Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Tuesday, June 18, 2013

Yaliyotokea Arusha yanahitaji Tume Huru


   
 
            Jumamosi ya Juni 15, 2013 Jiji la Arusha kwa mara ya pili ndani ya kipindi kifupi liliendelea kuandika historia ya hatari kwa kutokewa na vitendo vya kigaidi. Vitendo vya kurusha mabomu kwenye mikusanyiko ya watu na kusababisha maafa. Tukio la kwanza lilitokea Mei 5, 2013, katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasit mjini Arusha na kusababisha vifo vya watu watatu. Tukio hilo kwa sasa kesi yake iko mahakamani. Hata hivyo tukio la Jumamosi iliyopita lilitokea kwenye Uwanja wa Soweto mjini Arusha wakati wa mkutano wa kukamilisha kampeni za udiwani wa Chadema. Wasiwasi mkubwa ulizuka katika tukio hilo ni kuhusishwa polisi na vifo vilivyotokea.
     Kubwa zaidi ni kifo cha mtoto Amir Ally (7) anayedaiwa kupigwa risasi na polisi. Maelezo ya kifo cha Ally yamenukuliwa kutoka kwa mtoto mwenzake Abubakar Adam (11), ambaye amelazwa katika Hospitali ya Mount Meru akiuguza majeraha yanayodaiwa kutokana na risasi. Licha ya hao wawili, Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Arusha Medical Lutheran Center (ALMC), Dk Paul Kisanga aliwataja watoto wengine wawili ndugu Fatuma na Sharifa Jumanne ambao wamepelekwa Nairobi, Kenya, kwa matibabu zaidi baada ya miili yao kukutwa na vyuma. Dk Kisanga alimtaja mtoto mwingine Fahad Jamal (7) ambaye yuko chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu (ICU), akisubiri timu ya madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
          Kwa mujibu wa Dk Kisanga watoto hao watano walipatwa na matatizo hayo wakati wakitoka madrasa eneo la Kaloleni (Madrasa ni shule zinatoa elimu ya dini ya Kiislamu), iliyopo jirani na Uwanja wa Soweto. Tukio la Soweto limekuwa na matukio mawili ndani yake; kwanza ni tukio la kurushwa bomu ambalo mtuhumiwa wake hajafahamika, tukio la pili ni matumizi ya silaha za moto ambazo sababu za matumizi yake na wahusika bado ni kitendawili. Hata hivyo, mashuhuda wa tukio hilo akiwamo mtoto Amir Ally wanadai polisi walipiga risasi watu, wengine wanakwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa mtuhumiwa wa bomu hilo alionekana akisafirishwa na gari pale wananchi walipotaka kumvamia.
        Wakuu wa polisi kwa upande wao wamekiri kupatikana kwa maganda ya risasi katika eneo la tukio, hii ina maanisha kwamba ni kweli ndani ya tukio la ulipuaji bomu kulikuwa na tukio lingine la ufyatuaji risasi. Lakini bado hakujawa na ushahidi wa moja kwa moja kwamba nani alifyatua risasi na kwa sababu gani. Madai ya kufyatulia risasi watoto yana uzito wa pekee, pamoja na kutokuwepo kwa ushahidi wa moja kwa moja, vidole vingi vimekuwa vikinyooshwa kuwatuhumu polisi, kwamba risasi zilizofyatuliwa eneo la tukio zilitoka kwa polisi, na watoto walipigwa risasi na polisi. Hata hivyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Said Mwema tayari ameunda timu ya askari polisi kuchunguza tukio hilo ambalo polisi wanatuhumiwa.
       Kwanza tuweke wazi kwamba tuna imani kubwa na utendaji kazi wa Jeshi Polisi, hivyo maoni yetu ni katika kujenga nyumba moja kwa maana tukio la Soweto kwa watoto kupigwa risasi linahitaji Tume Huru itakayokuwa na kada mbalimbali za wataalamu. Tunaamini kuwa hata kama tume iliyoundwa na Mwema itafanya kazi yake kwa uadilifu mkubwa, bado hali ya wasiwasi itaendelea kuwapo kwa kuwa polisi wananyooshewa kidole karibu na watu wengi. Ni vyema Serikali ingeunda Tume Huru.
Source: Mwananchi (June 2013).Yaliyotokea Arusha yanahitaji Tume Huru. Retrieved from Mwananchi

No comments: