MIONGONI mwa wabunge wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaosisimua watu wanapochangia hoja bungeni ni
Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CHADEMA, Leticia Nyerere. Mwandishi wa Tanzania
Daima Jumapili, George Maziku, amefanya mahojiano maalumu na mbunge huyo.
Tanzania Daima Jumapili: Kwa kipindi kifupi ulichokaa bungeni umeonyesha
uwezo mkubwa, umekuwa mbunge unayejiamini tofauti na wabunge wengi wanawake,
umewezaje kuwa hivyo?
Leticia: Kwanza mimi nimezaliwa na kukulia katika familia ya
mwanasiasa, baba yangu marehemu Musobi Mageni alikuwa waziri wakati wa uongozi
wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na baadaye akawa Mwenyekiti wa taifa wa
CUF. Kwa hiyo nilijifunza mambo mengi
kutoka kwa marehemu baba yangu. Pia nimebahatika kuishi karibu sana na
mwanasiasa mahiri, hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere nilipoolewa
katika familia yake na nilijifunza mengi kutoka kwake.
Hata hivyo, ujasiri na kujiamini
nimeupata kutokana na kuishi kwangu kwa muda mrefu nchini Marekani, ambako
jamii ya kule inaheshimu na kuthamini haki za binadamu zikiwamo haki za
wanawake. Wenzetu hawana tofauti kati ya
mwanamke na mwanamume, ukiacha tofauti za maumbile tu. Wanaamini kuwa mwanamke
na mwanamume wana uwezo sawa wa akili, mawazo na fikra.
Mimi huwa simuogopi mwanamume yeyote
kwasababu siamini kama mwanamume ana akili nyingi au uwezo mkubwa wa utendaji
kazi kuliko mwanamke, naamini wote tuko sawa na inawezekana mimi mwanamke
nikawa na akili na uwezo mkubwa zaidi kuliko mwanamume. Kwahiyo, kama kuna mwanamume anadhani
anaweza kutumia jinsia yangu kama nyenzo ya kupambana nami kisiasa
anajidanganya sana.
Akitokea mwamume wa aina hiyo siwezi
kulalamika wala kulialia ila nitapambana naye kikamilifu mpaka aione dunia chungu.
Mimi namuogopa Mungu pekee, lakini si binadamu kama mimi.
Tanzania Daima Jumapili:
Mwaka 2010 uligombea ubunge katika Jimbo la Kwimba,
pamoja na kwamba ilikuwa mara yako ya kwanza lakini ulionekana kuwa na uelewa
wa mambo ya siasa na ulitoa upinzani mkubwa dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM
ambaye ndiye mbunge wa sasa wa jimbo hilo, hali hiyo ilitokana na nini? Je,
utagombea tena mwaka 2015?
Leticia: Uelewa na uzoefu wa mambo ya siasa nimeupata
Marekani kwasababu mwaka 2008 nilikuwa katika timu ya kampeni ya Rais Barack
Obama na nilikuwa kiongozi wa kundi la watu 80 tuliokuwa tukimfanyia kampeni
Rais Obama katika Jimbo la Virginia. Tulipatiwa mafunzo mazuri ya
kutuwezesha kusimama majukwaani na kujenga hoja za kutaka Rais Obama
achaguliwe, hiyo ilinisaidia sana. Kuhusu kugombea mwaka 2015, hilo lipo
wazi kabisa, najiandaa kugombea tena na ninaendelea kufanya kazi kwa
kushirikiana kwa karibu na wananchi wa Kwimba.
Tanzania Daima Jumapili: Umezaliwa na kukulia kwenye familia ya mwanachama na
kiongozi wa TANU na baadaye CCM, baadaye ukaolewa kwenye familia ya mwasisi wa
TANU na CCM hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere; ilikuwaje wewe
ukajiunga na chama cha upinzani?
Leticia: Itikadi haina uhusiano wowote na mahusiano ya kifamilia.
Itikadi ni mtazamo binafsi wa mtu na inatokana na uchambuzi wa kina anaoufanya
kila mtu kuhusu mambo mbalimbali, iwe siasa, uchumi au jamii. Mimi siamini kwamba mtazamo wa baba
au mama kuhusu siasa unapaswa kuwa pia mtazamo wa watoto, kila mtu ana uhuru
wake wa kuamini chochote bila kuingiliwa na wazazi au wanafamilia wengine.
Kwa mfano, kule Marekani aliyekuwa
Gavana wa California, Anold Schwazniger, ni mwanachama wa Chama cha Republican
wakati mkewe ni mwanachama wa Democratic na hapakuwa na tatizo lolote. Hata baba mkwe wangu hayati Mwalimu
Nyerere nilikuwa nikimwambia wakati wa uhai wake kuwa mfumo wa chama kimoja cha
siasa haufai. Napenda ifahamike kuwa haifai na ni
kinyume cha demokrasia na haki za binadamu kwa mzazi, mume au mke kuwalazimisha
wanafamilia wao kufuata itikadi zao. Tunapaswa kubadilika haraka kimtazamo ili
kila mtu afurahie uhuru wake wa kisiasa.
Tanzania Daima Jumapili: Kuna watu wanadai kuwa viti maalumu haviwasaidii
wanawake kujenga ujasiri na uwezo wa kisiasa na badala yake wanadai
vinawapumbaza na wanataka vifutwe, wewe unasemaje?
Leticia: Nafikiri ni muhimu viendelee kuwapo kwa sababu ni
muhimu wanawake kujumuishwa kwa usawa katika vyombo vya maamuzi na kutunga sera
katika nchi. Wanawake ni kundi kubwa sana na wana
mchango mkubwa sana katika kila nyanja ya maisha ya binadamu, iwe uchumi,
siasa, au jamii, hivyo wanastahili kuwakilishwa kwa usawa na wanaume.
Kwahiyo, cha kujadili hapa kwa
mtazamo wangu ni namna ya kuwapata hao wawakilishi wa wanawake katika vyombo
hivyo vya kutunga sheria na sera, na mimi ninaunga mkono mfumo uliopendekezwa
na Tume ya Jaji Joseph Warioba kwamba kuwe na wagombea wawili katika kila
jimbo, yaani mmoja mwanamke na mwingine mwanamume.
Tanzania Daima Jumapili: Watu wanadai kuwa wabunge wanawake wengi hawana msaada kwa
wanawake wenzao walio nje ya Bunge, na kwamba wengine wamekuwa wakiwahujumu
wanawake wenzao wanaoonyesha kunyemelea nafasi zao, una maoni gani kuhusu hilo?
Leticia: Sijui kwa wabunge wengine, lakini kwa upande wangu
siamini kama kuna ukweli wowote kwasababu nimekuwa nikiwasaidia wanawake
wengine hususan katika Jimbo langu la Kwimba kuwajengea uwezo wa kisiasa na
kiuongozi. Pia ni wajibu na jukumu la kila
mwanamke kuonyesha utayari wa kuwa mwanasiasa. Lazima wewe binafsi ufanye kazi
kwa bidii na ujiandae kikamilifu kwa kila nyanja ili kukuwezesha kuwa
mwanasiasa na kiongozi katika jamii yako, usisubiri kuwezeshwa na mtu, mimi
nilifanya hivyo mpaka kufikia hapa nilipo.
Tanzania Daima Jumapili: Kuna maneno ya hapa na pale kwamba ninyi wabunge
wanawake wengi wenu mmepata nafasi hizo kwa upendeleo wa undugu, urafiki na
hata rushwa ya ngono, na kwamba wengi wenu hamna uwezo, nini maoni yako kuhusu
tuhuma hizi?
Leticia: Si kweli kabisa na ni dharau mbaya sana kwa wanawake wote.
Kila chama kina njia na vigezo tofauti vya kuwapata wabunge wanawake. Sisi
katika CHADEMA tuna vigezo vyetu ambavyo vilitumiwa kuwapata wabunge wanawake
wote wa chama chetu, hapakuwa na upendeleo wa aina yoyote.
Kwa mfano, mimi sikujua hata kidogo
kuwa nitakuwa mbunge kwasababu wakati wa mchakato nilikuwa kwenye kampeni zangu
za ubunge Jimbo la Kwimba. Na baada ya uchaguzi nilianza kuwasiliana na mwajiri
wangu nchini Marekani kumuomba nirejee kazini kwa sababu nilikuwa nimeshindwa
kuchaguliwa mbunge. Baadaye Tume ya Uchaguzi ilitangaza majina ya wabunge wa
viti maalumu na jina langu likawemo, ndipo nikaahirisha kurudi Marekani.
Tanzania Daima Jumapili: Wewe ni mwanamke mwenye familia, unafanyaje kutofautisha
majukumu yako ya kikazi na kifamilia?
Leticia: Sipati shida, nina muda wa kufanya kazi zangu kama mama wa
familia na pia muda wa kutekeleza kazi zangu kama mbunge na mwanasiasa. Familia yangu inaelewa kuwa nina
wajibu wa kufanya kazi na wakati mwingine kusafiri kikazi, hawana tatizo.
Isitoshe sina watoto wadogo nyumbani, watoto wangu wote ni wakubwa na wapo
Marekani wanasoma vyuoni.
Tanzania Daima Jumapili: Wewe ulikuwa waziri kivuli, ilikuwaje ukajiuzulu?
Leticia: Nilitaka kuwapatia watu wengine nafasi ya kujifunza,
hapakuwa na tatizo lolote kati yangu na viongozi wangu ndani ya Bunge wala
katika chama. Ni vizuri kila mbunge wa CHADEMA akapata nafasi ya kujifunza
mambo ya uongozi.
Tanzania Daima Jumapili: Unafanya nini kama haupo bungeni? Je, unasoma au unafanya
biashara?
Leticia: Nasoma shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu
Huria cha Tanzania (OUT). Nasoma sayansi ya siasa na sasa hivi nafanya utafiti
na nimeamua kutafiti masuala ya wanawake na uchaguzi Tanzania, na nategemea
kumaliza mwakani.
No comments:
Post a Comment