Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Tuesday, July 23, 2013

Mchele wa nje waharibu soko la mpunga nchini


MAKALA 
Rodrick Mushi

KUSHUKA kwa bei ya mpunga kwa zaidi ya asilimia 50 mwaka huu tofauti na bei iliyokuwa sokoni msimu uliopita kumewaathiri wakulima wa mpunga katika mikoa mbalimbali nchini. Wakulima wengi wanaeleza kuwa wamelazimika kuuza mpunga kwa bei ya hasara ili kupata fedha ya kurejesha kwenye mikopo waliyokopa na kuwekeza kwenye kilimo kinachoendesha maisha yao ya kila siku.

     Kushuka kwa bei ya mchele kumesababishwa na asilimia kubwa serikali kuruhusu kuingizwa mchele kutoka nje ya nchi ili kuweza kupunguza mfumuko wa bei. Gunia la mpunga kwa wakulima wa Kata ya Magugu mkoani Manyara wanauza sh 50,000 hadi 40,000, kitu ambacho wameeleza kuwa kuna tofauti kubwa na msimu uliopita ambapo gunia lilikuwa likiuzwa kwa sh 100,000.

     Utafiti uliofanywa na mwandishi wa makala hii kwenye mikoa ya Manyara, Kilimanjaro, Tanga na Morogoro umebaini kuwapo kwa tofauti ya bei ambapo maeneo mengine hususan maeneo ya vijijini hali ni mbaya zaidi. Kwa baadhi ya masoko ambayo niliweza kufanya utafiti mchele unaotoka nje ya nchi ndio umeteka soko la ndani zaidi kutokana na bei unaouzwa sh 700 kwa kilo kuwa tofauti na mchele unaozalishwa nchini.

      Kwa upande wa Mkoa Manyara, Jumanne Athumani, ambaye ni Katibu wa Skimu ya Muungano, anasema skimu hiyo pekee zaidi ya wakulima 492 waliolima zaidi ya ekari 913 waliweza kupata zaidi ya magunia 27,390 na watalazimika kuuza kwa bei ya hasara. Anasema kwa ekari moja wana uwezo wa kuvuna magunia 28 hadi 30, ambapo kwa ekari moja hugharamikia kiasi cha sh 700,000 hadi sh 1,000,000, hivyo kushuka kwa bei kumekuwa hasara kubwa kwa wakulima.


      Kutokana na kushuka kwa bei ya mpunga, wakulima wa vijiji zaidi ya vinne vya Kata ya Magugu ambapo ni sawa na tarafa nzima ya Mbugwe watapata hasara ya zaidi ya sh bilioni 2.5 katika msimu huu wa kilimo. Licha ya wakulima kulima kila mwaka lakini mwaka huu kwao imekuwa sawa na kilio kutokana na kukopa kwa ajili ya kilimo hicho cha mpunga kuwalipia watoto wao ada pamoja na kuendesha familia zao.

     Wakulima wa Magugu wanategemea kilimo cha umwagiliaji, wanachoeleza kuwa kila mwaka wanatakiwa kukarabati mifereji kwa ajili ya msimu mwingine wa kilimo ambapo pia inahitajika gharama. Ofisa Mtedaji wa Kijiji cha Matufa, Selini Mwangumba, anamueleza mwandishi alipofika kijiji hapo kuwa kushuka kwa bei ya mpunga kumewaathiri wakulima kwa kiasi kikubwa kwani asilimia 80 ya wakulima wanategemea kilimo cha mpunga.

    Wananchi wilayani Lushoto, Mkoa wa Tanga, Tarafa ya Umba nao wanalalamikia kushuka kwa bei ya mchele mpaka kufikia sh 25,000 kwa gunia la mpunga, kitu ambacho kimewasikitisha na kukata kabisa tamaa ya kuendelea na kilimo hicho, kwani hata gharama yao waliyotumia katika kulima haijarudi.

      “Kama mkulima angekuwa analima kwa kuhesabu na kuandika kila gharama anazotumia katika kilimo na mwisho wa siku katika kipindi cha mavuno kufanya mlinganisho kama amepata faida kutokana na gharama alizotumia, wengi ungekuta hawalimi,” hiyo ni kauli ya Masumbuko Francis, mama mwenye watoto wanne, anayejishughulisha na kilimo cha mpunga eneo la Chito kwenye Bonde la Kilombero.

    Anasema mpunga kushuka bei kumewaathiri kwa kiasi kikubwa, kwa kuwa mpunga ndio kilimo wanachotegemea kwa ajili ya kulea familia pamoja na kusomesha watoto wao, ambapo kwa sasa wamefika elimu ya vyuo. Kushuka kwa bei ya mpunga kumekuwa na madhara makubwa kwake, ambapo hadi sasa watoto wake ambao wanasoma wameshindwa kuendelea na masomo baada ya mpunga aliolima mwaka huu bei yake kushindwa kufikia malengo aliyokuwa anahitaji kusomesha watoto.

    “Bei ya mchele imeanza kupungua msimu wa mwaka 2012 na 2013 ambapo wakulima tunategemea kuuza mpunga kwenye Desemba na Januari kwa ajili ya maandalizi ya shamba lakini mwakaa huu mambo yalikuwa tofauti,” anasema. Mkulima, Stanford Magige, ambaye katika msimu huu amelima ekari 80 za mpunga anasema kuwa kilimo cha mpunga kinakabiliwa na changamoto mbalimbali, lakini suala la kushuka kwa bei limezidi kumpigilia msumari mkulima.

    Anasema kuwa kwa sasa gunia la mpunga lenye ndoo 10 linauzwa kwa sh 40,000 hadi 35,000 tofauti na ilivyokuwa mwaka jana ambapo gunia lilikuwa linauzwa sh 100,000. Nilifika kwenye vijiji vya Nawala, Ilete, Mlimbi na Mkangawala ambavyo wakulima wanakuomba kununua mpunga wao, hata kwa bei ya hasara, debe hadi sh 400 ili kuweza kuhudumia familia zao. Wakulima wanazungumza kwa uchungu na inasikitisha, kwani baadhi ya fedha walizokuwa nazo walitumia kununua pembejeo na kuishia kwenye kilimo wakitegemea kuwa baada ya mavuno watapata ahueni lakini mambo yamekuwa tofauti.

   Magige anasema kuwa wakulima wamekuwa wakiteseka na kutumia gharama kubwa katika uzalishaji, hivyo kitendo kilichofanywa na serikali kuingiza mchele kutoka nje ya nchi ni kuendelea kuwakandamiza wakulima. “Badala ya serikali kuruhusu mchele ambao unatoka nje ya nchi, kwanini isingenunua mchele kutoka kwa mkulima na kuhifadhi wakati wa mavuno ili kusaidia kuwapo kwa bei nzuri hususan wakati wa mavuno?,” anahoji Magige.

     Mkulima huyo anaeleza kuwa wakulima wanalima kwa kutumia gharama zao wenyewe lakini wanapangiwa kutouza nje ya nchi, lakini serikali inaingiza mchele na kuuzwa kwa bei rahisi huku mpunga wao ukikosa soko na mwingine kuharibika. “Wakati mwingine wakulima tunaona kuingia kwenye sekta ya kilimo ni sawa na kupotea kwa kuwa licha ya kuwa na mchango mkubwa kwa taifa lakini wakulima hatuthamini sisi ndio tunatumika kama chambo linapotokea tatizo lolote nchini,” anasema.

    Magige anasema kwa sasa wakulima hao wa mpunga wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo teknolojia duni wanayotumia katika uvunaji ambayo inapoteza mazao, pamoja na kuwapo kwa ushuru mkubwa wa sh 5,000 kwa gunia. Wakulima wanasema licha ya serikali kuwapiga mabomu wakati wakidai kupunguziwa ushuru, bado imeendelea kutoza ushuru kwa zaidi ya asilimia 200, ambao umekuwa mzigo mkubwa kwa wakulima.

     Awali ushuru wa mpunga ulikuwa ukitozwa sh 1,000 kwa gunia la kilo 100 za mpunga lakini kwa sasa unatozwa sh 5,000 kwa gunia lenye uzito huo, au asilimia tano ya bei iliyopo sokoni kwa gunia. “Ukiangalia mazao tunalima sisi wenyewe kwa gharama zetu lakini serikali ndiyo inatupangia tuuze wapi, mbaya zaidi wametuzuia kuuza nje lakini wao wameingiza mchele kutoka nje na sisi mpunga wetu kushuka bei,” anasema.

    Jukwaa la Kilimo kupitia kwa Mkurugenzi wake, Audax Rukonge, anasema kuwa nchi haiwezi kuendelea kuingiza mazao ya chakula kutoka nje ya nchi, kinachotakiwa ni kuwawezesha wakulima kwani asilimia 80 ya chakula nchini kinazalishwa na wakulima wadogo. “Ifike wakati serikali imhurumie mkulima na kubadilisha mtazamo kuwa kilimo ni biashara na mkulima naye anataka kupata faida,” anasema Rukonge. Kila kukicha changamoto kwa mkulima zinaibuka upya ingawa zilizokuwepo bado hazijatatuliwa, kama serikali ilivyoamua kuingiza mchele kutoka nje ili kushusha bei na kumfurahisha mkulima huku mkulima akiendelea kuumia.

No comments: