Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Sunday, July 7, 2013

CCM watwangana



       HALI ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na jumuiya zake inazidi kudorora siku hadi siku, ambapo juzi usiku kulitokea vurugu kubwa katika kikao cha Kamati ya Utekelezaji ya Taifa ya Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT). 
Vurugu hizo zilisababisha kikao hicho kilichofanyika kwenye makao makuu ya jumuiya hiyo jijini Dar es Salaam kuvunjika. Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa chanzo cha kuvunjika kwa kikao hicho majira ya saa 4:30 usiku ni vuta nikuvute ya nani ateuliwe kushika wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu Bara na Zanzibar. Majina yaliyopendekezwa na Mwenyekiti wa Taifa, Sophia Simba, ndiyo yaliyozusha vurugu na mabishano makali huku baadhi ya wajumbe wa kikao hicho wakipinga uteuzi huo.

    Wapingaji wa majina hayo walidai kuwa uteuzi wa Simba haukuzingatia sifa na vigezo vinavyoweza kuupa heshima umoja huo nchini. Simba aliingia kikaoni akiwa na majina mawili la Salama Aboud Talib kutoka Zanzibar na kwa upande wa Bara alipendekeza jina la Ever Kiwele. Majina hayo yaliwafanya wajumbe kukataa kuyapitisha kwa madai kuwa hila zilitumika kuyateua. Tanzania Daima Jumapili, lilidokezwa kuwa msimamo wa wajumbe haukumzuia Simba kutetea uteuzi wake ulioonekana kuwagawa wajumbe. Habari zaidi zinadai licha ya Simba kutetea uteuzi wake, wajumbe walimtaka aache kukiburuza kikao na jumuiya hiyo kwa manufaa binafsi kama anavyotaka kufanya.


    “Wajumbe naomba kuwasilisha kwenu majina mawili ya Salama Aboud na Ever Kiwele kuwa manaibu katibu wakuu Bara na Zanzibar, natumaini mtaheshimu uteuzi wangu na kuyapitisha kwa masilahi ya Jumuiya yetu,” alisikika Simba. Mjumbe mmoja kutoka Kanda ya Mashariki (jina tunalo) alisimama na kukiambia kikao kuwa kuna haja na umuhimu wa kupitishwa kwa majina ya manaibu katibu mkuu kulingana na vigezo vya elimu, sifa njema katika jamii na utendaji usio na makovu ya ubadhirifu wa mali za jumuiya. Mjumbe huyo alisema litakuwa ni kosa kubwa kuyapitisha majina hayo kabla ya tuhuma mbalimbali zinazowakabili kupatiwa majibu ya msingi.

     Alitaka wajumbe hao waeleze kuhusu mali za jumuiya kama kuuzwa kwa nyumba za UWT zilizoko Zanzibar, pia uwezo wa kielimu wa kila mtendaji. Kutokana na hali hiyo, Katibu Mkuu wa UWT, Amina Makilagi, alilazimika kutoka nje ya kikao kupisha mjadala juu yake. Kundi kubwa la wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji walidai kutoridhishwa na utendaji wa manaibu katibu wakuu, zikiwamo tuhuma za ubinafsi na utendaji usio na ufanisi wa jumuiya hiyo. “Mwenyekiti kwa heshima kubwa ya chama chetu na jumuiya, hapa tulipofika inatosha, hatuko tayari kuona jumuiya yetu ni shamba la bibi, genge la marafiki na ushoga na badala yake sasa tunahitaji kujipanga ili kujenga imani na kupata ushindi mwaka 2015, vinginevyo ‘no way’”, alisikika akisema mjumbe mmoja kutoka Kanda ya Ziwa.

   Mjumbe huyo alisema kitendo cha kupendekeza watendaji dhaifu kinakwenda kinyume cha wosia wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete. Alisema Rais Kikwete alizitaka jumuiya za CCM kuwa na viongozi wenye upeo kielimu na kiutendaji kutokana na mabadiliko ya kisiasa ulimwenguni. “Mwenyekiti uteuzi wako ni zaidi ya usaliti kwa Mwenyekiti wetu wa CCM, hatuko tayari kumlamba kisogo Dk. Kikwete na kupuuza ushauri wake, majina uliyotuletea siyo na hatuko tayari kuyapitisha kwa namna yoyote iwavyo,” alisema mjumbe huyo. Mjumbe mmoja kutoka Zanzibar alisikika akisema ni vema wakawa na UWT yenye hadhi na heshima kama enzi za Bibi Titi Mohamed na Sofia Kawawa waliofanya kazi kwa kuweka mbele masilahi ya wanawake na maendeleo, badala ya urafiki na kuteketeza mali za jumuiya. Jitihada za Tanzania Daima Jumapili kuzungumza na Sophia Simba kwa undani zaidi ziligonga ukuta baada ya simu ya kiongozi huyo kuita kwa muda mrefu bila majibu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu hakujibu.

Source: Tanzania Daima (July 2013). CCM waumizana. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: