Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Friday, July 19, 2013

Nyerere: JK ataje wauza ‘unga’


    KUCHAFUKA kwa Tanzania kimataifa ikituhumiwa kuwa ‘lango’ la kusafirisha dawa za kulevya kumewalazimisha wanasiasa kumtaka Rais Jakaya Kikwete kuwakamata haraka vigogo wanaohusika na biashara hiyo. Mmoja wa wanasiasa hao, Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Vincent Nyerere (CHADEMA), amelazimika jana kutoa taarifa kwa vyombo vya habari nchini akimwomba Rais Kikwete kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika ambao aliwahi kudai anawajua kwa majina. Nyerere ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani, katika taarifa yake alisema Rais Kikwete ndiye aliyeutangazia umma kuwajua wahusika wa biashara hiyo, lakini ameshindwa kuwataja, badala yake kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaojihusisha na biashara hiyo kiasi cha kuchafua jina la nchi katika ngazi za kimataifa.

        Alisema kushamiri kwa biashara hiyo haramu kiasi cha kuilazimu serikali kutangaza kuwa janga la taifa kunatoa picha kwamba imezidiwa nguvu na vigogo wanaoendesha biashara hiyo. “Rais Kikwete alisema anawafahamu wafanyabiashara wa madawa ya kulevya na alipiga hatua kubwa zaidi na kusema wamo pia viongozi wa dini, lakini nashangaa kuona sasa hajafanya hivyo, licha ya maaskofu kumtaka awataje hadharani,” alisema Nyerere. Mbunge huyo alisema ukimya wa rais, huku hali ikizidi kuwa mbaya kutokana na kuwapo kwa madai ya kukamatwa kwa wasichana wawili Watanzania nchini Afrika Kusini wakiwa na kilo 150 za madawa ya kulevya yenye thamani ya sh bilioni sita, kunazidi kuzua maswali mengi.

      “Ukimya wa rais unaweza kuchukuliwa kuwa serikali yake haina tena ubavu wa kupambana na wauza unga, jambo ambalo ni hatari kwa vijana wetu,” alisema. Mbali na kutaka rais kuchukua hatua, Nyerere pia aliwataka Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema, kuwaeleza Watanzania kulikoni hadi Tanzania inakuwa uchochoro wa kupitisha dawa za kulevya katika ukanda huu wa Afrika Mashariki. Mbunge huyo alimtaka pia Kamishina wa Tume ya Dawa za Kulevya kujieleza, iweje kiasi kikubwa cha dawa za kulevya katika tukio la hivi karibuni la kukamatwa kwa wasichana hao nje ya nchi kiliweza kupitishwa katika uwanja wa ndege bila kujulikana.

      Watu wengine maarufu waliowahi kuzungumzia hatari ya biashara hiyo na tuhuma za kuhusisha watu wazito nchini ni pamoja na Mwenyekiti wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi na Mbunge wa Jimbo la Mwibara, Kangi Lugola (CCM). Ripoti iliyotolewa mwaka jana na Tume ya Kupambana na Dawa za Kulevya ilibainisha kuwa kati ya mwaka 2008 na 2012, watuhumiwa 10,799 walikamatwa na dawa za kulevya hapa nchini, wengine 240 wakikamatwa na dawa hizo katika nchi za Brazil, Pakistan, China na Afrika Kusini, jambo ambalo limetia dosari kubwa katika jumuiya ya kimataifa.

Source: Tanzania Daima (July 2013). Nyerere: JK ataje wauza "unga". Tanzania Daima

No comments: