KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdul-rahman Kinana
amemfungulia kesi Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema), kutokana na
kumtuhumu anajihusisha na ujangili na biashara haramu ya pembe za ndovu.
Kinana amefungua kesi hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam kutokana na kitendo cha Mbunge huyo kutoa tuhuma hizo dhidi yake kwa
nyakati tofauti nje na ndani ya Bunge, pia alikataa kuzikanusha na kumuomba
radhi.
Inadaiwa kuwa Aprili 21 mwaka huu Msigwa ambaye ni Waziri Kivuli
wa Maliasili na Utalii alitoa tuhuma hizo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika
katika Shule ya Msingi Mbuguni wilayani Nyamagana mkoani Mwanza.
Aidha alizitoa bungeni wakati akiwasilisha hotuba ya Kambi ya
Upinzani katika Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka
2013/2014. Katika hati ya madai, Kinana anadai kuwa kutokana na tuhuma hizo
ameharibiwa tabia yake, uaminifu, hadhi yake kitaaluma na weledi na kumfanya
achukiwe na kudharauliwa katika jamii.
Anadai jina lake na heshima ambayo ameijenga kwa muda mrefu,
vimeharibiwa na Msigwa kwa nia mbaya, pia kwa tuhuma hizo anazosisitiza kuwa ni
za uwongo, licha ya kumsababishia maumivu ya kisaikolojia, pia zimemsababishia
hasara ya fedha.
Anadai kuwa kabla ya tuhuma hizo alikuwa katika hatua za mwisho
za mchakato wa mazungumzo ya mradi wa ubia wa kilimo cha mboga na mwekezaji
kutoka kampuni ya nje, lakini tuhuma hizo zimesababisha kampuni hiyo kuvunja
majadiliano hayo.
Kinana anadai kuwa sababu iliyotolewa na kampuni hiyo kuvunja
mazungumzo hayo ni kutajwa kwake na mbunge huyo kuwa ni jangili
anayejishughulisha na biashara hiyo.
Kwa mujibu wa hati ya madai, Mradi huo ulikuwa na thamani ya
Dola za Marekani milioni nne, Hisa za ushiriki wa Kinana zilikuwa ni asilimia
25 katika kipindi cha miaka mitano hivyo anatathmini kuwa amepata hasara ya Sh
milioni 350.
Kinana anaiomba Mahakama hiyo imwamuru Msigwa amlipe fidia ya Sh
milioni 350 kama hasara rasmi, pamoja na fidia ya maudhi na fidia ya hasara
ikiwemo gharama za kesi.
Aidha anaiomba Mahakama imwamuru amlipe riba kwa kiwango
kitakachopangwa na Mahakama, tangu tarehe ya hukumu hadi malipo ya mwisho,
imwamuru kufuta tuhuma dhidi yake na kumuomba radhi kwa kuchapisha katika
magazeti mawili ya Kingereza na mawili ya Kiswahili yanayosambazwa nchini.
Pia Mahakama itoe zuio la kudumu kumzuia Msigwa, au wakala wake
kutoa au kuchapisha taarifa zozote za kashfa dhidi yake. Katika hati ya madai
amenukuu baadhi ya kauli za Msigwa, ikiwemo "Kinana (naomba waandishi wa
habari mnisikie na nyie Usalama wa Taifa mkapeleke habari) hana sifa za kupita
barabarani na kuwaambia Watanzania waiamini CCM. Kinana mikono yake si
misafi."
"Hata kwenye Nassaco, Shirika la Meli Tanzania kuna harufu
ya ufisadi ndani yake; ajibu hoja...Kinana meli zake ndizo zinazohusika kubeba
pembe za ndovu nchini. hajajibu hoja hizo! Kwa siku nchi hii tembo 67 wanauawa.
Hao ndio wanaokifadhili Chama Cha Mapinduzi, halafu wanakuja eti kuwashawishi
Watanzania muwasikilize na kwamba Chama Cha Mapinduzi eti ni kizuri."
".Haya mambo ninayoongea ni hatari kwa sababu haya yote ni
majangili ni organized Crime. Ni mtandao wa Kimafia, uko duniani kote, unaweza
ukatuua lakini wabunge tumesimama tunawatetea..."
HabariLeo
No comments:
Post a Comment