Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora

Wasiliana nasi : chademadiaspora@gmail.com -Fair and Balanced Platform- Twitter @ChademaDiaspora
----------------------WE THANK AND APPRECIATE YOU FOR VISITING CHADEMA DIASPORA BLOG. AGAIN, THANK YOU!-----------------------

Sunday, June 23, 2013

CHADEMA yataka Pinda awajibishwe


       CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kanda ya Ziwa Magharibi, kimelitaka Bunge kumjadili na kumwajibisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutokana na kauli yake ya kubariki polisi kupiga raia. CHADEMA imesema kauli ya Pinda imelenga kuchochea uvunjifu wa amani nchini, hivyo ni vema Bunge likachukua hatua zinazostahili kwa kiongozi huyo, ili kulinusuru taifa na machafuko yanayoweza kutokea kutokana na agizo hilo. Katibu wa CHADEMA Kanda ya Ziwa Magharibi, Robert Bujiku pamoja na ofisa mwingine wa chama hicho Kanda ya Ziwa, Tungaraza Njugu, walitoa kauli hiyo juzi walipozungumza na waandishi wa habari mjini hapa.

       Bujiku alisema kauli za namna hiyo zinastahili kulaaniwa ndani na nje ya Bunge, kwani zimelenga kuchochea mapambano baina ya raia wanaoona wanaonewa na Jeshi la Polisi. “Kwanza CHADEMA Kanda ya Ziwa Magharibi tunalaani sana kauli ya Waziri Mkuu Pinda kuruhusu polisi kupiga raia. Kauli ya Pinda imelenga uchochezi unaoweza kusababisha machafuko nchini. “Kwa hiyo, tunawaomba wabunge bila kujali itikadi zao za vyama, wamjadili na ikiwezekana wamwajibishe kutokana na kauli yake hiyo,” alisema Bujiku. Naye Njugu alisema kauli ya Pinda imedhihirisha udhaifu wa Serikali ya CCM, hivyo wananchi hawana budi kuichagua CHADEMA mwaka 2015, ili kiongoze dola kwa maslahi ya wote.


     “Kwa kweli, kauli ya Pinda imedhihirisha udhaifu wa Serikali ya CCM katika kuwaongoza Watanzania. Sasa tunajiuliza Tanzania imeanza kuongozwa kidikteta badala ya kidemokrasia? “Na hii inaonesha pengine hata matukio ya mauaji ya mwandishi Daud Mwangosi, utekaji na uteswaji wa Mhariri, Absalom Kibanda na Dk. Steven Ulimboka ni maagizo ya Serikali. CHADEMA hatutakubali uonevu wa aina yoyote,” alisema Tungaraza.

       Alhamisi ya wiki iliyopita, Pinda akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM), aliyehoji kama serikali ipo tayari kutoa tamko juu ya vurugu zilizotokea mjini Arusha, Mtwara na maeneo mengine pamoja na hatua ya vyombo vya dola kutumia nguvu, kiongozi huyo alibariki polisi kupiga raia wanaokaidi amri. “Sasa kama wewe umekaidi, hutaki, unaona kwamba ni imara zaidi, wewe ni jeuri zaidi, watakupiga tu, na mimi nasema wapigwe tu maana hakuna namna nyingine, tumechoka,” alikaririwa Pinda akisema bungeni.

Source: Tumma S. (June 2013). CHADEMA yataka Pinda awajibishwe. Retrieved from Tanzania Daima

No comments: