*Adai askari alivaa sare za polisi
*Asema wana ushahidi wa mikanda ya video
*Serikali yatangaza bingo ya Sh mil 100
MWENYEKITI wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amefichua siri
kuhusu tukio la mlipuko wa bomu lililotokea jusi katika viwanja vya Soweto,
jijini Arusha. Katika kauli
yake jana, Mbowe ameibua tuhuma nzito dhidi ya Jeshi la Polisi, ambapo alidai
kuwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) ndiye aliyerusha bomu hilo. Akizungumza na
waandishi wa habari mjini hapa,baada ya kutembelea majeruhi katika Hospitali ya
Selian, Mbowe alisema chama chake kina ushahidi wa kutosha juu ya askari huyo
kurusha bomu. Mbowe ambaye
pia ni kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni,alisema wamefanikiwa kupata
ushahidi wa kutosha juu ya tukio hilo baya linalochafua taswira ya nchi.
Alisema chama
chake kipo tayari kuweka ushahidi huo hadharani, iwapo Serikali itaendelea
kufanya siasa na kuficha ukweli. “Tunao
ushahidi wa kutosha, ikiwamo wa picha za video unaoonyesha shambulio la bomu na
risasi lilivyofanyika katika mkutano wangu jusi eneo la Soweto. “Picha zinaonesha
wazi aina ya silaha zilizotumika kwenye shambulio lile ni tatu, bomu la
gurumeti ambalo lilitupwa na askari wa FFU aliyekuwa kwenye uniform. “Kutokana na
ushahidi huu tulikuwa tumewaeleza Polisi kama wataendelea kuficha tutaueleza
umma na tutaiambia dunia, kwani aina ya silaha zilizotumika ni SMG na bastola. “Makasha ya
risasi kama ushahidi wa jambo hili zilizotumika tuliyaokota eneo la tukio na
tayari tumeyarekodi na kuyakabidhi kwa askari waliokuwa wakichunguza tukio
lile,” alisema Mbowe.
Hata hivyo
Mbowe alipinga tamko la Serikali kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Uratibu na Bunge), William Lukuvi na kusema kauli yake ni ya kitoto mbele ya
jamii. “Kauli ya
Serikali kupitia kwa Lukuvi kwamba vurugu zilisababishwa na vikundi, wanasiasa
na mashirika yasiyo ya kiserikali ambavyo havijulikani ni sawa na kuwadhihaki
Watanzania,” alisema. Kutokana na
hali hiyo Mbowe alisema tayari wanasheria wa chama hicho akiwemo Mabere
Marando, Tundu Lissu na Profesa Abdallah Safari wanashughulikia suala hilo. Alisema baada
ya polisi huyo kurusha bomu, alikimbilia katika gari ya Toyota Land Cruizer
yenye rangi ya bluu akiongozana na askari mwenzake ambapo gari hilo liliondoka
kwa kasi, huku likisindikizwa kwa kukingwa na gari ya TDI hadi kituo cha
polisi.
SPIKA
Alisema
anashangazwa na hatua ya Spika wa Bunge Anne Makinda, kushindwa kuguswa na
jambo hilo ambalo limelitikisa taifa na kuruhusu Bunge liendelee. Alisema Spika
Makinda, ameendelea kuongoza Bunge licha ya Hotuba ya Waziri Kivuli wa Fedha
kuwekwa kando kutokana na tukio hilo lililovuta hisisa za watu wengi. “Kila
linapotokea tukio kubwa la mauaji kama haya shughuli za Bunge husimama ili kulishughulikia,
lakini Spika hakushtuka hata pale alipoona wabunge wote wa Chadema hawapo
bungeni.
“Spika Makinda
ameshindwa hata kunipigia simu hata ya kunipa pole kama mbunge niliyenusurika
kuuawa …. Yaani hawajaona sababu sababu ya kufanya hivyo na huenda watu
waliokufa hawana thamani kwao, wameona ni sawa na kuku. “Jeshi la
Polisi, wamekuwa na kazi ya kuchunguza mambo yasiyoisha, inakuwaje waue wenyewe
halafu wajichunguze? msione misafara ya magari ya viongozi yanakuja hapa
hospitali ni unafiki mtupu. “Wanawajua
wauaji, tutayaweka haya yote hadharani sura za wauaji zitaonekana na suala hili
tutalipigania mpaka haki itendeke ikibidi hata mpaka umoja wa mataifa,” alisema
Mbowe.
Hata hivyo,
aliishauri serikali kwa kuiambia kuwa kama haitaki ushindani wa vyama vya
upinzani ni vema ikavifuta vyama vya siasa vilivyopo kulikoni kuendelea kuwaua
wananchi wasio na hatia wakiwemo watoto wadogo wanaposhiriki shughuli za siasa.
SHILINGI
MILIONI 100
Katika hatua
nyingine, Serikali imeamua kutenga Sh milioni 100 kama zawadi kwa mtu yeyote
atakayetoa taarifa zitakazofanikisha kunaswa kwa mhalifu au watu wenye mtandao
wa ulipuaji mabomu. Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, alisema
bungeni mjini hapa jana, kuwa kila mtu mmoja atakayetoa taarifa za siri na za
uhakika kufanikisha kukamatwa kwa mhalifu huyo, atapatiwa Sh milioni 10 “hadi
fedha hizo ziishe na serikali ina uwezo wa kuongeza fedha zaidi hadi mtu huyo apatikane.” Lukuvi,alikuwa
akitoa kauli ya Serikali kuhusu mlipuko uliotokea katika mkutano wa hadhara wa
kampeni za uchaguzi katika Kata ya Sowote, Arusha, Jumamosi iliyopita. Mkutano
huo, ulikuwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Alisema mtu
yeyote atakayetoa taarifa hizo atahakikishiwa usalama wake na polisi. Alisema watu
wawili walikufa katika tukio hilo, ambao ni Judith William (48) na Ramadhani
Juma (15), huku watu 70 wakijeruhiwa, watatu vibaya na kati yao wawili hali zao
ni mbaya. Alisema
uchunguzi wa awali, umeonyesha mlipuko huo ulikuwa wa bomu la kurushwa kwa
mkono, lililorushwa kutoka upande wa mashariki kuelekea magharibi, kulikokuwa
na gari aina Fuso lililokuwa likitumika kuhutubia.
“Jaribio la
polisi kutaka kumfuata aliyerusha bomu hilo lilizuiliwa na makundi ya wananchi,
ambao walianza kuwashambulia polisi kwa mawe na kuwazomea na hivyo polisi
kulazimika kuanza kujiokoa badala ya kumsaka mhalifu huo. “Aina ya
urushaji wa bomu hilo, hautofautiani na mbinu iliyotumika kwenye shambulio
jingine la bomu lililotokea Mei 5, mwaka huu, katika Kanisa Katoliki la Olasiti
katika jiji hilo hilo la Arusha,” alisema.
“Nataka
niwaambie wahalifu hao kuwa njama zao za kutugawa kwa misingi ya dini,
makabila, rangi, rasilimali na itikadi za vyama zitashindwa. “Tutapambana
nao usiku na mchana kwa silaha zote tulizonazo mpaka tutakapowashinda na
kuwafikisha mbele ya mikono ya sheria,” alisema.
MBATIA
Naye
Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), James Mbatia, ameitaka
Serikali kuchukua hatua za haraka kukabiliana na hali ya uvunjifu wa amani
iliyopo nchini. Mbatia alitoa
taarifa hiyo mjini Dodoma jana, wakati akizungumzia tukio la bomu lililotokea
mkoani Arusha. Alisema
imekuwa kawaida ya Serikali yanapotokea matukio ya mauaji kama ya Arusha, kutoa
majibu mepesi. "Zamani
ilikuwa nadra kutokea kwa matukio ya kuuana wenyewe kwa wenyewe, sasa imekuwa
kama utamaduni.
“Hii inatokana
na wenye mamlaka kutoa majibu mepesi ambayo hayana utekelezaji, tunapaswa
kusema na kutenda, vinginevyo nchi inaelekea kubaya," alisema Mbatia. “Kuanzia
matukio ya Mtwara na matukio ya mabomu Arusha, kauli zinazotolewa na Serikali
ni za kubabaisha.
Source: Kimwanga B., Makaranga R., & Sanja D. (June 2013). Mbowe: FFU alirusha bomu. Dodoma. Retrieved from Mtanzania
No comments:
Post a Comment