*Rasimu kutumika kuwaondolea sifa ya kugombea urais
*Yumo pia Membe, Magufuli, Sitta, Zitto na Wassira
MKAKATI wa
kuwaengua vigogo wanaotajwa kung’ang’ania kugombea nafasi ya Urais katika
Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 sasa umebainika, MTANZANIA Jumapili linaripoti. Kwa mujibu wa
uchunguzi wa kina uliofanywa na gazeti hili, mkakati huo ambao umelenga
kuwang’oa viongozi hao, unadaiwa kutekelezwa na baadhi ya wanasiasa ndani ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Rasimu ya Katiba Mpya, iliyotolewa hivi
karibuni na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Imeelezwa kuwa
kupitia Rasimu hiyo ya Katiba Mpya, kuna vipengele vilivyopenyezwa kwa nia ya
kuwabana watu fulani fulani ndani na nje ya CCM ambao wanatajwa kuusaka ukuu wa
dola mwaka 2015 na chama hicho hakitaki kuona wanakuwa kikwazo dhidi yake.
Mtoa habari
wetu ndani ya CCM alilidokeza gazeti hili kuwa vipengele hivyo ambavyo
vimewekwa kama mtego, ni vile vinavyotaja sifa za mgombea Urais na mgombea
Ubunge. Kwa mujibu wa taarifa
zilizotufikia, kutokana na hilo, baadhi ya wanasiasa ndani ya CCM kwa makusudi
wameamua kuufanya mjadala kuhusu serikali tatu kuwa mkali, ili kuzuia mjadala
mpana katika masuala mengine. Kipengele ambacho kama
kikiachwa bila kufanyiwa marekebisho kinaweza kuwabana wanasiasa wengi ndani na
nje ya CCM wanaotajwa kuwania Urais 2015 ni pamoja na kile cha Sura ya Saba,
ambacho kinazungumzia Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuhusu Serikali, Rais na
Makamu wa Rais, katika sehemu ya kwanza C kwenye kipengele cha 75 (E)
kinachozungumzia sifa za Rais kimeeleza kuwa mtu atakuwa na sifa ya kuchaguliwa
kushika nafasi ya madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano ikiwa: anazo sifa za
kumwezesha kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Katiba
hiyo.
Vigogo hao wanaotajwa
kutoka CCM ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Mbunge wa Monduli,
Edward Lowassa, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, Waziri wa Uchukuzi, Dk.
Harrison Mwakyembe na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe. Wengine ni Waziri wa Mambo
ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi na Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia,
Januari Makamba, wakati kutoka Chadema ni Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, Katibu
Mkuu wa chama hicho, Dk. Willbroad Slaa na Zitto Kabwe.
Watakaokuwa wametupwa nje
Kulingana na sifa
zinazotajwa kwenye kipengele hicho, viongozi wanaotajwa kutaka kuwania nafasi
hiyo lakini watakuwa wamegonga mwamba ni pamoja na wafuatao; Edward Lowasa ambaye
aliwahi kuwa Waziri Mkuu kwa muda wa miaka miwili na hadi sasa ni Mbunge wa
Monduli kupitia CCM, ameshika nafasi hiyo kwa vipindi vitano vya miaka 25 kuanzia
mwaka 1990 hadi sasa, moja kwa moja atakuwa amepoteza sifa ya kuwania Urais,
kwani tayari amezidi vipindi vitatu vya kuwa mbunge. Samuel Sitta, ambaye ni
Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), ameshika nafasi hiyo kwa vipindi sita kwa
muda wa miaka 30, kuanzia mwaka 1975 hadi 1995 na 2005 hadi sasa, naye pia
atakuwa amepoteza sifa.
Dk. John Magufuli, ambaye
ni Mbunge wa Chato (CCM) kwa vipindi vinne vya miaka 20 kuanzia mwaka 1995 hadi
2015, naye atakuwa ameshapoteza sifa, kwani amezidi vipindi vitatu. Bernard Membe, ambaye pia
ni Mbunge wa Mtama (CCM) naye atakuwa ametupwa nje, kwani hadi sasa ameshika
nafasi hiyo ya Ubunge kwa vipindi vitatu vya miaka 15 kuanzia mwaka 2000 hadi
2015. Dk. Willborad Slaa,
atakuwa ametupwa nje ya ulingo kwani amewahi kutumikia vipindi vitatu vya
Ubunge kunzia 1995 hadi 2010 katika Jimbo la Karatu kwa kupitia Chadema. Zitto Kabwe ambaye ni
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, atakuwa ametimiza sharti la kuwa mbunge kwa vipindi
viwili, lakini atagonga mwamba katika sharti la umri, kwani atakuwa hajatimiza
umri wa miaka 40 kama rasimu ilivyoendelea kupendekeza, badala yake atakuwa na
umri wa miaka 39.
Waliosafishiwa njia
Dk. Harrison Mwakyembe,
ambaye ni Mbunge wa Kyela (CCM) ameshika nafasi hiyo vipindi viwili vya miaka
10 kuanzia mwaka 2005 hadi 2010. Dk. Emmanuel Nchimbi
ambaye ni Mbunge wa Songea Mjini (CCM) ametumikia nafasi hiyo kwa kipindi
kimoja cha ubunge wa jimbo kuanzia mwaka 2010 hadi sasa. Januari Makamba, ambaye ni
Mbunge wa Bumbuli (CCM) amedumu kwa kipindi kimoja kuanzia mwaka 2010 hadi sasa
hivyo atakuwa na sifa za kuwania urais. Freeman Mbowe, ambaye ni
Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema na Mbunge wa Hai, naye atakuwa na sifa ya
kuwania nafasi hiyo, kwani atakuwa ametumikia nafasi hiyo kwa vipindi viwili
kwa miaka 10 kuanzia 2000 hadi 2005 na 2010 hadi sasa. Suala la Urais limezua
mjadala mkubwa ndani na nje ya CCM, baadhi wakikomoana kuhakikisha mwingine
hapiti kwenye nafasi hiyo. CCM ndicho kinachoonekana kuathirika zaidi, kwani
jambo hilo tayari limesababisha makundi yanayosigana.
Source:Mushi G. (July 2013). Dk. Slaa, Lowassa wawekewa mtego - Waliosafishiwa njia. Retrieved from Mtanzania
No comments:
Post a Comment