TAMKO RASMI CHADEMA UK
CHADEMA UK awali ya yote tunapenda kutoa pole kwa waTanzania na
wapenzi wa CHADEMA waliopatwa na kukutwa na janga la kurushwa kwa bomu kwenye
mkutano wa CHADEMA wa kuhitimisha shughuli za kampeni za uchaguzi wa madiwani
huko Arusha. Tunatuma salam zetu kuwafariji wale wote walioguswa kwa namna moja
ama nyingine katika jambo hili. Kama waTanzania, tunapinga vikali na kukemea kitendo hichi kwa
nguvu zetu zote. Mazingira na jinsi kitendo hichi kilivyotekelezwa tuna kila
sababu ya kuamini kwamba hili ni tendo la kigaidi. Na kwa sababu hiyo ni jukumu
la mamlaka (yaani serikali) na vyombo vyake vya dola kulinda na kuepusha
matendo ya kigaidi kama haya.
CHADEMA ni chama kinachoongozwa na watu makini (effective and
responsible leaders) wenye kuheshimu mamlaka ya sheria za nchi. Wanachama wa
CHADEMA wamekuwa watulivu siku zote wakifuata na kuheshimu sheria kama chama
kinavyowaelekeza. Hata pamoja na kwamba yamekuwepo matendo mengi sana
yanayoashiria kuukandamiza upinzani (hasa CHADEMA) kwa uwazi kabisa, viongozi
wamekuwa mstari wa mbele kuwatuliza wananchi na kuwataka waendelee kuwa na
imani na mamlaka. Hii ni dhahiri kwamba imesaidia kuepusha vurugu kusambaa na
kuiingiza nchi kwenye balaa la vita baina yetu sisi wenyewe.
Japokuwa chama na hasa sisi wanaCHADEMA UK tutaendelea kutafuta
mbinu nyingine katika kupambana na uonevu huu kwa njia ya amani (baadhi kama
tulivyoanisha hapo chini), tunapenda pia kuitahadharisha mamlaka kutokujisahau
(against complacency) kwamba kama hatua za msingi hazitachukuliwa uvumilivu wa
waTanzania utafikia kikomo. Hili ni KARIPIO KALI kwa mamlaka
zinazohusika na kwa sababu hiyo tumechukua hatua zifuatazo:
1. Tumetuma barua ya rasmi ya
ushauri kwa kwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano mh. J.M Kikwete. Pamoja na mambo
mengine tumetoa maoni yetu kama ifuatavyo:
Usalama wa taifa ufanyiwe marekebisho makubwa: Tanzania
Intelligence Services (TIS) inahitaji kufanyiwa marekebisho na ikibidi ivunjwe
na kuwe na vikosi vifuatavyo:
2 Tanzania Secret Intelligence Services
(TSIS): Hii iwe ni mamlaka ya kutafuata, kupata na kusimamia siri za kimataifa
ikiwa ni katika kulinda nchi na mipaka yake. Kwa kushirikiana na vyombo mbali
mbali TSIS itakuwa na jukumu la kupata siri za kijeshi, ugaidi wa kimataifa,
n.k.
o Tanzania Serious Organised Crime Unit
(TSOCU): Kitengo hiki kiwe na wajuzi wa maswala mbali mbali ikiwahusisha Polisi
maalumu, wataalamu wa computer na mawasiliano, na wajuzi wenye uelewa wa
kuchunguza matendo ya kijangili. Kazi kubwa ya kitengo hiki iwe ni kuchunguza
na kuwakamata wahalifu wote wanaofanya matendo ya kijangili ikiwa ni pamoja na
madawa ya kulevya; wizi ndani ya mashirika na taasisi za serikali unaofanywa na
kupangwa na wafanyakazi kwa kushirikiana na watu mbali mbali; Mauaji; n.k. Hata
hivyo kazi nyingine muhimu ya TSOCU iwe ni, kwa kutumia njia za kisasa kabisa,
kugundua mapema na kuzuia uhalifu kutokea. Kama wakipatikana wana usalama wenye
uwezo, kitengo hiki kitaepusha upotevu wa maisha ya watu wasio na hatia kwa
kiwango cha juu. Cha muhimu ni kuhakikisha kitengo hiki kinapatiwa vifaa na
mafunzo ya kisasa kabisa ili kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi.
Kuna umuhimu mkubwa sana wa kuvipa uhuru vyombo hivi vya usalama
kutoka kwa wansiasa. Kwa mfano ilivyo sasa wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa
ndiyo wenyeviti wa kamati za usalama za wilaya na mikoa. Hivi vyote ni vyeo
(appointement) vya kisiasa. Kwa hivyo kama CHADEMA hatuamini kabisa kwamba
vyombo hivi vinaweza kusimamia maswala ya kiusalama kwa haki bila upendeleo wa
kisiasa.
Kazi za jeshi la polisi ziwe za kufanya kazi karibu kabisa na
wananchi katika kusimamia sheria, kulinda wananchi na mali zao, kuzuia uhalifu,
na kuwapunguzia wananchi hofu ya kufanyiwa vitendo vya kihalifu ili kumfanya
kila mwananchi ajisikie huru. Hii itakuwa ni kuhakikisha jamii inaishi kwa
kufuata sheria na taratibu (maintaining public order), kupambana na wahalifu na
kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama.
Hata hivyo jeshi hilo linahitaji kufanyiwa mabadiliko makubwa.
Dosari kubwa zinaonekana dhahiri kuanzia kwenye ngazi za mkuu wa jeshi hilo
nchini (IGP), kwenda chini kwenye ngazi za wakuu wa polisi wa mikoa (RPCs),
wakuu wa vitu (OCSs) na polisi wa kawaida. Kwa mfano mauaji yanapotokea, hakuna
uwajibikaji (accountability). Kwa sababu hiyo kuna umuhimu wa kuzipa nguvu kamati ya ulinzi na
usalama ya bunge ili ziweze kuwaita na kuwahoji wakuu wa usalama ili wajieleze
mbele ya kamati pale inapohitajika.
2. Tumeandika barua kwenda kwenye
ofisi za haki za binadamu (International Human Rights Office) hapa London. Nia
na madhumuni ni kuwapa picha ya vitendo vya kinyama vinavyofanywa na baadhi ya
watu kwa manufaa yao binafsi.
3. Tumetuma barua kwenye balozi
zaidi ya nane za nchi mbali mbali tukiyaeleza na kuyaanisha matukio
yanayoendelea ndani ya nchi huku viongozi wetu wakikaa kimya.
4. Tumevitaarifu vyombo mbali mbali
vya habari kama vile BBC, RT Television na Aljazeer kuhusu hali na mwelekeo wa
kisiasa Tanzania ambao umeanza kuchukua sura mpya.
Kwa nguvu zote tutaendelea kuueleza ulimwengu na kukaripia
uhalifu huu tunaofanyiwa ndani ya nchi. Ni muhimu kwa waTanzania kufahamu
kwamba upinzani siyo dhambi . Upinzani ni mawazo mbadala.
Kwa wana-CHADEMA wenzetu
Tanzania ni nchi yetu tunayoipenda na kuithamini. Tunaamini
kabisa kwamba amani na utulivu ni vitu muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu.
Sote tunatamani kuwarithisha watoto wetu (next generation) nchi itakayowapa
fursa ya kusonga mbele. Hata hivyo amani tunayoiongelea hapa si amani ambayo
tumeaminishwa na serikali ya ccm kwa miaka mingi. Amani tunayoisema ni amani ya
kweli, amani inayoheshimu utu, amani inayompa fursa kila mwananchi kufanya
shuughuli zake bila kuogopa ili mradi anafuata sheria za nchi.
Ni dhahiri kwamba wengi tumechoshwa na uongozi mbovu ambao
tumeifikisha nchi hii hapa tulipo leo. Wengine hata tunashangaa kwamba hawa
hawa ambao wamekuwa madarakani kwa miaka zaidi ya 50 bila kuleta maendeleo
yeyote, leo hii wanaonekana kutaka kung’ang’ania madaraka kwa gharama zozote
zile hata kwa kumwaga damu. Watu hawa wanaonesha uchu na jazba ya hali ya juu
lakini wakiambiwa wajieleze ni nini wamekifanya kwa miaka 50 hawana jibu. Ikiwa
kama haitoshi, wengi tunaona kwamba sasa imetosha, tumeshavumilia vya kutosha
(enough is enough).
Pamoja na hayo tunawaomba tuendelee kutetea bila kuchoka juhudi
za kulikomboa taifa letu. Endeleeni kuwaelimisha na wengine ambao bado
wanahitaji kufumbuka macho. Ukiona hali inafikia hapa ilikofikia, kwa wale
wanaojua kusoma nyakati, watajua kwamba ushindi umekaribia.
No comments:
Post a Comment