Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Tuesday, June 25, 2013

Kauli ya Pinda inahitaji mjadala wa kitaifa



   
Tangu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda atoe kauli tete Bungeni wiki iliyopita ya kulichochea Jeshi la Polisi liendeleze vipigo na mateso kwa wananchi aliodai wanakaidi sheria za nchi, wamejitokeza baadhi ya watu, wakiwamo mawaziri wakijaribu kuipaka sukari kauli hiyo ili itafsiriwe na kuonekana kama ni ya kuhimiza utiifu wa sheria. Hatari ya kauli hiyo kwa amani na usalama wa wananchi inatokana na ukweli kwamba inaonyesha kama vile nchi yetu inatawaliwa kijeshi. Kinyume chake, nchi yetu inaongozwa na Katiba, kwa maana kwamba Serikali iliyopo madarakani ilichaguliwa na wananchi kupitia sanduku la kura. Haikupatikana kwa mtutu wa bunduki na mapinduzi ya kijeshi.
        Kwa maana hiyo, Katiba ya Tanzania na sheria zilizotungwa na Bunge ni mwongozo kwa watawala kuhusu namna ya kuendesha Serikali kwa njia za kidemokrasia na kuhakikisha usalama wa raia na mali zao. Anapotokea kiongozi wa juu wa Serikali akalichochea Jeshi la Polisi kuvunja Katiba na sheria za nchi kwa kufanya vitendo vinavyosababisha hofu na kuhatarisha amani na maisha ya raia lazima wananchi wapaze sauti, wamlaani kwa nguvu zote na wamwambie ‘hapana’. Kauli ya Waziri Mkuu Pinda inatia hofu, hasa inapotolewa kwa Jeshi la Polisi lenye muundo uliorithiwa kutoka kwa wakoloni. Tofauti na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambalo mwaka 1964 lilifanyiwa mabadiliko makubwa kutoka jeshi la kikoloni na kuwa jeshi la wananchi, Jeshi la Polisi tulilorithi kutoka kwa wakoloni lilibakia hilohilo kimuundo na kwa kiasi kikubwa kisera.
     Kimsingi ni Jeshi lililoundwa kupokea amri na kutekeleza matakwa ya watawala ya kuwakandamiza wazalendo, hata kama wazalendo hao wanadai haki zao za kiraia na kikatiba kama Jeshi la Polisi la Makaburu wa Afrika Kusini lilivyokuwa likiwaua na kuwatesa wazalendo waliokuwa wakipinga ubaguzi wa rangi. Ndiyo maana hapa nchini umekuwapo uhasama mkubwa kati ya jeshi hilo na wananchi. Watawala wanaonekana kufurahia hali hiyo ambayo tayari imesababisha vifo na mateso kwa raia wasiokuwa na hatia. Waziri Mkuu anasema jeshi hilo lazima liwapige wananchi anaodai wanakaidi amri halali ya Polisi. Tunauliza amri halali ya Polisi ni ipi? Kupiga marufuku mikutano ya vyama vya upinzani na kuisambaratisha kwa mabomu na silaha za kivita bila sababu za msingi ni amri halali ya wapi? Tunasema hiyo siyo amri halali na inakwenda kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 inayovitaka vyama hivyo kutoa tu taarifa ya mikutano hiyo kwa Polisi ndani ya saa 24 ili vipatiwe ulinzi. Jeshi hilo sasa limejipachika madaraka ya kutoa vibali, kukataa ama kukubali kwa kutoa masharti ya ajabu. Je, hayo ni maagizo ya chama tawala na serikali yake?
       Sisi tunasema kauli ya Waziri Mkuu Pinda inahitaji mjadala wa kitaifa. Ni kauli hatari. Tuikatae, kwani inalenga kuhatarisha amani na umoja wetu. Jaji mstaafu Mark Bomani juzi alionyesha njia alipotahadharisha Serikali na jeshi hilo dhidi ya kutumia nguvu kubwa kukabiliana na umma kwa kutumia silaha za moto. Alionyesha wasiwasi kama kweli Polisi wana uelewa mzuri wa sheria kuhusu matumizi ya silaha za moto au wanafanya kazi kwa kuagizwa tu. Tunahitaji sauti nyingi kama hiyo.
Source: Mwananchi (June 2013).Kauli ya Pinda inahitaji mjadala wa kitaifa. Retrieved from Mwanacnhi

No comments: