changu (CCM) basi nitaamua kuachia ngazi kama nimeingizwa kwenye mkenge nisioujua, maana sielewi, nimetimiza wajibu wangu na wala sijamtishia kumwamisha mtu kwenye eneo langu bali ni kweli nilipita kwa baadhi ya wakazi wa mtaa huu na kutekeleza yale tuliyoambiwa kama mabalozi,’’ alisema.


      Akizungumzia malalamiko hayo msimamizi mkuu wa uchaguzi huo, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Sipora Liana, alisema anaandaa mitego ya kuwakamata wanaohusika na kuendesha zoezi hilo na kampeni za usiku za nyumba kwa nyumba. “Naomba muwasaidie watu hao kwa kuwapa namba yangu ya simu ili hao wanaowafuata usiku wakifika wanipigie nitume askari wakamatwe kwani wanakiuka sheria za uchaguzi kwa kufanya hivyo,” alisema Liana. Homa ya uchaguzi huo inazidi kupanda kutokana na taarifa za ndani kutoka serikalini kuwa uchaguzi huo unafanyika wakati Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwepo kutokana na kudaiwa siku ya Jumamosi kuwa wilayani Monduli kwa ajili ya kutoa kamisheni kwa maofisa wa jeshi.

      Hali hiyo imeongeza ari kwa viongozi wa CCM kuendelea kujipanga kila kona kuhakikisha wanashinda katika uchaguzi huo na kutomtia aibu Rais Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho tawala. Naye Katibu Mkuu wa CCM Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, alisema waliishajiandaa vyema tangu mwanzo katika uchaguzi huo na wanaamini wananchi wa Arusha wanawaunga mkono na hivyo kuwapa kura za kutosha. Tanzania Daima Jumatano, iliwashuhudia askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) wakiwa katika viwanja vyao eneo la Olasiti wakifanya mazoezi jana kuanzia asubuhi hadi majira ya mchana.

       Askari hao wakiwa na viongozi wao walikuwa na vifaa vyote ambavyo hubeba nyakati za kutuliza ghasia wakivitumia katika mazoezi hayo kwa lengo la kuhakikisha wanajiandaa vyema kwa ajili ya uchaguzi huo. Uchaguzi huo wa madiwani unaotarajiwa kufanyika siku ya Jumapili ni wa kujaza nafasi za waliokuwa madiwani wa kata hizo kwa tiketi ya CHADEMA waliotimuliwa uanachama. Kata hizo ni Themi, Kaloleni, Kimandolu na Elerai.

Source: Siwanjombe R. (July 2013)> Rafu za udiwani zaanza Arusha. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: