Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Saturday, July 6, 2013

Mwenyekiti CCM aibua utata


         MADAI ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Gairo, Omar Awadhi kwamba amemwagiwa tindikali, yameibua utata baada ya kubainika kuwa hakukuwa na tukio la aina hiyo. Taarifa za mwenyekiti huyo kumwagiwa tindikali, zilisambaa kwa kasi nchi nzima mwishoni mwa wiki, huku baadhi ya wanasiasa wakilihusisha na itikadi za vyama vya siasa. Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa kuzungumza na viongozi na makada mbalimbali wa CCM wilayani hapa, umebaini kuwa mwenyekiti huyo hakumwagiwa tindikali badala yake alitumia mbinu hiyo kukwepa kuenguliwa na wajumbe wa mkutano wa Halmashari Kuu ya Wilaya uliofanyika siku moja baada ya tukio la kumwagiwa tindikali.

       Mmoja wa makada wa CCM wilayani hapo ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema siku moja baada ya kudai kumwagiwa tindikali, mwenyekiti huyo aliendesha kikao cha Halmashauri Kuu ya Wilaya ambacho pamoja na mambo mengine kilipanga kumshughulikia baada ya kutoridhishwa na utendaji wake. “Kwa hiyo kutokana na hofu hiyo, ghafla tukasikia kamwagiwa tindikali lakini asubuhi alipokuja ukumbini tulimwona akiwa mzima wa afya. Tulipomuuliza alisema aliwahi kunawa maji, hivyo hakudhurika. Hivyo aliendesha kikao hadi mwisho na hakukuwa na ajenda ya kumshughulikia,” alisema kada huyo. Akizungumza na gazeti hili juu ya sakata hilo, Mwenyekiti Awadhi alisisitiza kuwa alimwagiwa tindikali, lakini aliwahi kunawa maji hivyo hakudhurika.

     Alisema anahisi kitu alichomwagiwa ni tindikali kwani sehemu ilipomwagikia, imeunguza sakafu. “Walikuja watu usiku, wakaniita kutoka dirishani, nilipochungulia walinimwagia kitu chenye maji ambacho nahisi ni tindikali, lakini haikunipata vizuri na nikawahi kunawa maji,” alisema. Mwenyekiti huyo alililalamikia Jeshi la Polisi mkoani Morogoro kwa kutochukua hatua tangu alipotoa taarifa za kumwagiwa tindikali. Alienda mbali zaidi kwa kuwatuhumu baadhi ya wanasiasa wilayani humo kwamba ndio waliopanga kumdhuru kwa sababu za kisiasa.

Source: Tanzania Daima (July 2013). Mwenyekiti CCM aibua utata. Gairo. retrieved from Tanzania Daima

No comments: